Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Fedha zitumwazo na wahamiaji makwao zazidi misaada rasmi ya maendeleo 

Fedha zinazotumwa na wahamiaji waishio ugaibuni kwa  jamii nyumbani zinasaidia watu milion 800 ulimwenguni kote
Picha-IFAD
Fedha zinazotumwa na wahamiaji waishio ugaibuni kwa jamii nyumbani zinasaidia watu milion 800 ulimwenguni kote

Fedha zitumwazo na wahamiaji makwao zazidi misaada rasmi ya maendeleo 

Ukuaji wa Kiuchumi

Kiwango cha fedha zinazotumwa na wanafamilia kutoka ughaibuni kwenda katika nchi zao ni mara tatu zaidi ya misaada rasmi ya maendeleo, au ODA ambayo mataifa hayo hupokea kama msaada kutoka nchi zinazoendelea, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres hii leo katika ujumbe wake wa siku ya kimataifa ya utumaji wa fedha kwa familia. 

Guterres amesema fedha hizo husaidia kupunguza umaskini, kuimarisha afya na elimu na kusongesha usawa wa kijinsia. 

Siku hii imeanzishwa na Umoja wa Mataifa mahsusi kutambua mchango wa mamia ya mamilioni ya wafanyakazi wahamiaji kwa jamii ambako wametoka. 

Fedha ni mhimili wa familia 

Katibu Mkuu amesema fedha hizo siyo tu ni chanzo kikuu cha kipato kwa familia, bali pia huchangia kwa kiasi kikubwa katka pato la ndani la taifa, GDP, ambako fedha hizo zinapokelewa hususan nchi za kipato cha chini na cha kati. 

Ni kwa kutambua umuhimu huo ndio maana maudhui ya siku hii leo ni “kujikwamua na kujenga mnepo kupitia ujumuishwaji kidijitali na kifedha,” amesema Katibu Mkuu akiongeza kuwa takribani nudu ya wakazi wa dunia hawana uwezo wa kupata intaneti na hivyo kushindwa kupokea fedha kutoka kwa jamaa zao. 

“Janga la coronavirus">COVID-19 limeongeza pengo la kidijitali. Tunapaswa kusongesha kasi ya kuhakikisha kila mtu yuko mtandaoni, huku tukiwekeza pia katika mbinu za ujumuishaji kifedha na kidijitali,” amefafanua Guterres. 

Gharama za utumaji fedha zipunguzwe hadi karibu na asilimia 0 

Sambamba na hilo ametaka gharama za utumaji zipunguzwe karibia na kufutwa kabisa ili kusaidia familia ziweze kumudu majukumu yao kwa ufanisi. 

Amekumbusha kuwa vita ya Ukraine nayo pia inaathiri utumaji wa fedha na hivyo kuchochea kuenea kwa ongezeko la gharama za maisha. 

“Nchi zinavyoelekeza misaada yao ya maendeleo ili kukidhi mahitaji ya lazima, suala la kulinda hoja ya utumaji fedha kwa familia ni muhimu,” amesema Guterres kwa kuwa litaimarisha mnepo, kuchochea ukuaji uchumi na mtangamano wa kijamii. 

Ni kwa mantiki hiyo amesema katika siku hii ya utumaji fedha kwa familia, “hebu turejelee upya ahadi yetu ya kutomwacha yeyote nyuma katika kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.”