Mradi wa Sola wa UNICEF watatua changamoto za waathirika wa ukame Kori Ethiopia 

20 Mei 2022

Mradi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF wa kuweka paneli za sola kwa ufadhili wa mfuko wa dharura wa Umoja wa Mataifa CERF umeleta nuru kwa maelfu ya waathirika wa ukame katika eneo la Kori jimboni Afar nchini Ethiopia hasa tatizo la maji.

Jimbo la Afar Kaskazini mwa Ethiopia linakabiliwa na ukame mkali kuwahi kushuhudia katika historia yake.  

Maelfu ya watu wameathirika vibaya ikiwemo katika Kijiji cha Kori ambako sasa UNICEF imechukua hatua ya kuwasaidia wakazi walio hatarini zaidi kama Zara mama anayejitahidi kufanya kila awezalo kuwapatia maji na chakula watoto wake. 

Na asante kwa mfuko wa dharura wa Umoja wa Mataifa CERF sasa pampu ya kusukuma maji inayotumia paneli za sola imewekwa kijijini hapa ili kukabiliana na changamoto ya maji iliyosababishwa na upungufu wa mafuta. Zara anasema,“Kabla ya pumpu hii tulipata shida sana kutokana na ukata wa mafuta, ili kuweza kununua mafuta waendeshaji wa pumpu iliwabidi kwenda Semera zaidi ya kilometa 130 kutoka hapa. Wakati mwingine tulikuwa tunakaa bila maji kwa siku moja ama mbili. Lakini tangu walipotuwekea paneli za sola tunapata maji kila wakati hata wakati wa jua kali.” 

Mradi huo wa UNICEF sasa unawanufaisha takriban wakazi 10,500, ambapo 4,500 kati yao wanatoka katika vijiji vya Jirani.  

Mbali ya watu UNICEF imejenga mfereji mkubwa wa maji ili kuisaidia mifugo pia kunywa wakiwemo ng’ombe na mbuzi. 

Na haya ni matumaini makubwa yaliyoletwa na UNICEF kwa jamii hii iliyoathirika vibaya na ukame. 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter