Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto milioni 108 duniani kote wanatumikishwa hususan kwenye kilimo- FAO

Watoto wakiuza matunda kwenye soko  moja mjini Korhogo, Kaskazini-magharibi mwa Côte d’Ivoire
© UNICEF/Frank Dejongh
Watoto wakiuza matunda kwenye soko moja mjini Korhogo, Kaskazini-magharibi mwa Côte d’Ivoire

Watoto milioni 108 duniani kote wanatumikishwa hususan kwenye kilimo- FAO

Haki za binadamu

Shirika la chakula na kilimo duniani, FAO limesema bado watoto wanaendelea kutumikishwa kwenye sekta ya kilimo ulimwenguni kote na hivyo kuathiri uwezo wao wa kustawi na kujinasua kwenye umaskini pindi wanapokuwa watu wazima. Assumpta Massoi na ripoti kamili.

FAO inasema kuwa duniani kote watoto milioni 108 wa kike na wa kiume wanatumikishwa ambapo asilimia 70 wanafanya kazi kwenye sekta za kilimo, ufugaji, misitu, uvuvi na ufugaji wa samaki.

Idadi hiyo, kwa mujibu wa FAO imeongezeka kwa watoto milioni 10 tangu mwaka 2012, licha ya jitihada za Umoja wa Mataifa za kutokomeza utumikishaji watoto kwenye sekta hizo.

Ariane Genthon ambaye anahusiska na programu ya FAO ya kuondokana na utumikishwaji wa watoto kwenye kilimo anasema sababu kubwa ni umaskini kwenye familia ambao husababisha wazazi kutumia watoto wao kufanya kazi kwenye kilimo.

Amesema watoto wanapotumikishwa kwenye kilimo wanashindwa kwenda shule, na hata pale wanapokwenda wanakuwa wamechoka na wanashindwa kusoma ipasavyo kama wenzao ambao hawaendi kwenye kilimo.

Bi. Genthon amesema pamoja na uchovu, watoto wanakuwa wanakumba na madhara ya kiafya kutokana na kemikali zinazotumika kwenye sekta ya kilimo na mara nyingi wazazi hutumia watoto wao kwa kuwa wanafanya kazi bila ujira.

Kwa mantiki hiyo amesema FAO wanasisitiza programu ya kuimarisha maeneo ya vijijini ili yawe na uwezo wa kuzalisha chakula na kushiriki kilimo bila kutumia watoto kwenye sekta ya kilimo.

Halikadhalika miradi ya kutokomeza umaskini inayolenga familia maskini ili angalau zipate kipato bila kutumikisha watoto wao.