Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19 na machafuko vyaendelea kutawanya watu Burkina Faso:IOM

Zore Yusef wakila chakula na mmoja wa watoto wake.Mzozo wa silaha ulilazimisha familia yake kukimbia mkoa wa kaskazini wa Burkina Faso.
WFP/Marwa Awad
Zore Yusef wakila chakula na mmoja wa watoto wake.Mzozo wa silaha ulilazimisha familia yake kukimbia mkoa wa kaskazini wa Burkina Faso.

COVID-19 na machafuko vyaendelea kutawanya watu Burkina Faso:IOM

Wahamiaji na Wakimbizi

Zaidi ya watu milioni moja wametawanywa na kuwa wakimbizi wa ndani na machafuko yaliyozuka upya nchini Burkina Faso,  kwa mujibu wa ripoti ya mwezi Agosti ya baraza la taifa kwa ajili ya masuala ya dharura na misaada (CONASUR). 

 

Shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM, linasema idadi hiyo ni ongezeko la asilimia 100 ukilinganisha na takwimu za mapema mwaka huu wa 2020 ambapo Burkina Faso ilikuwa na wakimbizi wa ndani 450,000. 

Abibatou Wane mkuu wa IOM nchini Burkina Faso amesema “mtu 1 kati ya 20 nchini humo hivi sasa ni mkimbizi wa ndani na ni idadi inayotisha. Idadi kubwa ya wakimbizi hawa wa ndani ni wanawake na watoto na mahitaji yao ni makubwa sana hususan wakati huu wa janga la corona au COVID-19 ambalo limesababisha madhila zaidi kwa mgogoro ambao ulikuwa tayari ni mbaya janga kubwa la kibinadamu.” 

Ameongeza kuwa majimbo yaliyoko ukanda wa Sahel likiwemo Sanmatenga, Soum, Bam, seno na Namentenga yanasalia kuwa maeneo kitovu cha watu waliotawanywa. 

Bwana Wane amesema “hali na mahitaji ya jamii zilizotawanywa yanahitaji msaada mkubwa kutoka kwa wadau mbalimbali ili kusaidia maelfu kwa maelfu ya watu ambao wamepoteza kila kitu au karibu kila kitu walipokimbia machafuko na kuziacha nyumba zao ili kuokoa maisha yao.” 

Wakimbizi wa ndani ambao huzikimbia nyumba zao kutokana na tishio la mashambulizi ya silaha mara nyingi huwa wanaenda kusaka usalama. 

Baraza la CONASUR limesema kipaumbele chake ni mahitaji ya lazima ya watu hao ambayo ni Pamoja na malazi, chakula, huduma za afya, fedha kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya dharura na ajira. 

Fatima ni mmoja wa wakimbizi hao wandani ambaye kwa sasa anaishi kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani ya Youba kwenye jimbo la Kaskazini kwa miezi saba sasa anasema “wengi wetu ni wanawake na tunalea Watoto wetu wenyewe. Tunahitaji msaada ili kutusaidia kufanya shughuli zitakazoweza kutuingizia kipato tuweze kutunza watoto wetu.” 

Ndoto za Fatima hivi sasa ni kujenga upya maisha yake kwa usalama na utu. 

IOM kwa msaada wa washirika wake inafanya kazi kwa karibu na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa kusaidia watu katika majimbo ya Sahel, Kaskazini, Katikati na kaskazini na Kaskazini na Mashariki mwa Burkina Faso. 

Msaada unaotolewa na IOM kwa jamii hizo ni Pamoja na malazi ya dharura kwa wakimbizi wa ndani na msaada wa kisaikolojia, lakini pia kuendesha mafunzo ya ujenzi wa amani na shughuli za kuunganisha jamii. 

Na kama sehemu ya kupambana na COVID-19, IOM pia inasaidia vituo vya afya 34 katika majimbo ya Kaskazini na Sahel kwa kuwagawia vifaa vya kujikinga na vya usafi na kuendesha shughuli za uelimishaji kwa faida ya wakimbizi wa ndani na jamii zinazowahifadhi. 

Mwezi Juni mwaka huu IOM ilitoa ombi la dola milioni 37.8 ili kusaidia kwa msaada wa kuokoa Maisha kwa watu 460,000 nchini Burkina Faso, Mali na Niger.