Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtambo wa Zaporizhzhia uko salama licha ya kudhibitiwa na Urusi - Grossi

Rafael Mariano Gross, Mkurugenzi Mkuu wa IAEA akizungumza na waandishi wa habari.
IEA/Dean Calmaa
Rafael Mariano Gross, Mkurugenzi Mkuu wa IAEA akizungumza na waandishi wa habari.

Mtambo wa Zaporizhzhia uko salama licha ya kudhibitiwa na Urusi - Grossi

Amani na Usalama

Shirika la Umoja wa Mataifa la nishati ya atomiki, IAEA limesema hadi sasa hakuna dalili zozote za kuvuja kwa mionzi ya nyuklia kutoka katika mtambo wa nyuklia wa Zaporizhzhia nchini Ukraine ambao hivi sasa uko chini ya udhibiti wa majeshi ya Urusi yaliyovamia taifa hilo la Ulaya.

Taarifa hizo zimetolewa leo na Mkurugenzi Mkuu wa IAEA Rafael Mario Grossi wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi akisema kuwa walijulishwa na Ukraine kuhusu kutwaliwa huko kwa mtambo wa nyuklia.

Hata hivyo Ukraine imeijulisha IAEA kuwa mtambo huo ingawa unadhibitiwa na majeshi ya Urusi, bado wafanyakazi wa Ukraine ndio wanauendesha na hakuna uvujaji wowote wa miali ya nyuklia.

Kuhusu moto uliowaka kwenye mtambo huo, Bwana Grossi amefafanua kuwa “wadau wa Ukraine waliijulisha IAEA kuwa kombora lililorushwa usiku wa jana lilipiga jengo kwenye moja ya vinu vya mtambo huo na kusababisha moto ambao hata hivyo baadaye ulizimwa.”

Amefafanua kuwa mifumo ya usalama katika vinu vyote sita vya mtambo huo wa nyuklia havikupata zahma yoyote na hakuna miali ya nyuklia iliyovuja wakimaanisha kuwa mifumo ya ufuatiliaji wa miali na minururisho bado inafanya kazi.

Hata hivyo, mwendeshaji wa mtambo huo ameripoti kuwa hali inasalia kuwa ya changamoto kubwa na kwamba bado hawajaweza kuwa na tathmini kamilifu ya eneo zima kubaini iwapo mifumo hiyo inafanya kazi kwa kina.

Katika vinu vyote sita, kinu namba 1 kimefungwa kwa matengenezo, kinu namba 2 na namba 3 kinafungwa taratibu, kinu namba 4 kinafanya kazi kwa asilimia 60 ilhali kinu namba 5 na 6 viko katika kiwnago cha chini cha utoaji nishati kwa lengo la kuweka akiba.

IAEA iko katika mfumo wa dharura hivi sasa 

Kwa sasa IAEA iko katika mfumo wa dharura kutokana na hali inayoendelea kwenye mtambo wa nyuklia wa Zaporizhzhia na taarifa zitakuwa zinatolewa kila wakati.

Kwa sasa IAEA lengo lake ni kuhakikisha usalama wa mtambo huo na wa watu wanaouendesha.
“Nina wasiwasi mkubwa na hali katika mtambo wa Zaporizhzhia na kile kilichotokea usiku. Mashambulizi ya makombora kwenye eneo hilo la mtambo wa nyuklia ni kinyume na misingi  ya kwamba maeneo ya mitambo ya nyuklia lazima yasalie salama,” amesema Grossi.