Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Poleni wananchi wa Somalia kutokana na shambulizi kutoka Al Shabaab- UN

Askari polisi wanaohudumu chini ya ujumbe wa mpito wa Muungano wa Afrika nchini Somalia (ATMIS) wakiwa kwenye doria ya pamoja na polisi wa Somalia ili kuimarisha usalama wakati wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani tarehe 20 Machi mwaka 2023 kwenye mji mkuu wa S…
ATMIS / Mukhtar Nuur
Askari polisi wanaohudumu chini ya ujumbe wa mpito wa Muungano wa Afrika nchini Somalia (ATMIS) wakiwa kwenye doria ya pamoja na polisi wa Somalia ili kuimarisha usalama wakati wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani tarehe 20 Machi mwaka 2023 kwenye mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.

Poleni wananchi wa Somalia kutokana na shambulizi kutoka Al Shabaab- UN

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ameleaani vikali shambulizi kubwa la hivi karibuni dhidi ya kituo cha ujumbe wa mpito wa Muungano wa Afrika nchini Somalia (ATMIS) huko Buulo Mareer eneo la Lower Shabelle nchini Somalia, kituo ambacho watendaji wake ni wanajeshi kutoka Uganda.

Taarifa iliyotolewa leo Jumamosi na msemaji wa Umoja wa Mataifa, licha ya kutotaja idadi ya waliouawa au waliojeruhiwa kwenye shambulio la Ijumaa, imemnukuu Katibu Mkuu akituma salamu za rambirambi kwa familia za waliouawa, serikali ya Uganda na wananchi wa Uganda huku akiwatakia ahueni ya haraka majeruhi.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari, wapiganaji wa kikundi cha kigaidi cha Al Shabaab walishambulia kituo hicho kilicho kilimeta 120 kusini-magharibi mwa mji mkuu wa Somalia, Mogadishu kwa kutumia gari lililokuwa limebeba vilipuzi pamoja na watu waliokuwa wamevaa mabomu ambapo idadi kubwa ya askari wa Uganda na Al Shabaab wameuawa.

Katibu Mkuu ametoa shukrani kwa wanajeshi wa ATMIS na kuelezea shukrani zake kwa huduma na mchango wao katika kusaka amani na utulivu Somalia.

“Ninasisitiza wito wangu kwa jamii ya kimataifa kusaidia ATMIS na majeshi ya Somalia katika harakati zao za kupambana na misimamo mikali nchini humo,” amenukuliwa Katibu Mkuu.

Ujumbe wa mpito wa Muungano wa Afrika nchini Somalia ulianzishwa tarehe Mosi mwezi Aprili mwaka 2022 kufuatia kumalizika kwa muda wa ujumbe wa Mungano wa Afrika nchini Somalia, AMISOM tarehe 31 mwezi Machi mwaka 2022.

ATMIS imejikita katika kujengea serikali ya Somalia uwezo wa kijeshi na kitaasisi  wakati huu ambapo Muungano wa Afrika unajiondoa taratibu Somalia.

Muda wa ATMIS utamalizika tarehe 31 mwezi Desemba mwaka 2024.