Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yazindua ripoti ya kwanza kabisa ya kimataifa kuhusu kuzuia na kudhibiti maambukizi 

Mfanyikazi wa afya huvaa PPE katika kliniki ya kupima COVID nchini Mauritius.
© UNDP Mauritius/Stephae Bellar
Mfanyikazi wa afya huvaa PPE katika kliniki ya kupima COVID nchini Mauritius.

WHO yazindua ripoti ya kwanza kabisa ya kimataifa kuhusu kuzuia na kudhibiti maambukizi 

Afya

Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa, WHO limezindua ripoti ya kwanza kabisa ya kimataifa kuhusu njia ya vitendo, yenye msingi wa ushahidi wa kulinda wagonjwa na wahudumu wa afya wasidhuriwe na maambukizi yanayoweza kuepukika.  

Ripoti hiyo “Kuzuia na Kudhibiti Maambukizi” imezinduliwa leo mjini Geneva, Uswisis na kupitia taarifa yake WHO imesema janga la COVID-19 na milipuko mingine mikubwa ya maonjwa ya hivi karibuni imeonesha kiwango ambacho mipangilio ya huduma za afya inaweza kuchangia kuenea kwa maambukizi, kuwadhuru wagonjwa, wahudumu wa afya na wageni, ikiwa tahadhari ya kutosha haitaelekezwa katika kuzuia na kudhibiti maambukizi (IPC).  

Pia ripoti hiyo mpya inaonesha kuwa pale ambapo usafi mzuri wa mikono na taratibu nyingine za gharama nafuu zinafuatwa, asilimia 70 ya maambukizi hayo yanaweza kuzuilika au kuepukika.  

Hali halisi kote duniani 

WHO inasema leo hii, kati ya kila wagonjwa 100 katika hospitali za wagonjwa wa papo hapo, wagonjwa saba katika nchi za kipato cha juu na wagonjwa 15 katika nchi za kipato cha chini na cha kati watapata angalau ugonjwa mmoja unaohusishwa na huduma ya afya (HAI) wakati wanapokuwa wamelazwa hospitalini.  

Kwa wastani, 1 kati ya wagonjwa 10 walioathiriwa atakufa kutokana na ugonjwa huo. 

Watu ambao ni wagonjwa mahututi na watoto wachanga wako hatarini. Na ripoti hiyo inafichua kwamba takriban kisa kimoja kati ya vinne vya maambukizi vilivyotibiwa hospitalini na karibu nusu ya visa vyote vya maambukizi vilivyo na upungufu wa viungo vinavyotibiwa katika vyumba vya wagonjwa mahututi vinahusishwa na huduma za afya. 

WHO leo inatathimini ripoti hiyo ya kwanza ya kimataifa ya kuzuia na kudhibiti maambukizi ambayo imeleta pamoja ushahidi kutoka kwa maandiko ya kisayansi na ripoti mbalimbali, na takwimu mpya kutoka kwa tafiti za WHO. 

"Janga la COVID-19 limefichua changamoto na mapungufu mengi katika mikoa na nchi zote, ikiwa ni pamoja na zile ambazo zilikuwa na programu za IPC za hali ya juu," amesema Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu wa WHO. 

"Pia imetoa fursa ambayo haijawahi kushuhudiwa kutathmini hali hiyo na kuongeza kwa haraka utayari wa kuzuka na kukabiliana na mlipuko kupitia mazoea ya IPC, pamoja na kuimarisha programu za IPC katika mfumo mzima wa afya. Changamoto yetu sasa ni kuhakikisha kuwa nchi zote zina uwezo wa kutenga rasilimali watu, vifaa na miundombinu inayohitajika.” Ameongeza mkuu huyo wa WHO. 

Muhudumu wa afya akitoa taarifa kuhusu COVID-19 kwa mgonjwa kwenye kituo cha afya Jerusalem.
© UNRWA/Louise Wateridge
Muhudumu wa afya akitoa taarifa kuhusu COVID-19 kwa mgonjwa kwenye kituo cha afya Jerusalem.

Hii ni tathimini ya kwanza  

Ripoti hiyo mpya ya WHO inatoa uchanganuzi wa kwanza kabisa wa hali ya kimataifa wa jinsi programu za IPC zinavyotekelezwa katika nchi kote ulimwenguni, ikiwa ni pamoja na malengo ya kikanda na nchi.  

