Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtoto Charline atamani mapigano yaishe ili arudi Bunagana aendelee na masomo

Charline mwenye umri wa miaka 11, anatabasamu licha ya kuwa katikati ya majanga. Amekimbia mapigano Bunagana yeye na familia yake na sasa wanaishi kambini huko Rutshuru jjimboni Kivu Kaskazini nchini DRC.
© UNICEF/Jean_CLaude Wenga
Charline mwenye umri wa miaka 11, anatabasamu licha ya kuwa katikati ya majanga. Amekimbia mapigano Bunagana yeye na familia yake na sasa wanaishi kambini huko Rutshuru jjimboni Kivu Kaskazini nchini DRC.

Mtoto Charline atamani mapigano yaishe ili arudi Bunagana aendelee na masomo

Amani na Usalama

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limetembelea eneo la Rutshuru jimboni Kivu Kaskazini ili kutathmini hali ya mahitaji ya watoto na familia zao baada ya kufurushwa na kuhamia kwenye kambi za muda kufuatia mashambulizi kutoka vikundi vilivyojihami. 

Watendaji wa Umoja wa Mataifa walifika Rutshuru kwa kutumia helikopta na kisha wakaelekea moja kwa moja hadi uwanja wa mpira wa Rugabo hapa Kitchanga kuliko na kambi ya wakimbizi wa ndani. 

Walijionea shughuli mbalimbali zikiendelea ikiwemo mapishi, ambapo watoto walikuwa wanapika, halikadhalika wanawake. 

Mtoto Charline akumbuka alichokiona Bunagana

UNICEF haikusita kuzungumza na mtoto aliyekuwa anapika na ambaye alijitambulisha akisema, “jina langu ni Charline, na nina umri wa miaka 11. Nilikimbia vita Bunagana. Tuliambiwa tukimbie kwa sababu hapo  ndio walikuwa wanaweka mabomu. Tulikimbia na kuja hapa Rutshuru.”

Charline anasema wakiwa njiani walisikia milio ya risasi, na hivyo ilibidi wazidi kukimbia.

Watoto wa familia za wakimbizi wa ndani wakipika katika kambi iliyoko Rutshuru jimboni Kivu Kaskazini nchini DRC.
© UNICEF/Jean-Claude Wenga
Watoto wa familia za wakimbizi wa ndani wakipika katika kambi iliyoko Rutshuru jimboni Kivu Kaskazini nchini DRC.

“Natumai kuwa amani itarejea ili niweze kurejea nyumbani, kwa sababu nilipokuwa vita, niliumia sana kwa sababu niliacha shule. Napendani nirudi shuleni ili niweze kufanikiwa na niwe huru maishani,” anasema Charline.

Charline akiwa na mawazo hayo, kwingineko, ni mgeni njoo mwenyeji apone!! Watoto walitumia fursa ya uwepo wa Naibu Mratibu wa kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, Suzana Tkalec, na kuambatana naye huku  wakiimba.

Hofu ya UNICEF

Jean-Jacques Simon, Mkuu wa Mawasiliano UNICEF anasema « Kwa UNICEF hofu kubwa ni watoto kukimbia makwao, kuacha jamii zao na wamesambaa.  Hofu yetu ni ulinzi wao kwani mara nyingi hawana maji wala dawa. Tunachohofia ni kwamba katika siku chache zijazo hawatakuwa na mazingira yao kama vile shule na mahali pa kucheza, na hii ndio tumekuja kuangalia na hali inatoi shaka.”