Kila mtu anapaswa kutambua thamani halisi ya maji katika maisha :Guterres

22 Machi 2021

Ikiwa leo ni siku ya maji duniani , Katibu Mkuu wa Umoja wa Mastaifa Antonio Guterres amesema upatikanaji wa maji ni kinga dhidi ya maradhi,utu na changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi na hasa panapokuwa na mzunguko unaosimamiwa vizuri wa maji ukijumuisha maji ya kunywa, usafi wa mazingira na kujisafi, maji taka, na mambo menghine muhimu.

Kupitia ujumbe wake maalum wa siku hii amesema “Hebu tujitolee kuongeza juhudi za kimataifa ili kuhakikisha wote wanaweza kupata usawa wa rasilimali hii ya thamani zaidi duniani. Hii inamaanisha kwamba kuchukua hatua za kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi na ongezeko la mahitaji ya rasilimali hiyo kote duniani”

Ameongeza kuwa hoja ya msingi ni kutambua thamani halisi ya maji, ili kuweza kuilinda vyema rasilimali hiyo muhimu kwa kila mtu na kwa kila sababu hasa wakati huu mgogoro wa uhaba wa maji ukiongezeka duniani.

Maudhui ya siku ya maji mwaka huu ni “Thamani halisi ya maji”.

Leo hii duniani karibu mtu 1 kati ya 3 anakosa fursa ya maji safi ya kunywa na kuna hofu kwamba ifikapo mwaka 2050 takribani watu bilioni 5.7 watakuwa wanaishi katika maeneo ambako maji ni haba kwa angalu mwezi mmoja kwa mwaka.

Zaidi yah apo inakadiriwa kwamba ifikapo mwaka 2040 mahitaji ya maji duniani yataongezeka kwa zaidi ya asilimia 50 na kuongerza shinikizo Zaidi kwa rasilimali hiyo muhimu.

Maudhui ya siku ya maji mwaka huu ni “Thamani halisi ya maji”

Mtoto akioga katika mtaa wa mabanda wa Kallyanpur kwenye mji mkuu wa Bangladesh, Dhaka.
UN Photo/Kibae Park
Mtoto akioga katika mtaa wa mabanda wa Kallyanpur kwenye mji mkuu wa Bangladesh, Dhaka.

Kuzuia upotevu na matumizi mabaya

Kwa mujibu wa ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa, moja ya sababu kuu za upotezaji wa maji na matumizi mabaya ni kutoweza kutambua thamani ya maji.

"Kutambua, kupima na kuonyesha thamani ya maji, na kuyajumuisha katika kufanya maamuzi, ni muhimu katika kufanikisha usimamizi endelevu na usawa wa rasilimali za maji", iimesema ripoti hiyo, iliyopewa jina “Kuthamini maji”. 

Ripoti hiyo iliyozinduliwa sanjari na maadhimisho ya siku ya maji duniani  pia inatoa mwongozo bora na uchambuzi wa kina ili kuchochea maoni na vitendo vya usimamizi bora katika sekta za maji na zinazohusiana.

Bango katika shule moja nchini Sudan Kusini likisema "Bila maji hakuna uhai"
UNICEF/Helene Sandbu Ryeng
Bango katika shule moja nchini Sudan Kusini likisema "Bila maji hakuna uhai"

Maji na maendeleo endelevu

Katika ujumbe wake, Bwana Guterres alisisitiza kwamba maji na maendeleo endelevu yanahusiana sana.

"Kimsingi hakuna kipengele cha maendeleo endelevu ambacho hakitegemei maji", amesema.

Kuhakikisha upatikanaji na usimamizi endelevu wa maji na usafi wa mazingira kwa wote, pia ni moja wapo ya malengo ya maendeleo endelevu (SDGs), ambayo nchi zimejitolea kuyafikia ifikapo mwaka 2030. 

Amesisitiza kwamba wakati hatua za maendeleo zimepigwa kiasi kuelekea Lengo hili, kasi inahitaji kuongezeka mara nne ili kulitimiza.

“Uwekezaji mdogo wa muda mrefu katika upungufu wa maji na usafi wa mazingira na unaathiri idadi kubwa ya watu. Hii haikubaliki ”, mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema, akitoa wito kwa kila mtu" kujitolea kuimarisha juhudi za kuthamini kweli maji ili wote waweze kupata usawa wa rasilimali hii ya thamani zaidi. "

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter