Skip to main content

Vitisho dhidi ya haki za binadamu vinaongezeka, halikadhalika suluhisho-Bachelet

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu, Michelle Bachelet alipotembelea Bunia, huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC mwezi Januari mwaka huu wa 2020
MONUSCO
Kamishna Mkuu wa haki za binadamu, Michelle Bachelet alipotembelea Bunia, huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC mwezi Januari mwaka huu wa 2020

Vitisho dhidi ya haki za binadamu vinaongezeka, halikadhalika suluhisho-Bachelet

Haki za binadamu

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet hii leo akihutubia mkutano wa 43 wa Baraza la Haki za binadamu mjini Geneva Uswisi amesema vitisho dhidi ya haki za binadamu, maendeleo na amani vinaweza kuwa vinaongezeka lakini pia utatuzi kwa vitendo unaozingatia kaanuni nzuri za haki nao unaongezeka.

Akisisitiza kuhusu hilo amesema makubaliano ya kimataifa ya miaka ya hivi karibuni yameleta masuluhisho mengi ya namna hiyo akitaja baadhi kama Ajenda ya mwaka 2030, Mkataba wa kimataifa wa wakimbizi, Mpango wa Umoja wa Mataifa dhidi ya mabadiliko ya tabianchi UNFCC, miongoni mwa nyingine nyingi.

Akiwazungumzia vijana Bi Bachelet amesema vijana wavumbuzi ni lazima pia waonekane kama sehemu ya suluhisho la majanga dunia inayopitia akisema, “leo, wengi wanakosoa kukosekana kwa usawa, na wanatoa wito kwa utawala bora zaidi, usawa mkubwa wa fursa, na heshima kwa haki za binadamu.”

Katika kulisisitiza hilo ametoa mfano wa Jonas Salk mvumbuzi wa chanjo ya polio ambaye alipata kusema kuwa jukumu letu ni kuwa kizazi cha zamani kizuri akimaanisha kuwa kizazi cha kale kinatakiwa kuandaa kwa ajili ya vijana wadogo, na kizazi kijacho, ulimwengu ambao una maisha yenye hadhi, uhuru na amani.

Mazingira ya leo ya kisiasa yenye msukosuko yanahitaji zana za sera ambazo zina mizizi ya uzoefu, na zenye rekodi ya mafanikio ya kuthibitika.

Akizitaja zana hizo ameeleza kuwa hatua ambazo  zinaendeleza ufikiaji wa elimu, utunzaji wa afya, kinga ya jamii kwa wote, na maisha ya hadhi yameonyesha matokeo chanya kwa kijamii pana, kiuchumi na kwa mtu mmoja mmoja.

Aidha amesema ushiriki mpana wa watu, wakiwemo vijana na taasisi ambazo ziko wazi na zinawajibika, zinaweza kuendeleza maelewani katika jamii, na kudumisha uchumi na uvumbuzi.

Bi Bachelet ametoa ahadi akisema, “ofisi yangu imejitolea kufanya kazi na mataifa, Umoja wa Mataifa na wadau pamoja na asasi za kijamii kuhakikisha kuwa kunakuwa na maendeleo haraka zaidi kuelekea ujumuishwaji wa jamii na kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu SDGs. Malengo haya yanayoweza kufikiwa, yatazinufaisha nchi na jamii.”