Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mabadiliko ya tabiachi yaanza kubadilisha maisha ya jamii ya Maasai, Loliondo, Tanzania

Kutokana na mabadiliko ya tabianchi, jamii ya wafugaji, Maasai wa Loliondo kaskazini mwa Tanzania wamelazimika kuhamia katika kilimo.
Mathias Tooko
Kutokana na mabadiliko ya tabianchi, jamii ya wafugaji, Maasai wa Loliondo kaskazini mwa Tanzania wamelazimika kuhamia katika kilimo.

Mabadiliko ya tabiachi yaanza kubadilisha maisha ya jamii ya Maasai, Loliondo, Tanzania

Tabianchi na mazingira

Watu jamii ya Maasai huko Loliondo, wilaya ya Ngorongo, Tanzania ambao kwa miaka yote ya uwepo wao shuguli yao ya kujipatia kipato na chakula ni kupitia mifugo hususani ng’ombe, na chakula chao ni nyama na maziwa, sasa wameanza kulazimika kuanza kuhamia katika shughuli za kilimo baada ya shughuli yao hiyo ya  asili ufugaji kuathiriwa na mabadiliko ya tabianchi. 

Mwishoni mwa mwaka jana 2021, mwezi Novemba, wakuu wa nchi, viongozi wa Umoja wa Mataifa, mashirika ya kiserikali na yasiyo ya kiserikali pamoja na wadau wa mazingira kutoka kila pembe ya dunia walikusanyika mjini Glasgow Scotland kujadili namna ya kuiokoa dunia na mabadiliko ya tabianchi. 

Kupitia mkutano huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alifikia kiasi cha kuueleza ulimwengu kuwa ikiwa hatua madhubuti hazitachukuliwa, ni dhahiri wanadamu wanajichimbia kaburi.  

Kingine kilichovutia ni ushiriki wa watu wa asili katika mkutano huo ambapo walieleza namna wanavyoyategemea mazingira ya asili na hivyo yasiharibiwe. Watu wa asili ambao wanashiriki kikamilifu ndani na nje ya ukumbi wa COP26 walieleza kuwa hakuna anayejua vyema jinsi ya kulinda asili kuliko watu wa asili. Waliitumia fura hiyo ya mjini Glasgow kushawishi mazungumzo kwa kila njia iwezekanavyo ikiwa ni pamoja na maandamano ya mitaani. 

Kilichokuwa kinapiganiwa katika mkutano wa COP26 ni kitu dhahiri kuwa kweli dunia inakabiliwa na mabadiliko ya tabianchi. Mfano huu tunaoenda kuuona katika makala hii pengine ni mdogo ikilinganishwa na maeneo mengine ya dunia, lakini unaleta tahadhari kuwa, “wanadamu tusipochukua hatua tunajichimbia kaburi”.  

Na sasa tuelekee kaskazini mwa Tanzania, katika moja ya maeneo ya wilaya ya Ngorongoro, Loliondo, mkoani Arusha ambako watu jamii ya Maasai ambao kwa miaka yote ya uwepo wao shuguli yao ya kujipatia kipato na chakula ni kupitia mifugo hususani ng’ombe, na chakula chao ni nyama na maziwa, sasa wameanza kulazimika kuanza kuhamia katika shughuli za kilimo baada ya shughuli yao hiyo ya  asili ufugaji kuathiriwa na mabadiliko ya tabianchi. 

Mathias Tooko wa redio washirika wetu Loliondo FM amewatembelea wakiwa shambani na ameshuhudia mwenyewe mizoga ya ng’ombe ikiliwa na mbwa. Ng’ombe wamekufa kutokana na ukame na sasa wafugaji wanaona ni bora waanze kulima ili wawe na chakula katika ghala zao kwani hawana uhakika kama ng’ombe, mbuzi na kondoo wataweza kuhimili hali mbaya ya ukame iwapo hali itaendelea kuwa hivyo. Na hata mvua zikinyesha mwaka huu, hawana uhakika kama hali haitabadilikabadilika kwani hivi sasa majira hayatabiriki kutokana na mabadiliko ya tabianchi. 

Kutokana na mabadiliko ya tabianchi, jamii ya wafugaji, Maasai wa Loliondo kaskazini mwa Tanzania wamelazimika kuhamia katika kilimo.
Screenshot
Kutokana na mabadiliko ya tabianchi, jamii ya wafugaji, Maasai wa Loliondo kaskazini mwa Tanzania wamelazimika kuhamia katika kilimo.

  

Bwana Loserian Maoi ni mfugaji kutoka Loliondo anasema wameanza kujikita kwenye kilimo kama njia mbadala ya kuongeza kipato na chakula kutokana na kuwepo kwa mabadiliko ya tabia nchi ambayo yanaathiri sana wafugaji, pale ambapo mifugo kama ng'ombe, mbuzi na kondoo wanakosa afya na kupelekea kukosa bei huku familia zikihitaji chakula na mahitaji muhimu. 

“Sisi sio wataalamu sana wa kilimo. Asili yetu sana ni ufugaji. Zamani sisi tulikuwa hatulimi lakini sasa tumeanza kulima nyakati zimebadilika na tumeona mabadiliko ya tabianchi ni halisia. Hii njia ya mbadala, ya kilimo ambayo tumeichagua tumeona ya kwamba kwa kweli itatusaidia kwa sababu hatutajua kwamba kiangazi kitaanza muda gani na mifugo watakosa nyasi kwa muda gani, kwa hiyo tukiwa na chakula ambacho kinatokana na kilimo tunakuwa na uhakika kidogo wa maisha.” Anaeleza Loserian Maoi. 

Naye Lazaro Nasero, ni mfugaji pia. Sasa kama wenzake amehamia kaytika kilimo anasema, “mimi ni maasai naishi katika kijiji cha Sakala ni mkulima na ni mfugaji. Ng’ombe wanakufa kwa hiyo tunalima ili tupate chakula. Kwa hiyo ninaiambia serikali kwamba hawa wataalamu wa kilimo watusaidie kutupa mbegu bora n aza bei nafuu kwa kuwa ng’ombe wanakufa mara kwa mara kwa hiyo hatuna pesa ya kununua mbegu kwa hiyo watupe kwa bei nafuu. Na madawa kwa ajili ya kudhibiti wadudu waharibifu wa mazao yetu. Kwa hiyo nawaambia wamasai wenzangu tulime tisitegemee mifugo tu.” 

Hata hivyo wafugaji hao wameiomba serikali kupitia idara za kilimo na mifugo kuwa karibu nao ili kuwapatia ushauri nasaha juu ya mbegu bora inatostahili kulingana na maeneo wanayohishi pamoja na kupatiwa pembejeo za kilimo kwa bei nafuu sambamba na dawa za mifugo ili kuweza kukabiliana na changamoto ya magojwa.  

Soundcloud

 

Bwana Lawrence Ledio, ni Afisa Kilimo wilaya Ngorongoro anawaasa wafugaji kuwa makini wanapo hamia kwenye kilimo ili kuzingatia kilimo hifadhi ambayo ni rafiki kwa mazingira pamoja na kuwashauri aina ya mbegu inayoendana msimu huu ambayo mvua zinaonekana kuwa chini ya wastani. 

“wakulima ambao huku kwetu ni wafugaji, wameanza kulima kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya tabiachi kwa sababu sasa mifugo haina afya ya kutosha, haina soko la kutosha kwa sababu ya ukame, sasa tumeenda kwenye kilimo. Nini tufanye kwenye kilimo? Tunawashauri wakulima walime kilimo ambacho ni kilimo hifadhi ambacho kinahifadhi mazingira ili tuendelee kupata mvua za kutosha. Tutumie mbegu bora ambazo zimethibitishwa na wataalamu. Na sasa hivi tuna mfumo wa kidijitali ambao ni M-Kilimo ambao tumesajili wakulima kwenye mfumo, mkulima anatumia simu yake ya mkononi *152*7 halafu anafuata maelekezo anaweka ushauri wake (au swali) na sisi tutamjibu kwa njia ya SMS pale alipo.”  Anaeleza Bwana Lawrence Ledio.

Akieleza hali ilivyokuwa hapo awali Mzee Olenesero mkazi wa Loliondo amesema zamani hakukuwa na shida ya mvua wala shida ya maji tofauti na hivi sasa ambapo vyanzo vya maji vinakauka, nyanda za malisho zimepunguwa na hawawezi tena kutabiri nyakati huku wakilaumu maendeleo na ongezeko la watu kuchangia uharibifu wa mazigira na kuleta mabadiliko ya tabianchi, “naitwa Lazaro Nesero mfugaji kutoka Loliondo. Kuna tofauti kubwa ukilinganisha kipindi cha nyuma na hivi sasa, wafugaji tulikuwa na maeneo makubwa ya wazi, mvua za mara kwa mara lakini sasa tumeshuhudia  maendeleo yanayokuja kwa kasi, na haya yote ni mabadiliko kwetu, hatukuwa wakulima bali tulitegemea nyama na maziwa kama chakula, maendeleo haya, yameleta changamoto zake jambo linalopelekea, wafugaji kujikita kwenye kilimo kama njia mbadala ya kuongeza kipato na chakula zamani hakukuwa na shida ya mvua wala shida ya maji tofauti na hivi sasa ambapo vyamzo vya maji vinakauka,nyanda za malisho zimepunguwa. Hatuwezi tena kutabiri nyakati kwa kutumia waataalam wetu wa asili. Mimi nafikiri, maendeleo yamechangia pakubwa kuleta mabadiliko. Kwa upande wa kilimo, nashauri tulime lakini tuheshimu vyanzo vya maji , nyanda za malisho pamoja na misitu Ya asili ili kuweza kukabiliana na hali na mifugo yetu wawe salama.”