Tanzania, ILO, na wadau wanusuru watoto kutumikishwa kwenye mashamba ya tumbaku

14 Juni 2022

Tanzania imeridhia mikataba yote muhimu ya kimataifa ya kuzuia ajira kwa watoto na imeendelea kutekeleza mipango ya kuwaondoa watoto katika mazingira magumu kama hayo. Kwa msaada wa wadau mbalimbali - kama vile Umoja wa Mataifa kupitia shirika lake la kazi duniani, ILO, mashirika yasiyo ya kiserikali na mashirika ya kiraia - sheria na sera zilizopo zimebadilishwa ili kutoa haki bora na ustawi.

Hata hivyo, changamoto katika sheria za kazi na utekelezaji wa sheria za jinai bado ni changamoto katika ajira kwa watoto.

Hali ya utumikishaji watoto duniani na Tanzania

Takwimu mpya za shirika la Umoja wa Mataifa la kazi duniani ILO, zinaonesha kuwa watoto milioni 160 duniani kote wanatumikishwa kwenye sekta mbalimbali ikiwemo mashambani. Idadi hiyo ni sawa na mtoto 1 kati ya 10 na idadi zinaongezeka huku janga la COVID-19 likitishia kufuta mafanikio yote yaliyopatikana katika kutokomeza ajira kwa watoto.

Nchini Tanzania, takwimu za kitaifa, asilimia 29.3ya watoto wote wenye umri wa miaka 5-14 nchini Tanzania wanajihusisha  na  ajira kwa watoto katika sekta mbalimbali za kiuchumi, ikiwa ni pamoja na kilimo, kazi za nyumbani, uvuvi na madini.

Zaidi ya hayo, asilimia 24.6 ya watoto wanaofanya kazi wenye umri wa miaka 7-14 wako kazini na shuleni. Kilimo ni sekta kuu ambayo watoto hufanya kazi zaidi, hasa katika mazao ya tumbaku, ambayo huchangia  asilimia 94.1ya ajira zote za watoto.

Kilimo ni sekta inayoongoza kwa uchumi katika Mkoa wa Tabora, ambapo asilimia 81.5 ya kaya, kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2012 asilimia 64 ya wananchi wa Tabora wanajihusisha na kilimo cha tumbaku kama zao kuu la kibiashara katika mkoa huo, na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika uchumi wa kaya na nchi kwa ujumla.

Shamba la mmea wa tumbaku nchini Kenya
© WHO
Shamba la mmea wa tumbaku nchini Kenya

Mradi wa PROSPER RESET wanusuru watoto mashambani

Mfuko wa ECLT unaosaidia kutokomeza utumikishwaji watoto katika nchi zinazolima tumbaku duniani, ulifanya utafiti wa awali kupitia mradi wa "PROSPER", ambao ulitekelezwa katika Mkoa wa Tabora kutoka 2011 hadi 2015.

Geofrey Damson, mkazi wa Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora, alizungumzia hali aliyoipata wakati wa utoto wake katika familia yake: "Nilianza kufanya kazi ya tumbaku nikiwa na umri wa miaka mitano.  Wakati nilikuwa na umri wa miaka nane, nilijua jinsi ya kufanya kazi na kuanza kukata magogo ya kukausha tumbaku. Wakati wa msimu wa kilimo cha zao la tumbaku, sikuhudhuria hata shule, kwa sababu familia nzima iko shambani," anasema Damson.

Damson anasema mpango wa PROSPER wa kutokomeza ajira kwa watoto katika maeneo ya mashamba ya tumbaku, unaotekelezwa na "Tanzania Development Foundation" (TDFT) na chama cha wanawake viongozi kwenye kilimo na mazingira Tanzania, (TAWLAE) na kufadhiliwa na  ECLT Foundation, sio tu ulitoa elimu juu ya madhara ya ajira kwa watoto lakini pia ilitoa mafunzo juu ya  bustani, ufugaji wa kuku na nyuki kwa vijana, wazazi, na walezi.  Baada ya mafanikio ya utekelezaji wa programu hii ya mafunzo, Damson sasa ana mizinga 100, na maisha  yake yamebadilika kwa kuongeza mapato yake.

Chanzo cha utumikishaji watoto kwenye mashamba ya tumbaku

Utumikishwaji wa watoto katika mashamba ya tumbaku husababishwa na sababu kadhaa, ikiwa ni pamoja na kujitenga kwa familia, hali ngumu ya maisha katika familia (kipato cha chini ambacho hakikidhi mahitaji ya msingi ya kila siku), vifo vya wazazi, mila na desturi kwa baadhi ya makabila.

Reginald Omulo mkulima ambaye aliachana na kilimo cha tumbaku na kugeukia kulima maharagwe nchini Kenya.
© WHO
Reginald Omulo mkulima ambaye aliachana na kilimo cha tumbaku na kugeukia kulima maharagwe nchini Kenya.

Norbat Silwamba, mkazi wa kata ya Gua wilayani Songwe ni mmoja wa wanufaika wa  mradi wa "PROSPER RESET", anasema: "Tulikuwa tunatumia muda mwingi kushirikiana na familia zetu kuboresha uchumi wetu, bila kujali athari zinazoweza kutokea kwa watoto. Wakati mwingine watoto walikuwa wakisumbuliwa na ugonjwa usioeleweka. Wazazi pia walitumia muda mwingi hospitalini. Lakini sasa, baada ya kuelimishwa juu ya ajira kwa watoto katika umri mdogo, tabia hiyo imeisha na watoto wanahudhuria shule."

