Watu wenye ulemavu wakumbukwe katika suala la utalii-Mbunge Tanzania

Mkutano wa 12 wa nchi wanachama wa mkataba wa haki za watu wenye ulemavu, CRPD, ukiingia wiki yake ya pili hii leo katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani, wadau wanaendelea kujadili mikakati mbalimbali ya kuhakikisha ahadi ya kutomwacha yeyote nyuma inatekelezwa.
Miongoni mwa washirii ni Riziki Saidi Lulida, mbunge katika Bunge la Jamhuri ya muungano Tanzania ambaye anapigania haki mbalimbali za watu wenye ulemavu . Nilipata fursa ya kuzungumza naye kando ya mkutano huu kuhusu mkakati wake wa sasa wa kuhakikisha watu wenye ulemavu kama yeye hawaachwi katika suala la utalii na akaanza kwa kunieleza haki ambazo amekuwa akizipigania na namna anavyoisukuma ajenda yake ya sasa, « Haki ya elimu, haki ya afya, hali ya mazingira, lakini sasa hivi tumekuja kusimamia sana haki za wenye ulemavu katika suala la michezo na utalii. Manake nilikuwa nimeshawahi kuhudhuria mikutano mbalimbali hapa UN nikaona matukio mablimbali yanaletwa kuhusu suala la utalii lakini sisi Tanzania lile dawati la utalii kwa walemavu lilikuwa halijaanzishwa. Mimi katika bunge nikasema ni lazima serikali lazima isimamie suala la utalii na walemavu. Mfano hivi karibuni ilikuja meli ya watalii wanaozunguka Dunia lakini walipofika Dar es Salaam walishindwa kutembelea jiji hilo kwakuwa kulikosekana miundombinu wezeshi.”
Hata hivyo Bi Riziki anasema anaendelea kupata moyo wa kuendeleza hamasa kwani juhudi zake na wenzake zimeanza kufanyiwa kazi na serikali ya Tanzania, « Kwa mfano serengeti mwaka huu imeshinda kuwa mbuga ya pili duniani lakini ya kwanza Afrika kwa huduma nzuri. Ngorongoro nayo imepata heshima kubwa sana kwasababu wana huduma nzuri kwa watalii, lakini hapo awali hakukuwa na dawati la wenye ulemavu, kwa hivyo tulivyokuja hapa ni kuwahamasisha watalii kuwa sasa Tanzania tuna dawati la watu wenye ulemavu. Kuna watalii wametoka Afrika kusini na mwingine hapa Marekani wameweza kufika kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro. Hii inaonesha watalii wanavyoweza kutembelea Kilimanjaro, Ngorongoro na Zanzibar. »
Umoja wa Mataifa tayari umezindua mkakati wake wa ujumuishi wa watu wenye ulemavu katika nyanja mbalimbali kama mojawapo ya hatua za kutekeleza kwa vitendo kwa mfano ahadi yake ya kutomwacha nyuma mtu yeyote kwenye utekelezaji wa ajenda 2030.