Skip to main content

Utumikishaji wa watoto utaendelea hadi lini?

Mtoto wa kiuke akitumikishwa huko karibu na Kathmandu, mji mkuu wa Nepal
David Longstreath/IRIN
Mtoto wa kiuke akitumikishwa huko karibu na Kathmandu, mji mkuu wa Nepal

Utumikishaji wa watoto utaendelea hadi lini?

Haki za binadamu

Watoto! Watoto! Watoto! Utoto wao unapokwa kutokana na shida lukuki zilizosheheni kwenye jamii zao. Kuuza nyanya, machungwa kwaonekana ni kawaida ilhali kunamnyima mtoto haki zake.

Shirika la kazi duniani, ILO linataka hatua za dharura zichukuliwe ili kukabiliana na matatizo  ya kiuchumi yanayotumbukiza watoto kwenye ajira.

Mkurugenzi Mkuu wa ILO Guy Ryder amesema hayo mjini Geneva, Uswisi kando mwa mkutano mkuu wa shirika hilo, ikiwa ni katika kuelekea siku ya kupinga ajira kwa watoto duniani tarehe 12 mwezi huu wa Juni.

Ametaja maeneo ambayo yamekithiri kwa kuajiri watoto kuwa ni mfumo mzima wa kimataifa wa usambazaji wa huduma ambako watoto hutumikishwa kwa kificho pamoja na kilimo ambako watoto hufanya kazi ili kusaidia familia zao.

Image
ILO
Watoto wanapaswa kuwa shuleni na si mashambani au viwandani

“Changamoto siyo tu kwenye viwanda vinavyoshona nguo zinazouzwa kimataiaf, tumbaku au kakao bali pia kwenye masoko ya mashinani ya mtama, uwele na hata ufyatuaji wa matofali ambako watoto wanatumikishwa,” amesema Ryder.

Amesema hivi sasa ajira kwa watoto inakumba watoto wapatao milioni 152 wenye umri kati ya miaka 5 hadi 17.

Bwana Ryder anasema kinachosikitisha zaidi kati ya mwaka 2012 hadi 2016 hakukuwepo na kupungua kokote kwa idadi ya watoto wanaotumikishwa huku namba ya watoto wanaotumikishwa kwenye ajira hatarishi ikiongezeka.

“Hii ni kwasababu watoto wanaanza kutumikishwa wakiwa na umri wa miaka 6 wakati bado wako kwenye familia zao wakishiriki shughuli za kilimo na kadri wanavyokua wanazidi kufanya kazi hatarishi,” amesema mkuu huyo wa ILO.