Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Walinda amani wa Burundi wauawa Somalia; Guterres atuma rambirambi 

Mtazamo wa mitaa ya kaskazini mwa Mogadishu kupitia shimo lililoachwa na risasi kwenye dirisha ya hoteli Somalia.
UN Photo/Stuart Price
Mtazamo wa mitaa ya kaskazini mwa Mogadishu kupitia shimo lililoachwa na risasi kwenye dirisha ya hoteli Somalia.

Walinda amani wa Burundi wauawa Somalia; Guterres atuma rambirambi 

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani vikali mashambulizi yaliyofanywa Jumatatu tarehe 2 mwezi huu wa Mei na kikundi cha kigaidi cha Al Shabaab dhidi ya ujumbe wa mpito wa Muungano wa Afrika nchini Somalia, ATMIS, shambulio lililosababisha vifo vya walinda amani kutoka Burundi. 

Taarifa iliyotolewa jijini New York, Marekani  na msemaji wa Umoja wa Mataifa  Stéphane Dujarric inasema shambulio hilo lilitokea katika kituo cha ATMIS cha walinda amani kutoka Burundi huko Shabelle ya kati nchini Somalia. 

Vyombo vya habari vinaripoti kuwa walinda amani 10 kutoka Burundi waliuawa huku wengine 25 walijeruhiwa baada ya Al Shabaab kuvamia kambi yao. 

“Katibu Mkuu anatuma salamu za rambirambi kwa familia za waliopoteza maisha pamoja na serikali na wananchi wa Burundi. Anatakia ahueni ya haraka majeruhi,” imesema taarifa hiyo. 

Guterres pia ameshukuru walinda wanajeshi wa ATMIS kwa huduma yao na azma yao ya kuhakikisha kuna amani na usalama nchini Somalia. 

“Natoa wito kwa jamii ya kimataifa kupatia ATMIS na vikosi vya ulinvi vya Somalia msaada muhimu unaohitajika  ili kuweza kukabiliana na AL Shabaab” amesema Guterres kwenye taarifa hiyo. 

Kutoka AMISOM hadi ATMIS 

ATMIS imechukua majukumu ya ujumbe wa zamani wa Muungano wa Afrika nchini Somalia, AMISOM, kufuatia uamuzi wa Baraza la Amani na Usalama la Muungano wa Afrika uliotolewa tarehe 8 mwezi Machi mwaka huu wa 2022 katika mkutano wake wa 1068. 

Uamuzi huo unapatia ATMIS mamlaka ya kusaidia serikali ya shirikisho ya Somalia katika utekelezaji wa mpango wake wa mpito pamoja na kumpango wa kuhamishia majukumu ya usalama kwenda majeshi na taasisi za ulinzi za Somalia.