Migogoro ya kijamii nchini Chad yawalazimisha watu 8,300 kukimbilia Darfur

25 Februari 2020

Zaidi ya watu 6000 nchini Chad, wakwiemo  wanaume, wanawake na watoto wamekimbilia katika mji wa Tina na Karnoi huko Kaskazini mwa Darfur Sudan kutokana na mapigano kati ya makundi tofauti ya kabila la Zaghawa katika eneo la Tina, upande wa pili wa mpaka nchini Chad, imeeleza taarifa ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR iliyochapishwa hii leo.

Aidha watu wengine takribani 2300 wametawanywa kutoka Chad kuingia Jebel huko Darfur Magharibi. UNHCR na wadau wake wanatoa msaada wa haraka wakati tahimini kuhusu hali ikiendelea.

Taarifa hiyo ya UNHCR imekumbushia kuwa mnamo tarehe 13 na tarehe 14 mwezi huu wa Februari, mapigano yaliibuka kati ya makundi madogo ya kabila la Zaghawa hususani katika miji ya Tina, Duguba na Iriba mashariki mwa Chad.

Zaidi ya watu 6000 tangu wakati huo wamefika katika maeneo ya vijijini ya Tina Kaskazini mwa Darfur, miongoni mwao raia wa Sudan ambao wana hadhi ya ukimbizi nchini Chad, raia wa Chad na pia raia wa Sudan ambao wanaishi upande wa pili wa Sudan nje ya mpaka wa nchi yao.

 Mamlaka za kijamii nchini Sudan zimeunda kamati ya kuwaandikisha wanaowasili. Takribani watu 100 wamerejea katika vijiji vyao vya asili katika maeneo ya Karnoi, Sudan na walipokelewa na mamlaka za maeneo hayo. Hali nchini Chad bado ni tete na kwa mujibu wa ripoti, mapigano na utawanyaji watu unaendelea.

UNHCR kwa kushirikiana na wadau wengine wamefanya tathimini ya pamoja na kubaini kuwa watu wapya wanaowasili hivi sasa hawana makazi. WFP na UNHCR wamelazimika kuanza kugawa vyakula tangu jana tarehe 23 ya mwezi huu wa Februari, kwa watu 5000.

 Watu waliko hatarini, kama wajawazito na wale walio na magonjwa kama kuhara na utapiamlo hawawezi kupata dawa ambazo wangezihitaji.

 

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter