Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Askari wa kulinda amani wakisindikiza msafara wa misaada ya kibinadamu kuelekea kijiji cha Pinga huko Kivu Kaskazini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Helikopta ikiwa kwenye operesheni za ulinzi wa amani DRC yaanguka, Baraza lajulishwa usalama unadorora

© UNICEF/Guy Hubbard
Askari wa kulinda amani wakisindikiza msafara wa misaada ya kibinadamu kuelekea kijiji cha Pinga huko Kivu Kaskazini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Helikopta ikiwa kwenye operesheni za ulinzi wa amani DRC yaanguka, Baraza lajulishwa usalama unadorora

Amani na Usalama

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC helikopta iliyokuwa imebeba watu wanane wakiwemo wafanyakazi 6 kutoka jeshi la Pakistani na wanajeshi wawili mmoja kutoka Urusi na mwingine kutoka Serbia imeanguka ikiwa katika uchunguzi jimboni Kivu Kaskazini. 

Msemaji wa Umoja wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric akizungumza na waandishi wa habari hii leo jijini New York, Marekani amesema helikopta hiyo ilikuwa eneo la Tshanzu, kusini-mashariki mwa mji wa Rutshuru jimboni humo. 

“Hivi karibuni kumekuweko na mapigano kwenye eneo hilo kati ya kundi lililojihami la M23 na jeshi la serikali ya DRC, FARDC,” amesema Dujarric. 

Amenukuu taarifa kutoka ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani DRC, MONUSCO ukisema operesheni za kusaka na uokoaji zilianza baada ya helikopta hiyo kupoteza mawasiliano na ujumbe huo mapema leo asubuhi. 

“Uchunguzi unaendelea na tutatoa taarifa zaidi kadri taarifa zaidi zitakavoypatikana. Fikra zetu ziko bila shaka na familia na marafiki za waliokuweko kwenye helikopta hiyo, na kwa wenzetu MONUSCO nchini DRC,” ametamatisha Bwana Dujarric. 

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likiwa kwenye mkutano kujadili hali inayoendelea nchini Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo DRC
© UN Photo/Eskinder Debebe
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likiwa kwenye mkutano kujadili hali inayoendelea nchini Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo DRC

Baraza lajulishwa hali ya usalama DRC inazidi kuzorota 

Wakati  hayo yakitokea, hii leo katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, wajumbe wamejulishwa na Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Matifa na mkuu wa MONUSCO, Bintou Keita, amesema hali ya usalama katika taifa hilo la Maziwa Makuu inazidi kuzorota kila uchao huku idadi ya mauaji ya raia na ukimbizi wa ndani ikiongezeka. 

Kando ya changomoto zilizoko, Bi  Keita amezungumzia ongezeko la mashambulizi k utoka kundi la M23. 

“Jana kundi hilo la M23 lilifanya mashambulizi ya kutisha ya kulenga raia huko Rutshuru. Mapigano yametokea pia katika maeneo matatu ya mpakani na Rwanda, DRC na Uganda karibu na mji wa Bunagana. Tangu kuanza kwa mwaka huu, na tuko mwezi wa tatu tu, MONUSCO imerekodi takribani vifo vya raia 2,300 mashariki mwa DRC,” amesema Bi. Keita. 

MONUSCO imeimarisha ulinzi 

Ni kwa kuzingatia mazingira hayo, Bi. Keita amesema MONUSCO imeongeza maradufu juhudi zake za kulinda raia lakini “lazima tuzingatie uhalisia. Bila kuchanganya mbinu za kulenga vichocheo vya hali ya sasa na dalili zake, rasilimali zetu na zile za jeshi la serikali, FARDC hazitatosheleza na hivyo hali ya usalama itazidi kudorora.” 

Ametoa wito kwa serikali ya DRC kutekeleza mpango wake wa kina wa mikakati ya kisiasa, ikiwemo hatua za marekebisho ambayo yatawezesha kufanikisha utulivu mashariki mwa nchi hiyo.