Matumizi endelevu ya bahari yaangaziwa Nairobi

27 Novemba 2018

Mkutano wa kimataifa kuhusu matumizi endelevu ya bahari kwa ajili ya ukuaji wa uchumi ukiingia siku ya pili hii leo huko Nairobi, Kenya, mwakilishi wa serikali ya Zanzibar kutoka Tanzania amezungumzia umuhimu wa bahari katika uchumi wa visiwa hivyo. 

Mshiriki  huyo Aboud Jumbe, mtaalamu wa mazingira, kutoka Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira ya serikali ya mapinduzi ya Zanzibar, SMZ amesema hayo wakati huu ambapo washiriki wa mkutano huo wanaangazia pamoja na mambo mengine umuhimu wa kuwa na maeneo yaliyotengwa ya baharini kwa ajili ya matumizi endelevu ya bahari.

Bwana Jumbe amesema, “Uchumi wa bahari ni kitovu cha maisha yetu, kwa Zanzibar, kwa Tanzania,  usafiri wa  baharini, masuala ya uvuvi masuala ya nishati, nishati ya mafuta na gesi.  Cha muhimu ni kwamba ni lazima tunapofanya mambo yote hayo kuangalia upeo wa mazingira, uhifadhi wa mazingira na jamii katika eneo zima la usimamizi wa uchumi huo.”

 Mtaalamu huyu wa mazingira akaenda mbali kuelezea manufaa ya uchumi wa bahari kwa Zanzibar.“Kwa nchi yetu,  uchumi wa baharí unachangia kiasi cha asilimia 33 ya GDP ya taifa. Na ni muhimu kwamba katika mipango yote ya kiuchumi, kijamii na kimazingira, suala zima la uenzi na uhifadhi wa baharí yetu pamoja na fukwe zetu kwa maslahi ya taifa, jamii, maendeleo ya utalii, uvuvi na mengine yanahifadhiwa.”

Mkutano huo unahudhuriwa na wakuu wa nchi na serikali, wataalamu, wasomi na wawakilishi wa vikundi vya kiraia.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter