Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ombi la msaada wa kibinadamu kwa Yemen mwaka huu litakuwa dola bilioni 4.3

Mabinti watatu wakitembea kwenda shule katika eneo lenye vita huko Taizz, Yemen (Februari 2021)
© UNICEF/Ahmed Al-Basha
Mabinti watatu wakitembea kwenda shule katika eneo lenye vita huko Taizz, Yemen (Februari 2021)

Ombi la msaada wa kibinadamu kwa Yemen mwaka huu litakuwa dola bilioni 4.3

Msaada wa Kibinadamu

Takribani Wayemeni milioni 19 watakuwa na njaa katika miezi ijayo wakati Mashirika ya kutoa misaada yakitumai kuwafikia zaidi ya watu milioni 17 kati ya milioni 23.4 wanaohitaji msaada wa kuokoa maisha, ametangaza Naibu Katibu Mkuu katika Masuala ya Kibinadamu ambaye pia ni Mratibu wa Misaada ya Dharura, Martin Griffith wakati wa kuwasilisha ripoti yake kuhusu hali ya kibinadamu nchini Yemen kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hii leo Jumanne katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani. 

 

Martin Griffith akiiomba jumuiya ya kimataifa kutoisahau Yemen, ingawa baada ya miaka saba ya vita migogoro, mingine imaeiondoa kwenye vichwa vya habari ameeleza kuwa “njaa, maradhi na majanga mengine yanazidi kuongezeka nchini Yemen, na kuelemea rasilimali za mashirika ya kibinadamu yanayotaka kuyapunguza.”

Inakadiriwa kuwa katika miezi ijayo idadi ya watu wenye njaa itaongezeka kwa asilimia 20 ikilinganishwa na mwaka jana 2021.

Griffith kupitia mkutano huo ametangaza kwamba "mashirika ya misaada yanatafuta karibu dola bilioni 4.3 kusaidia zaidi ya watu milioni 17 kote nchini Yemen mwaka huu."

Akifafanua zaidi, Bwana Griffith ameeleza kuwa tathmini za hivi karibuni zaidi zinathibitisha kwamba watu wanaohitaji msaada wa dharura katika taifa hilo la Kiarabu sasa jumla yao ni milioni 23.4, ambayo ni karibu asilimia 75 ya watu wote.

Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Yemen Hans Grundberg

Naye Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa Yemen Hans Grundberg hii leo kupitia Baraza la Usalama ametoa wito kwa Wayemen na jumuiya ya kimataifa kuvunja "mzunguko usio na mwisho wa ghasia" huko Yemen, ambako vita vimeendelea kwa zaidi ya miaka saba.

"Tunahitaji juhudi za pamoja za Wayemeni na jumuiya ya kimataifa ili kuvunja mzunguko huu usio na mwisho wa vurugu na kuweka misingi ya amani ya kudumu." Bwana Grundberg amewaeleza wajumbe wa Baraza la Usalama. Akitolea mfano wa matukio ya hivi karibuni ameeleza kuendelea kwa uhasama katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita katika maeneo kadhaa nchini kote, ikiwa ni pamoja na ufyatulianaji wa risasi huko Taiz ambao ulisababisha vifo vya raia na mashambulizi ya anga kwenye mstari wa mbele huko Marib na Hajjah.

Pia Hans Grundberg kuhusu tukio la Februari 21 ambapo makombora kutoka kwenye ndege isiyo na rubani, yalijeruhi raia 16 katika uwanja wa ndege wa mji wa Jizan, Saudi Arabia.

Mkutano wa wafadhili kesho Machi 16

Awali Martin Griffiths, alikuwa amelikumbusha Baraza la Usalama kwamba mkutano wa wafadhili umeandaliwa kufanyika kesho Jumatano Machi 16, wakati mashirika ya kibinadamu yakiwa na uhitaji wa takribani dola bilioni 4.3 kusaidia zaidi zaidi ya watu milioni 17 kote Yemen mwaka huu. Tangu mwaka 2015, wafadhili wametumia karibu dola bilioni 14 kuitikia wito wa Umoja wa Mataifa wa kupunguza mateso yanayotokana na vita na kuporomoka kwa uchumi wa Yemen. Zaidi ya asilimia 75 ya fedha hizi hutoka kwa wafadhili sita ambao ni Marekani, Saudi Arabia, Uingereza, Umoja wa Falme za Kiarabu, Ujerumani na Kamisheni ya Ulaya.