Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wenye ukoma bado wabaguliwa Angola; Mtaalamu apaza sauti

Mtu mwenye ukoma, Addis Abba, Ethiopia, April 2002
ILO/Fiorente A.
Mtu mwenye ukoma, Addis Abba, Ethiopia, April 2002

Wenye ukoma bado wabaguliwa Angola; Mtaalamu apaza sauti

Afya

Nchini Angola hali ya wagonjwa wa ukoma bado ni tete kutokana na ubaguzi wanaokumbana nao wao Pamoja na familia zao, amesema mtaalamu huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu utokomezaji wa ubaguzi dhidi ya wagonjwa wa ukoma, Alice Cruz mwishoni mwa ziara yake ya wiki mbili nchini humo. 

Taarifa ya ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu iliyotolewa leo huko Luanda, Angola, imemnukuu Bi. Cruz amesema pamoja na kukaribisha ahadi ya serikali ya Angola ya kushirikiana na mifumo ya haki za binadamu ya kimataifa na kutokomeza ubaguzi unaokumba watu wenye ukoma, bado mamlaka zinapaswa kuongeza maradufu hatua za kufanikisha lengo hilo. 

“Nina wasiwasi mkubwa kuw aidadi kubwa ya wagonjwa wanachelewa kupata huduma za uchunguzi, hali inayoweza kusababisha ugonjwa kukomaa na kuleta madhara yasiyoweza kupatiwa matibabu sambamba na huduma za uragibishi, upasuaji wa kurejesha viungo kwenye hali ya kawaida na hata vifaa vya kusaidia wagonjwa kumudu Maisha yao,” amesema Bi. Cruz. 

Angola haijajiandaa 

Mtaalamu huyo maalum amesema cha kusikitisha zaidi, mfumo wa afya Angola haujajiandaa kushughulikia tatizo la ukoma. 

Amesihi mamlaka kupatia kipaumbele masuala kadhaa ikiwemo ukusanyaji wa data zitakazotumika kutunga sera sahihi kuhusu ukoma, kuhakikisha watu wenye ukoma wanapata taarifa na kuwepo na uwajibikaji kwa vitendo halifu dhidi yao; mifumo ya ufuatiliaji na tathmini sambamba na bajeti ya kutosha kuanzia ngazi ya chini hadi ya taifa. 

“Takwimu kuhusu ugonjwa wa ukoma si za uhakika. Kama vile serikali inatambua, kuna uwezekano taarifa kuhusu wakoma ni za chini kuliko ukweli sahihi na hii inaweza kuongeza hali ya maambukizi, na ulemavu utokanao na ukoma hasa miongoni mwa Watoto,” amesema Bi. Cruz. 

Halikadhalika ametaka wale wanaokiuka haki za binadamu za wakoma na familia zao wawajibishwe. 

Wakati wa ziara yake. Bi. Cruz alikuwa na mazungumzo na wawakilishi wa serikali, mashirika ya kiraia, wasomi, wahudumu wa afya. 

Alitembelea pia kituo cha wagonjwa wa Kifua Kikuu na Ukoma ambako alikutana na wagonjwa na familia zao. 

Ripoti yake ataiwasilisha mbele ya Baraza Kuu la Haki za Binadamu mwezi Juni mwaka 2023. 

Ukoma ni nini? 

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO, Ukoma ni ugonjwa hatari unaoambukiza na husababishwa na kimelea aitwae Mycobacterium leprae,. 

 Ugonjwa huathiri ngozi na mishipa ya fahamu iliyo karibu na ngozi sambamba na mfumo wa hali ya hewa na macho. 

 Ukoma hutibika katika awamu ya mwanzo na tiba ikichelewa mgonjwa anaweza kupata ulemavu.