UNDP na SUZA katika mapinduzi ya ukusanyaji takangumu Zanzibar

2 Juni 2022

Nchini Tanzania shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa maendeleo duniani, UNDP linashirikiana na Chuo Kikuu cha Taifa, SUZA visiwani Zanzibar kutekeleza mradi wa kuibuka na mbinu bora zaidi za kukusanya taka ngumu ili kufanikisha lengo namba 12 la malengo ya maendeleo endelevu, SDGs. 
 

Lengo hilo linamulika ulaji na uzalishaji unaowajibika unaohusisha pia usimamizi bora wa taka.

Peter Nyanda kutoka kitengo cha Ubunifu, UNDP Tanzania anasema mradi huo uko chini ya Programu iitwayo Accelerator Lab, WasteXLab. 

“Programu hii inajaribu kuleta njia mpya za ufanyaji kazi katika sekta ya maendeleo. Hutumia njia za kisasa kutatua changamoto kama vile kasi kubwa ya kukua kwa miji ambako kunachochea njaa, taka na magonjwa,” amesema Bwana Nyanda. 

Kwa kushirikiana na SUZA kupitia vijana wanafunzi na wahitimu wa Chuo hicho, mradi unawezesha vijana kutumia data au takwimu kutambua matatizo na kisha kuchochea kasi ya kufanikisha SDGs ikiwemo lengo namba 12. 

Mradi wa kuweka mapipa ya taka Zanzibar 

Mradi wa kuweka mapipa ya taka unaofanyika Zanzibar unaendelea ambapo wanachuo wa SUZA wanatumia simu kukusanya takwimu. 

Miongoni mwa washiriki hao ni Abdulhafidh Ali Juma, mhitimu wa Shahada ya Teknolojia ya Habari, Usimamizi wa Mifumo na Usimamizi, SUZA ambaye anasema, “ taka nyingi sasa hivi zinazalishwa mijini.  Zaidi ya asilimia 70 ya taka zinazaliwa mjini. Tunachukua takwimu katika maeneo ambayo yamewekewa mapipa ya taka na pia katika maeneo ambako hakuna mapipa lakini kuna taka zimetupwa.” 

Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar, SUZA nchini Tanzania wakikusanya takwimu zitakazosaidia mamlaka kutambua maeneo sahihi ya kuweka mapipa ya  kukusanyia taka.
UNDP Tanzania
Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar, SUZA nchini Tanzania wakikusanya takwimu zitakazosaidia mamlaka kutambua maeneo sahihi ya kuweka mapipa ya kukusanyia taka.

Takangumu nyingi hutupwa kiholela 

Zanzibar huzalisha takribani tani 663 za takangumu kila siku, kwa mujibu wa Mamlaka ya usimamizi wa mazingira, Zanzibar, ZEMA. 

Halmashauri ya Manispaa ya Mjini, na Halmashauri za Magharibi A na Magharibi B huzalisha takribni tani 216 za taka kila siku ambazo ni takribani nusu ya taka zote za Zanzibar. 

Ni tani 120 pekee ndio zinakusanywa na kutupwa katika dampo la Kibele huko Tunguu wilaya ya Kati. 

Kiwango kikubwa cha taka ambazo hazikusanywi hutupwa hovyo na kuharibu mazingira na hivyo kutishia afya, utalii na hata kuwa mazalia ya wadudu na wanyama wanaosambaza magonjwa. 

Mradi WasteX Lab unaleta faida gani? 

“Kwa hiyo mradi huu utasaidia serikali kufahamu ni eneo gani inahitaji kuwekewa pipa la taka, na wapi pipa la taka liondolewe lihamishiwe sehemu ambako linaweza kukusanya taka zaidi,” anasema Bwana Juma. 

Ametolea mfano wakati anakusanya takwimu eneo la Magogoni huko Zanzibar ambako anasema, “nimeingia Magogoni, shehiya nzima ya Magogoni hakuna hata sehemu moja yenye pipa la kukusanyia taka. Na ukitazama ni eneo ambalo lina idadi kubwa ya watu.” 

Bwana Juma amesema “takataka nyingi zimetupwa kwenye mitaro ambayo inaweza kusababisha mafuriko kwenye eneo hilo, na maradhi ya mlipuko yakija ina maana yataanzia pale. Kwa hiyo mradi huu UNDP itakapopeleka taarifa hili kwenye watu wa takwimu na Baraza la Mji, wanaweza kutambua kuwa hapa panahitaji tuweke pipa la taka ili kuepusha madhara kama vile maradhi ya mlipuko. Wizara ya Afya itakuwa imesaidiwa kupitia mradi huu, na Wizara nyingine nyingi tu.” 

UNDP itawasilisha takwimu mamlaka husika

Kwa Zamzam Juma Hamadi ambaye bado anasoma SUZA Shahada ya Teknolojia ya Habari, Usimamizi wa Mifumo na Usimamizi, mradi huu unaotekelezwa katika wilaya 3 za Mkoa wa Mjini, yaani Mjini Magharibi A, B na Mjini unaleta mapinduzi. 

“Kwa baadhi ya wazanzibari yaani kitu uchafu  hatukichukulii sana kama kitu kizito kwetu, tunakichukulia kawaida tu. Mtu anaweza kula hapo akatupa tu hapo hapo. Hajisikii vibaya kwamba akitupa kitu kinaweza kuleta madhara. Mfano udongo unaathirika. Udongo unatakiwa uwe na rutuba lakini unaweza kutupa ambacho hakihusiani, udongo unaweza kuharibika,” anasema Bi. Hamadi. 

Takwimu ambazo zinakusanywa zitasaidia mji kuwa safi “kwani sehemu ambazo hawakuanisha za kutupa taka, zinatupwa taka, kwa hiyo serikali itaweka mkazo zaidi katika kusafisha mji.” 

Hatimaye UNDP itawasilisha takwimu hizo serikalini kwa hatua zaidi. 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter