Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tanzania: UN yahofia ghasia kutokana na madai ya kumegwa kwa ardhi ya asili ya wamasai

Nyumbu wakiwa kwenye bonde la Ngorongoro huko Arusha nchini Tanzania
© Unsplash/Ray Rui
Nyumbu wakiwa kwenye bonde la Ngorongoro huko Arusha nchini Tanzania

Tanzania: UN yahofia ghasia kutokana na madai ya kumegwa kwa ardhi ya asili ya wamasai

Haki za binadamu

Wataalam wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wameeleza hofu yao juu ya madai ya kuendelea kumegwa kwa ardhi ya asili ya wamasai huko Loliondo kaskazini mwa Tanzania.

Taarifa ya wataalamu hao 9 iliyotolewa leo jijini Geneva, Uswisi inasema kitendo hicho kinachoambatana na ukosefu wa uwazi na mashauriano na wamasai wakati wa mipango na uamuzi hivi karibuni kimehusisha pia matumizi ya vikosi vya usalama dhidi ya watu hao wa jamii ya asili wakati wakilinda eneo lao la kiasili.

Chanzo cha wasiwasi wa wataalamu 

“Tuna wasiwasi mkubwa na ripoti za vikosi vya usalama vya Tanzania kutumia risasi za moto na mabomu ya kutoa machozi tarehe 10 mwezi huu wa Juni, kitendo kinachoripotiwa kusababisha watu takribani 30 kupata majeraha madogo na wengine makubwa sambamba na kifo cha afisa mmoja wa polisi,” wamesema wataalamu hao.

Kwa mujibu wa wataalamu hao, tarehe 6 mwezi huu wa Juni, baada ya mashauriano ya faragha, Mkuu wa Mkoa wa Arusha alitangaza uamuzi wa kugeuza eneo la ukubwa wa kilometa 1,500 za mraba kutoka eneo la kilometa 4,000 za mraba la ardhi ya vijii linalojumuisha eneo la pori tengefu la Loliondo kuwa pori tengefu.

Tweet URL

Wataalamu hao wamesema mabadiliko hayo yanamaanisha kuwa wakazi 70,000 wa vijiji vya Ololosokwan, Oloirien, Kirtalo, na Arash villages,watalazimika kuhama.

Halikadhalika wamezungumzia pia eneo la Ngorongoro ambako wamesema, “tuna hofu juu ya mipango ya Tanzania ya kuhamisha wamasai 150,000 kutoka eneo la hifadhi la Ngorongoro pamoja na Loliondo bil aridhaa yao au kujulishwa na kuamua kwa mujibu wa sheria za haki za kibinadamu za kimataifa,” huku wakitaka Tanzania isitishe mpango huo.

Kwa mujibu wa wataalamu hao, tarehe 22 mwezi huu wa Juni, Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki itatoa uamuzi wake kuhusu zuio la kisheria dhidi ya kuondolewa kwa wamasai kutoka maeneo yao.

Mgao wa maeneo  umetokana na mashauriano- Tanzania

Hoja hizo zilijibiwa kwenye Mkutano wa 50 wa Baraza la Haki za binadamu la Umoja wa Mataifa, jijini Geneva, Uswisi na Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania kwenye ofisi ya Umoja wa Mataifa huko Geneva, Balozi Hoyce Temu.

“Baada ya serikali na jamii ya wakazi wa Loliondo kujadiliana na kukubaliana, kuwa kati ya kilometa za mraba 4,000 zilizopakana na vijiji 14, ilikubaliwa kuwa kilometa za mraba 2,500 zitumiwe na vijiji vya karibu kwa kujikimu kimaisha, na kilometa za mraba 1,500 ziwe kwa ajili ya uhifadhi chini ya serikali ya Tanzania au kwa jina jingine iwe pori tengefu,” amefafanua Balozi Temu.

Naibu Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania kwenye ofisi za Umoja wa Mataifa huko Geneva, Uswisi, Balozi Hoyce Temu akihutubia mkutano wa 50 wa Baraza la Haki za Binadamu la UN huko Geneva, USwisi.
UN News
Naibu Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania kwenye ofisi za Umoja wa Mataifa huko Geneva, Uswisi, Balozi Hoyce Temu akihutubia mkutano wa 50 wa Baraza la Haki za Binadamu la UN huko Geneva, USwisi.

 

Amesema alama za mipaka zimeanza kuwekwa kwenye pori hilo tengefu la Loliondo, “lakini watu wachache wenye nia mbaya ya mpango kamambe wa Tanzania wa kuwapatia maisha bora wakazi wa Loliondo na wakati huo huo kuendelea kuhifadhi eneo hilo kwa maendeleo endelevu, walianza kuandamana na kupinga mpango huo.”

Balozi Temu amesema “katika hatua hiyo, baadhi ya waandamanaji walichukua picha na kuchanganya na picha ambazo hazikuwa za eneo hilo.”

Hakuna aliyejitokeza kufuatia madai ya uvamizi au kuumizwa

Naibu Mwakilishi huyo wa Kudumu wa Tanzania amesema, “serikali imeitisha wale wanaodai kuvamiwa ama kuumizwa ili sheria ichukue mkondo wake, lakini hadi sasa hakuna aliyejitokeza na wananchi wa Loliondo wanaendelea na maisha yao kawaida na kwa amani.”

Amesisitiza kuwa serikali itaendelea na majadiliano kuhakikisha wananchi wananufaika kiuchumi na kijamii na wawe na haki katika kufaidi ardhi yao kwani ni watanzania kama walivyo watanzania wengine huku ikiona uhifadhi endelevu unaendelea kwa manufaa ya nchi na wananchi wake.

Mwaka 2010, eneo la hifadhi ya Ngorongoro lilitambuliwa na shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO kuwa eneo la urithi wa dunia.