Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bachelet na mambo makuu 4 ya kusongesha haki duniani 

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet
UN Photo/Antoine Tardy
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet

Bachelet na mambo makuu 4 ya kusongesha haki duniani 

Haki za binadamu

Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu, Michelle Bachelet amehutubia mkutano wa 50 wa Baraza la Haki za Binadamu la chombo hicho akitoa tathmini ya maendeleo ya haki za binadamu duniani kote wakati huu ambao amesema ni wa changamoto kubwa katika kusongesha haki hizo. 

Amesema ni zama za changamoto kubwa akianzia hali ya Ukraine ambako uvamizi wa Urusi unaendelea kusambaratisha maisha ya binadamu, “na vitisho na machungu yaliyokumba raia yataacha alama ya kudumu kwenye sio tu maisha  yao bali pia ya vizazi vijavyo.” 

Chakula kinasambazwa kwa watu 450,000 kaskazini mwa Ethiopia walioathiriwa na mzozo.
© WFP/Sinisa Marolt
Chakula kinasambazwa kwa watu 450,000 kaskazini mwa Ethiopia walioathiriwa na mzozo.

Majanga matatu ni mzigo kwa wengi duniani 

Zahma za kiuchumi, kijamii na kisiasa zinashamiri kila kona ya dunia na hakuna dalili ya kutokomea na hivyo kuleta madhara makubwa katika haki za  binadamu. 

“Majanga ya chakula, nishati na fedha yanatishia kutumbukikza mamilioni ya wakazi wa dunia kwenye ukosefu wa uhakika wa chakula na umaskini. Watu bilioni 1.2 wanaishi kwenye nchi ambazo zinakumbwa na majanga yote matatu,” amesema Bi. Bachelet. 

Ukosefu wa usawa nao unapamba moto ndani ya nchi na baina ya nchi na kutishia harakati za kujikwamua kutoka COVID-19 sambamba na utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu, SDGs na kuzorotesha hatua kwa tabianchi. 

“Changamoto hizi zinavyozidi kuongezeka, watu wengi ninaokutana nao wanahoji sio tu kuhusu mustakabali wao bali pia wa jamaa na dunia nzima,” amesema Kamishna Mkuu huyo wa haki za binadamu ambaye pia amesema mkutano huu wa 50 ndio wa mwisho kuhutubia kwani anatamatisha awamu yake ya miaka minne na hatowania tena nafasi hiyo. 

Hata hivyo ametaja mambo makuu manne ambayo anaona ni muhimu katika kutatua changamoto mtambuka zinazokabili dunia hivi sasa. 

Mosi kuondokana na ukosefu wa usawa na ubaguzi 

“Tunaishi katika dunia iliyogubikwa na ukosefu wa usawa ambapo utafiti mmoja umekadiria kuwa ukosefu wa usawa duniani hivi sasa ni mkubwa kama ilivyokuwa mwanzoni mwa karne ya 20,” amesema Bi. Bachelet. 

Anasema mazingira ni magumu kiasi kwamba ni vigumu kwa watu kuweza kukabiliana na majanga mengine. “kwa hiyo lazima tuazimie kuondokana na ukosefu wa usawa na ubaguzi. Uwe wa watu wa jamii ya asili, watu wenye ulemavu, ubaguzi wa kijinsia na kadhalika.” 

Ametolea mfano Georgia, Malawi, Msumbiji na Macedonia ambako wameshirikiana na serikali kusongesha haki za watu wenye ulemavu. 

Pili bajeti za kitaifa zijumuishe haki za binadamu 

Bi. Bachelet amesema iwapo bajeti hizo zitazingatia wajibu wake kwa haki za binadamu zinaweza kuwa kichocheo kikubwa katika kufanikisha SDGs. “Kuongeza matumizi katika sekta za kijamii, huduma ziweze kufikiwa na kila mt una huduma ziwe bora bila ubaguzi, hii itakuwa msingi bora. Na sasa tunasaidia nchi kuchambua bajeti zao, kuchangisha fedha na kupanga bajeti kwa lensi ya haki za binadamu.” 

Tatu mshikamano wa kimataifa na ushirikiano wa kifedha 

Ushirikiano huu unahitajika zaidi hivi sasa pamoja na msamaha wa madeni, amesema Bachelet akiongza kuwa, “bila ongezeko la kutosha la fedha, hatutaweza kufanikisha SDGs. Pengo la ufadhili kufanikisha SDGs limeongezeka kwa asilimia 70 kwa mwaka na kuwa dola trilioni 4.3.” 

Amekumbusha ahadi za kuongeza maradufu misaada rasmi ya maendeleo kwa nchi maskini pamoja na kubadili mfumo wa kimataifa wa fedha akisema, “taasisi za kimataifa za fedha zina wajibu wa kusaidia nchi zilizozidiwa madeni. Mfumo wa sheria wa kimataifa unatoa fursa hiyo ya usaidizi.” 

Nne: Fursa ya raia na uwazi 

Bi. Bachelet anasema raia kuwa na fursa ya kuzungumza na kutoa maoni ni muhimu sana hasa wakati wa majanga.  

“Lakini bado tunaendelea kupokea ripoti za kubinywa kwa fursa za kidemokrasia na raia kuzungumza iwe mitandaoni, kwenye majukwaa, duniani kote. Hatuwezi kutenganisha maendeleo ya kiuchumi kama vile kupunguza umaskini na hak iza wale wanaopaswa kuwa wanufaika wa maendeleo hayo, ikiwemo haki ya kusikilizwa,” amesema Bachelet. 

Amesema haki hizo ndio uhai wa jamii yenye haki na amani. 

Kikao changu cha mwisho, nang’atuka- Bachelet 

Bi. Bachelet ametumia hotuba yake ya leo kujulisha wajumbe kuwa ndio hotuba yake ya mwisho kwa Baraza hilo kwani anang’atuka. 

Alianza rasmi jukumu lake tarehe Mosi Septemba mwaka 2018 baada ya kuchaguliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na kuidhinishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. 

Kwa mujibu wa kanuni, nafasi hiyo hushikwa kwa kipindi cha miaka 4 na fursa ya kuongeza awamu nyingine. 

Kufuatia tangazo la Bi. Bachelet, Katibu Mkuu Guterres kupitia  msemaji wake amemshukuru Kamishna Mkuu huyo anayeng’atuka akisema alikuwa mstari wa mbele kusongesha haki za binadamu. 

«Katika kila alichofanya, aliishi na kupumua haki za binadamu. Alichukua hatua hata kwenye mazingira magumu ya kisiasa na ameleta mabadiliko makubwa chanya kwa watu duniani kote, » amesema Guterres katika taarifa hiyo iliyotolewa leo jiijni New York, Marekani. 

Amesema ataendelea kumuunga mkono na kuthamini busara zake, sauti yake na mafanikio ya kuhakikisha haki za binadamu ni msingi wa hatua zozote za Umoja wa Mataifa.