Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Acheni kutumia ukoma kwa manufaa yenu kisiasa-UN

Mgonjwa wa ukoma. (Picha:UN /Tim McKulka)

Acheni kutumia ukoma kwa manufaa yenu kisiasa-UN

Amani na Usalama

Viongozi wa kisiasa nchini Italia na Ufaransa wameshauriwa  kuacha mara mojakufanisha ukoma na masuala yao ya kisiasa.

Onyo hilo limetolewa leo jumanne mjini Geneva Uswisi na mtaalam wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya utokomezaji na kuondoa  ubaguzi dhidi ya wagonjwa  wa ukoma na familia zao, Alice Cruz.

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa alinukuliwa akisema wazalendo utawaona wanaongezeka kidogo kama ukoma barani kote Ulaya, kwenye nchi ambazo ingalikuwa si rahisi kuwaona tena hasa kwenye nchi jirani.

Kauli yake ilimuibua Naibu Waziri Mkuu wa Italia, Luigi Di Maio ambaye amesema ukoma mahsusi ni undumilakuwili wa Ulaya hasa kwa yule anayerejesha makwao wahamiaji huko Ventimiglia halafu anaanza kuhubiri jinsi ya kuwatunza.

Ventimiglia ni mji ulioko mpakani mwa Italia na Ufaransa.

Ni kutokana na kauli hizo mtaalamu Cruz amesisitiza kuwa matumizi ya maneno na marejeleo kuhusu ukoma katika mijadala ya kisiasa inaendeleza tu kutoelewana kuhusu ukoma na pia ubaguzi dhidi ya watu ambao wameathirika na ugonjwa huo.

Ameongeza kuwa  ukoma sasa si ugonjwa tena bali kuufananisha na kitu chochote kile ambacho kinachukuliwa na jamii kuwa ni aibu ni jambo lisilofaa.

Bi. Cruz amesema viongozi wa kitaifa wanafaa kutumia maneno kwa uangalifu na wanafaa kuepuka kushambulia  makundi ambayo bado yanatengwa.