Huku ikiangazia madhara kwa wagonjwa na wahudumu wa afya yanayosababishwa na HAIs na usugu wa viua vijidudu, ripoti hiyo pia inashughulikia athari na ufanisi wa gharama ya programu za kuzuia na kudhibiti maambukizi na mikakati na rasilimali zinazopatikana kwa nchi kuziboresha. 

Athari za maambukizo yanayohusiana na huduma ya afya na usugu wa dawa kwa maisha ya watu hazihesabiki.  

WHO imesema zaidi ya asilimia 24% ya wagonjwa walioathiriwa na maambukizi yanayohusiana na huduma za afya na asilimia 52.3% ya wagonjwa hao wanaotibiwa katika kitengo cha wagonjwa mahututi hufa kila mwaka.  

Vifo huongezeka mara mbili hadi tatu wakati maambukizi yanapokuwa sugu kwa dawa za viuavijasumu. 

Katika miaka mitano iliyopita, WHO imefanya tafiti za kimataifa na tathmini za pamoja za nchi ili kubaini hali ya utekelezaji wa programu za kitaifa za IPC.  

Ukilinganisha takwimu kutoka tafiti za mwaka 2017-18 na 2021-22, asilimia ya nchi zilizo na programu za kitaifa za IPC hazikuboreka,  zaidi ya hayo mwaka 2021-22 ni nchi nne tu kati ya 106 zilizofanyiwa tathmini (3.8%) zilikuwa na mahitaji yote ya chini ya IPC katika ngazi ya kitaifa.  

Hii inaonekana katika kutotekelezwa ipasavyo kwa mazoea ya IPC katika hatua ya kutoa huduma, huku kukiwa na asilimia 15.2 tu ya vituo vya afya vinavyokidhi mahitaji yote ya chini ya IPC, kulingana na utafiti wa WHO wa mwaka 2019. 

Kuna hatua zimepigwa 

Hata hivyo, maendeleo ya kutia moyo yamepatikana katika baadhi ya maeneo, huku ongezeko kubwa likionekana katika asilimia ya nchi kuwa na kituo maalum cha IPC, bajeti maalum ya IPC na mtaala wa mafunzo ya wahudumu wa afya walio mstari wa mbele, kuandaa miongozo ya kitaifa ya IPC na mpango wa kitaifa au mpango wa ufuatiliaji wa HAI, kutumia mikakati ya aina nyingi za uingiliaji kati wa IPC, na kuanzisha uzingatiaji wa usafi wa mikono kama kiashirio kikuu cha kitaifa. 

Nchi nyingi zinaonyesha ushirikishwaji thabiti na maendeleo katika hatua za kuongeza juhudi ili kuweka mahitaji ya chini kabisa na vipengele vya msingi vya programu za IPC.  

Maendeleo yanaungwa mkono kwa nguvu na WHO na wahusika wengine wakuu. Kudumisha na kupanua zaidi wigo wa maendeleo haya kwa muda mrefu ni hitaji muhimu ambalo linahitaji umakini wa haraka na uwekezaji kwa mujibu wa shirika hilo la afya. 

Ripoti inaonyesha kuwa nchi zenye mapato ya juu zina uwezekano mkubwa wa kuendeleza kazi zao za IPC, na zina uwezekano mara nane zaidi wa kuwa na hadhi ya juu zaidi ya utekelezaji wa IPC kuliko nchi zenye mapato ya chini.  

WHO inasema, uboreshaji mdogo ulionekana kati ya mwaka 2018 na 2021 katika utekelezaji wa programu za kitaifa za IPC katika nchi zenye mapato ya chini, licha ya kuongezeka kwa umakini kwa IPC kutokana na janga la COVID-19.  

WHO itaendelea kuunga mkono nchi kuhakikisha mipango ya IPC inaweza kuboreshwa katika kila eneo. 

Pia inatoa wito kwa nchi zote duniani kuongeza uwekezaji wao katika mipango ya IPC ili kuhakikisha ubora wa huduma na usalama wa wagonjwa na wafanyakazi wa afya.  

Hii haitalinda tu idadi ya watu, kuongezeka kwa uwekezaji katika IPC pia kumeonyesha kuboresha matokeo ya afya na kupunguza gharama za huduma za afya kutoka mfukoni mwa watu.