Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtoto mwenye umri wa miezi 11 miongoni mwa watoto 21 waliouawa Darfur Magharibi- UNICEF

Watoto wakicheza nje ya nyumba yao kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani huko El Fasher, Sudan.
© UNICEF/Shehzad Noorani
Watoto wakicheza nje ya nyumba yao kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani huko El Fasher, Sudan.

Mtoto mwenye umri wa miezi 11 miongoni mwa watoto 21 waliouawa Darfur Magharibi- UNICEF

Amani na Usalama

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limeelezea masikitiko yake juu ya ripoti za mauaji ya watoto wapatao 21 huko Darfur magharibi nchini Sudan.

 

Mkurugenzi wa UNICEF kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini, Adele Khod amenukuliwa katika taarifa ya UNICEF iliyotolewa leo mjini Amman, Jordan akisema kuwa miongoni mwa waliouawa ni mtoto mwenye umri wa miezi 11.

Tukio hilo limetokea huko Kerinik, Darfur Magharibi wakati huu ambapo kwa siku kadhaa kumekuweko na ghasia za baina ya watu wenye asili ya kiarabu na wasio waarabu.

Taarifa ya UNICEF inasema, “mauaji ya watoto ni ukiukwaji mkubwa wa haki zao za msingi. Hakuna kitu chochote kinachoweza kuhalalisha mauaji yao.”

UNICEF imerejelea wito wake wa kuweko kwa amani na kutoa wito kwa mamlaka nchini Sudan zilinde watoto huko Darfur na kwingineko dhidi ya ghasia wakati wowote ule.

Shirika hilo limekumbusha kuwa katu watoto hawapaswi kuwa wanalengwa waktai wa mizozo.

Mapema wiki hii, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alilaani mashambulizi ya jumapili huko Darfur magharibi, mashambulizi ambayo yalisababisha vifo vya watu 168.