Zaidi ya asilimia 50 ya hewa ya Oksijeni yatoka baharini lakini bado tunaichafua- Guterres
Zaidi ya asilimia 50 ya hewa ya Oksijeni yatoka baharini lakini bado tunaichafua- Guterres
Ongezeko la kiwango cha maji ya bahari, kwa joto la maji ya bahari, kiwango cha asidi baharini na kiwango cha juu cha hewa ya ukaa baharini, vinatishia ustawi wa bahari ambayo ni tegemeo la binadamu, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake hii leo ambayo ni siku ya bahari duniani.
Guterres anasema ripoti ya mwezi uliopitia ya shirika la Umoja wa Mataifa la hali ya hewa duniani, WMO, ilithibitisha kuwa matatizo hayo yanayokumba bahari yanachochewa utatu wa majanga ambao ni; mabadiliko ya tabianchi, kupotea kwa bayonuai na uchafuzi “na sasa afya ya bahari ambayo ni tegemeo letu sote iko hatarini.”
Katibu Mkuu amesema bahari inazalishaji zaidi ya asilimia 50 ya hewa ya Oksijeni inayotumika duniani na ndio chanjo kikuu cha kipato kwa watu zaidi ya bilioni 1.
“Licha ya utegemezi huo, bado rasilimali za baharini zinatishiwa na shughuli za binadamu. Zaidi ya theluthi moja ya samaki huvuliwa bila utaratibu wa kuzingatia uendelevu. Kiwango kikubwa cha matumbawe kimeharibiwa. Utupaji taka za plastiki umekithiri na kufikia hata visiwa vilivyo ndani zaidi,” amesema Katibu Mkuu.
Nini cha kufanya?
Katibu Mkuu anasema, ni wakati wa kutambua kuwa ili kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs pamoja na mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi, tunahitaji juhudi za pamoja kukwamua na kuchechemua bahari yetu.
Kusaka mbinu mpya ya uhusiano na bahari yetu. Tushirikiane na mazingira badala ya kupambana nayo. Kujenga ubia jumuishi na maeneo yote duniani, jamii na kusaka mbinu bunifu za kulinda bahari.
Hatua zimeanza kuchukuliwa
Kwa mujibu wa Guterres, hatua tayari zimeanza, mathalani mwezi Novemba mwaka jana wa 2021 huko Glasgow, Uingereza wakati wa mkutano wa kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi, wajumbe walitambua dhimay a mifumo anuai ya baharini katika kufanikisha malengo ya kimataifa kuhusu tabianchi.
Mwezi Machi mwaka huu, serikali zilikubaliana kuandaa mkataba mpya wa kuondokana na uchafuzi utokanao na plastiki, bidhaa ambayo inatishia uhai wa viumbe vya baharini.
Baadaye mwezi huu, huko Lisbon, mji mkuu wa Ureno, mkutano wa kimataifa utajikita katika kuongeza kasi ya kuchukua hatua kwa kuzingatia sayansi na ubunifu ili kufanikisha lengo namba 14 la SDGs ambalo linamulika viumbe chini ya bahari.
Guterres anatamatisha ujumbe wake akisema, “kuhakikisha afya ya bahari na bahari yenye tija, ni jukumu letu la pamoja, ambalo tunaweza kutimiza tu iwapo tutafanya kazi pamoja” akisema kuwa, “katika siku hii ya Kimataifa ya Bahari duniani, hebu niwasihi nyote mnaohusika na afya ya bahari mshirikiane kuchechemua upya bahari zetu.”