Serikali nayo ina nafasi yake

Aidha, Mkurugenzi wa Wilaya ya Urambo  Baraka Zikatimu alisema: "Tuna kamati inayoitwa MTAKUWWA – iliyowezeshwa na mradi wa  "PROSPER RESET" unaotekelezwa na TDFT na TAWLAE – katika kufuatilia masuala ya ukatili na ajira kwa watoto katika mashamba ya tumbaku.  Kwasasa watoto wanaendi shule, Hali mahudhurio darasani imeongezeka, wakati miaka minne iliyopita, hali haikuwa nzuri ya kutosha. Matokeo yake, watoto wengi  wameweza kufanikiwa na kuendelea na shule ya sekondari. Sasa tunaona kwamba maisha ya watoto  yameboreka. Tunaamini kuwa Wilaya ya Urambo itakuwa moja ya wilaya zilizofanikiwa sana katika suala la maendeleo, kwani tutakuwa tumeondoa ajira na ukatili kwa watoto katika makundi haya ya watoto na akina mama pia."

Mradi umeinua kiwango cha mahudhurio shuleni

Ili kupata ukweli kuhusu mahudhurio ya wanafunzi katika shule mojawapo, nilizungumza na  Genovena Mwanakulya, mwalimu  katika Shule ya Msingi Mtanila wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya. Alisema awali kulikuwa na tatizo kubwa kwa sababu, mara tu  msimu wa kilimo cha tumbaku unapoanza, wazazi wako tayari kulipa faini kwa kutowapeleka watoto wao shule, kwani badala yake watoto wanafanya kazi shambani.  Kwa hivyo, darasa la wanafunzi 50 litapungua  hadi wanafunzi 30 tu kwa siku.  Kwa msaada wa  kamati ya MTAKUWWA, jamii ilianza kuelewa athari za ajira kwa watoto na matokeo ya kutokuwepo kwa shule. Tangu wakati huo, pengo limepungua katika shule, wakati ufaulu wa watoto umeongezeka.

Mkulima wa tumbaku akiwa amebeba tumbaku iliyokaushwa
WHO/Marcelo Moreno
Mkulima wa tumbaku akiwa amebeba tumbaku iliyokaushwa

"Alliance One Tobacco Tanzania Ltd, ambayo inashiriki katika ununuzi wa tumbaku  inasaidia jamii ya wakulima kwa kushirikiana na "TDFT" kupitia mradi wa "PROSPER RESET" kupambana na ajira kwa watoto na ukatili katika mashamba ya tumbaku kwa kutoa elimu ya kuzuia vitendo hivyo, pamoja na kuunda vikundi vya akiba na mikopo  kwa  wazazi.

Mratibu wa ALP nchini Tanzania, Lawrence Safari, alisema: "Wakulima wengi wana kipato cha chini hasa linapokuja suala la msimu wa mavuno. Sio lazima wawe na pesa za kuwalipa wafanyakazi, kwa hivyo wanaomba familia zao, ikiwa ni pamoja na watoto, kwenda na kufanya kazi ya uvunaji wa tumbaku. Kwa kutambua ukweli huu, tunaunda vikundi vya  akiba na mikopo ili kuwasaidia kuweka akiba na kukopa fedha za kuwalipa wafanyakazi na kuwaacha watoto waende shule na wasitumike kwa shughuli za uvunaji wa tumbaku na maandalizi."

Mkurugenzi wa TDFT, Dick Mlimuka, alisema: "Miradi inayosaidia kuondoa watoto kutoka katika ajira za umri mdogo katika mikoa ambayo wakazi wake wanajihusisha na uzalishaji wa tumbaku imeanza tangu mwaka 2011, ikiwa ni pamoja na mradi wa "PROSPER RESET", hasa mkoani Tabora, ambao ni kitovu cha zao hilo nchini Tanzania.  Wakati huo, ajira ya watoto katika  mashamba ya tumbaku ilikuwa asilimia 90 kipindi hicho, Sasa hali imeimarika kwa kiasi kikubwa katika suala la elimu ambayo imekuwa ikitolewa kwa jamii, hasa kwa wakulima wa zao la tumbaku.

Matumizi ya tumbaku ndio chanzo kinachozuilika cha saratani duniani
WHO
Matumizi ya tumbaku ndio chanzo kinachozuilika cha saratani duniani

ILO inajengea uwezo wakaguzi pahala pa kazi

Umoja wa Mataifa kwa upande wake unamulika zaidi sera katika utokomezaji wa ajia kwa watoto ambapo Afisa wake nchini Tanzania Maridadi Phanuel anasema, ““Kwanza kabisa kile tunachofanya tunajengea uwezo wakaguzi wa pahala pa kazi ili wasimamie sheria. Kama ujuavyo wao kwa mujibu wa sheria za kazi na mahusiano kazi wana wajibu wa kusimamia sheria ili kuhakikisha mwajiri na mwajiriwa wanazingitia vipengele vya sheria. Kuajiri mtoto ni kosa kisheria. Kwa hiyo mtu anayeajiri mtoto anapaswa kutozwa faini kwa mujibu wa sheria za kazi. Hivyo tunajengea uwezo wakaguzi ili wasimamie sheria, na watoto waondolewe kwenye mazingira ya utumikishwaji kwenye machimbo na kilimo.”

TAGS: Tanzania, TAWLAE, ELCT, ILO, ALP, Utumikishaji watoto, Tumbaku, Tabora, Songwe, Mbeya

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter