Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Asilimia 6 tu ya wafanyakazi wa majumbani duniani ndio wenye ulinzi wa hifadhi ya jamii:ILO 

Wafanyakazi wa majumbani hawana uhifadhi wa jamii
UN Women/Joe Saad
Wafanyakazi wa majumbani hawana uhifadhi wa jamii

Asilimia 6 tu ya wafanyakazi wa majumbani duniani ndio wenye ulinzi wa hifadhi ya jamii:ILO 

Ukuaji wa Kiuchumi

Katika siku ya kimataifa ya wafanyakazi wa majumbani ripoti mpya iliyotolewa leo na shirika la kazi duniani imesema ni asilimia 6 pekee ya wafanyakazi hao ndio wenye ulinzi wa hifadhi ya jamii na hivyo kuwaacha asilimia 94 ya wafanyakazi hao kote duniani wakikosa fursa ya ulinzi muhimu wa kijamii unaojumuisha matibabu, magonjwa, ukosefu wa ajira, uzee, ajali kazini, familia, malipo ya uzazi, ulemavu na marupurupu mengine. 

Kwa mujibu wa ILO wafanyakazi wa majumbani wana mchango muhimu katika jamii wa kutoa huduma muhimu kwa familia na kaya lakini bado mchango wao hauthaminiwi vya kutosha. 

Ripoti hiyo, “Kuhakikisha hifadhi ya jamii inafanya kazi pia kwa wafanyakazi wa majumbani: Mapitio ya kimataifa ya mwelekeo wa sera, takwimu na mikakati”, karibu nusu ya wafanyakazi wote wa majumbani hawana ulinzi kabisa, na nusu iliyobaki inalipwa kisheria angalau huduma moja. 

Upanuzi wa wigo wa ulinzi wa hifadhi ya jamii bado ni mtihani 

Shirika hilo la kazi la Umoja wa Mataifa limesema upanuzi wa wigo madhubuti wa hifadhi ya jamii kwa kundi hilo bado umesalia nyuma kwa kiasi kikubwa kisheria.  

“Ni mfanyakazi 1 kati ya 5 pekee ndiye anayeshughulikiwa kwa vitendo kwa sababu wengi wao wameajiriwa kwa njia isiyo rasmi.” Limeongeza shirika la ILO Licha ya mchango wao muhimu kwa jamii, kusaidia kaya zilizo na mahitaji yao ya kibinafsi na ya utunzaji, wengi wa wafanyikazi milioni 75.6 wa majumbani kote duniani wanakabiliwa na vizuizi vingi vya kufurahia huduma za kisheria na ufikiaji mzuri wa huduma za hifadhi ya jamii, ripoti inaeleza na kuongeza kuwa mara nyingi hawajumuishwi katika sheria za hifadhi ya jamii za kitaifa. 

“Kwa kuwa asilimia 76.2 ya wafanyakazi wa majumbani (watu milioni 57.7) ni wanawake, mapengo hayo ya ulinzi wa kijamii huwaacha wanawake katika hatari zaidi.” Imesema ripoti. 

Ripoto imeongeza kuwa ingawa ni wafanyakazi wachache wa majumbani wanaofurahia ulinzi wa kina wa hifadhi ya jamii, wana uwezekano mkubwa wa kustahiki huduma za matibabu ya uzeeni, ulemavu na manusura, na kwa kiwango kidogo, huduma za uzazi na magonjwa.  

Wengi wao hawana fursa ya huduma za bima za kijamii zinazohusiana na ukosefu wa ajira au ajali kazini. 

Myanyakazi wa ndani akifua nguo kwa mikono mjini Delhi India (Picha toka maktaba)
ILO/B. Patel
Myanyakazi wa ndani akifua nguo kwa mikono mjini Delhi India (Picha toka maktaba)

Tofauti baina ya kanda 

Ripoti hiyo pia inaangazia tofauti kubwa kati ya kanda mbalimbali ikisema katika Ukanda wa Ulaya na Asia ya Kati, asilimia 57.3 ya wafanyakazi wa majumbani wanalipwa kihalali mafao yote.  

Huku zaidi kidogo ya asilimia 10 wana haki kama hiyo katika bara la Amerika, wakati katika mataifa ya nchi za Kiarabu, Asia na Afrika karibu hakuna kabisa huduma zinazoshughulikiwa kikamilifu licha ya kuwa ni maeneo ambayo yanajumuisha nchi ambazo zina idadi kubwa ya wafanyakazi walioajiriwa majumbani. 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya ILO janga la coronavirus">COVID-19 limeongeza zaidi mapungufu ya ulinzi wa hifadhi ya jamii inayopatikana na wafanyikazi wa majumbani.  

“Wafanyakazi hao walikuwa miongoni mwa walioathirika zaidi wakati wa janga hilo, huku wengi wakipoteza kazi na maisha yao. Wengi wa wale ambao waliendelea kufanya kazi mara nyingi walikabiliwa na ugonjwa huo bila kuwa na vifaa vya kutosha vya kujikinga. Hata hivyo, wafanyakazi wa majumbani hawakuweza kutegemea ulinzi wa kutosha wa huduma za afya, magonjwa au ukosefu wa ajira, na hivyo kuanika hatari inayowakabili” Imesema ripoti 

Changamoto za kuhakikisha ulinzi wa hifadhi ya jamii kwa wafanyakazi wa majumbani ni dhahiri lakini sio zinazoshindwa kukabilika ripoti imesema.  

Imebainisha viwango vya kimataifa vya ajira ambavyo vinatoa suluhisho.  

Viwango hivyo ni pamoja na Mkataba wa wafanyakazi wa majumbani wa mwaka 2011 (Na. 189), pendekezo la mwaka 2011 (Na. 201) , mapendekezo ya Ulinzi wa hifadhi ya Jamii, ya mwaka 2012 (Na. 202) na Hifadhi ya jamii (Viwango vya chini)  ya mwaka 1952 . 102). 

Mapendekezo ya ripoti 

Ripoti hiyo inatoa mapendekezo ya jinsi ya kuhakikisha wafanyakazi wa majumbani wanafurahia ulinzi wa kina wa hifadhi ya jamii, ikiwa ni pamoja na: 

• Kuhakikisha kwamba wafanyakazi wa majumbani wanafurahia hali muhimu za hifadhi ya jamii kama ilivyo kwa wafanyakazi wengine. 

• Kubadili na kurahisisha taratibu za usimamizi ili kuhakikisha kwamba maelezo ya kisheria yanatafsiriwa kwa vitendo. 

• Kurahisisha na kuhuisha taratibu za usajili na malipo na kuandaa mbinu za kutosha za ufadhili. 

• Kuunda mifumo ya mafao ili kuendana na kazi za majumbani. 

• Kuchagiza huduma za ukaguzi pamoja na njia za kufikisha malalamiko na rufaa ili kuhakikisha utiifu wa sheria na kanuni. 

• Kuongeza ufahamu miongoni mwa wafanyakazi wa majumbani na waajiri wao kuhusu haki na wajibu wao. 

• Kuchagiza uwepo wa mbinu shirikishi na jumuishi za sera.