Kuelekea mkutano wa Lisbon, nini matarajio ya Kenya na Ureno?
Kuelekea mkutano wa Lisbon, nini matarajio ya Kenya na Ureno?
Siku ya bahari duniani ikiadhimishwa hii leo, macho na masikio yanaelekezwa huko Lisbon, Ureno ambako kuanzia tarehe 27 mwezi huu hadi tarehe 1 mwezi Julai kutafaniyka mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu bahari.
Mkutano huo umeandaliwa kwa pamoja na serikali ya Ureno na Kenya wakati huu ambapo kinachotakiwa kunusuru bahari ni hatua mpya za ushirikiano wa pamoja kwa rasilimali hiyo inayozalisha zaidi ya asilimia 50 ya hewa ya Oksijeni inayotumiwa duniani.
Wawakilishi wa kudumu wa mataifa hayo mawili kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi Martin Kimani wa Kenya na Balozi Paula Zacarias, wa Ureno, kabla ya kwenda Ureno wamezungumza na Idhaa ya Umoja wa Mataifa na kuelezea maoni yao kuhusu bahari na hatua za kuhakikisha uhifadhi na matumizi endelevu ya bahari na rasilimali nyingine za bahari kwa faida ya wote.
Idhaa ya UN: Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu bahari una faida gani kwa Kenya na Ureno na nini matarajio?
Ana Paula Zacarias: Huu ni mkutano muhimu kwa Ureno. Bahari imeunganika na historia yetu, utamaduni wetu, ardhi yetu na uchumi wetu. Kuna uhusiano pia na ahadi yetu katika kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na kusongesha ajenda ya baharí sambamba na suala kuhusu mabadiliko ya tabianchi.
Tunatumai kuweko kwa washiriki wapatao 12,000 kutoka duniani kote. Na tayari tumepokea uthibitisho wa ushiriki kutoka kwa viongozi na wakuu wan chi 15 pamoja na mashirika ya kiraia, wasomi, mashirika ya vijana na jamii. Hata watu mashuhuri kama vile Mjumbe Maalum wa Marekani kuhusu tabianchi na wengine wengi.
Martin Kimani: Mkutano huu ni muhimu kwa kuwa unawakilisha fursa na uwajibikaji. Fursa kwa maendeleo endelevu ya kiuchumi, kumarisha uhakika wa kupata chakula, ajira kwa vijana duniani kote. Na ni uwajibikaji kwa kuwa tunapaswa kuhakikisha bahari zetu zinalindwa dhidi ya uchafuzi na mabadiliko ya tabianchi. Kama waandaaji wenza, Kenya na Ureno ziko makini kwa kuona ajenda nzito na chanya zinaibuka kutoka mkutano huo.
Kuna ongezeko la utambuzi kuwa lazima tubadili mwelekeo wa kuharibika kwa afya ya bahari il ikufikia lengo namba 14 la malengo ya maendeleo endelevu kuhusu uhai chini ya bahari. Katika kusongesha hilo, Kenya na Ureno pamoja na Umoja wa Mataifa wanaandaa fursa ya maamuzi ambayo yatasongesha hatua ya kulinda bahari kwa misingi ya sayansi na ubunifu.
Idhaa ya UN: Bahari zinapatia jamii kipato- wakazi wa pwani ya Kenya vijijini wanategemea uvuvi na kilimo kujipatia kipato. Tunawezaje kuhakikisha tunalinda jamii za pwani na mbinu zao za kujipatia kipato?
Martin Kimani: Ukanda wa pwani wa Kenya umejaliwa maliasili nyingi ikiwemo misitu ya mikoko, mabamba ya matumbawe, misitu, fukwe za mchanga na mimea iotayo chini ya bahari (seagrass) Vyote hivi ni vyanzo vya bayonuai na maji safi ambayo hatma yake ni kusaidia uchumi na maisha ya wakazi wa maeneo hayo.
Kwa kushirikiana kwa karibu na jamii za pwani, serikali imepatia kipaumbele suala la kuinua ustawi wa jamii hizo kiuchumi, kijamii na kuhakikisha ziko katika nafasi ya kujinasua iwapo kuna majanga. Halikadhalika tunachukua hatua matumizi ya kupita kiasi ya maliasili zilizoko baharini.
Mathalani, mradi wa Mikoko Pamoja ni mradi wa kijamii unaosongesha uchumi usioharibi mazingira huko Kaunti ya Kwale, pwani ya kusini mwa Kenya. Kwa msaada kutoka Taasisi ya Kenya ya utafiti wa uvuvi na viumbe bahari, KMFRI, na wadau wengine, wakazi wa pwain wanapanda upya mikoko na kurejesha ile iliyoharibika nah ii imedhihirika kusaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kufyonza hewa ya ukaa.
Mikoko Pamoja imekuwa ikitumia misitu ya mikoko kuuza hewa ya ukaa tangu mwaka 2013. Mapato kutokana na biashara hiyo hutumika kusaidia miradi ya jamii kama vile maji, huduma za kujisafi, elimu na uhifadhi wa mazingira.
Katika hali ya kawaida hii inamaanisha, wenyeji wamewezeshwa kufanya uamuzi wa kidemokrasia wa matumizi ya fedha zao na uwekezaji kama vile kununua vitabu vya shule, samani na visima vya maji. Takribani asilimia 73 ya wakazi 6,000 wa vijiji vya Makongeni na Gazi wanategemea visima vya maji viliyojengwa na mradi wa Mikoko Pamoja.
Na mradi huu bunifu hivi sasa umenakiliwa pia na wakazi wa maeneo Jirani yenye mikoko huko Vanga katika Kaunti ya Kwale na maeneo mengine yenye mikoko barani Afrika
Idhaa ya UN: Ni kwa vipi nchi zenu zinasongesha uchumi wa bahari usioharibu mazingira na hilo litakuwa na mchango gani kwenye mkutano huu?
Ana Paula Zacarias: Bahari ni msingi wa uhai duniani na hutupatia chakula lakini pia mambo mengine ya msingi ya maisha. Tunaweza kutumia bahari kwa burudani, utalii, michezo, usafirishaji na mambo mengine. Natumai kuwa mkutano huu utaongeza mambo hayo. Tutakuwa na majadiliano kuhusu uchumi endelevu kwa rasilimali za baharí ambako tutazungumzia kuhusu uchumi endelevu wa baharí; tunapaswa kufikiria uvuvi, bayonuai na utajiri ulioko chini ya baharí.
Martin Kimani: Kenya imepatia kipaumbele matumizi endelevu ya bahari na rasilimali zake ili kufanikisha ajenda yetu yam waka 2030. Kenya inaibuka kiuchumi na uchumi wa kupitia sekta ya bahari unatarajiwa kuchangia katika maendeleo yetu ya kiuchumi kupitia uhakika wa chakula, lishe ya uhakika, maendeleo ya pwani na vijijini na vipato kupitia mnyororo wa bidhaa za baharini, usafirishaji baharini na utalii.
Kando ya juhudi za kitaifa, Kenya inasalia kuwa mdau mwenye utashi wa kitaifa na kimataifa kusongesha harakati za kukabiliana na vitisho dhidi ya bahari
Idhaa ya UN: Nini dhima ya vijana katika mkutano wa Lisbon?
Martin Kimani: Tutakuwa na Jukwaa la Vijana kuhusu Bahari ambalo litatoa fursa ya kufahamu nafasi ya vijana katika kusongesha SDG14. Lazima tupatie vijana fursa ya kuweka maoni yao kwenye kusongesha uchumi utokanao na bahari.
Ukosefu wa ajira, hasa katika pwani ya Kenya huchochea vijana kwenye uhalifu, madawa ya kulevya na kutumbukia kwenye misimamo mikali ambayo hupelekea kwenye ugaidi.
Vitengo vya usimamizi wa Fukwe, au BMU hushirikiana na jamii katika kuajiri vijana wenye elimu rasmi na isiyo rasmi na kuwapatia mafunzo ya uhifadhi na hivyo baadaye kupata fursa za kijasiriamali na kupata vipato vya uhakika.