Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres alaani mauaji ya raia Darfur 

Walinda amani kutoka UNAMID wakitoa ulinzi kwa wanawake wenyeji wa kijiji cha Aurokuom eneo la Zalingei, Darfur Kati.
UNAMID/Amin Ismail
Walinda amani kutoka UNAMID wakitoa ulinzi kwa wanawake wenyeji wa kijiji cha Aurokuom eneo la Zalingei, Darfur Kati.

Guterres alaani mauaji ya raia Darfur 

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani vikali mauji ya raia kwenye kitongoji cha Kreinik huko Darfur Magharibi nchini Sudan. 

Mauaji hayo yalifanyika jana jumapili ambapo vyombo vya habari vinaripoti kuwa watu 168 waliuawa wakati wa mapigano ya kikabila kati ya watu wa jamii ya kiarabu na wasio na asili ya kiarabu. 

Taarifa iliyotolewa leo jijini New  York, Marekani na Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq inamnukuu Katibu Mkuu akitoa wito wa kukoma mara moja kwa ghasia hizo huku akituma salamu za rambirambi kwa familia za waliopoteza maisha na kutakia ahueni ya haraka waliojeruhiwa. 

Katibu Mkuu amesisitiza kuwa juu umuhimu na wajibu wa msingi wa serikali ya Sudan wa kulinda raia. 

“Ametambua juhudi zinazofanywa na serikali ya Sudan ya kushughulikia zahma hiyo ya mapigano ikiwemo azma yake ya kuhamisha raia waliojeruhiwa,” imesema taarifa hiyo. 

Halikadhalika Katibu Mkuu ametaka kuongezwa kasi ya kupeleka vikosi vya pamoja vya ulinzi kwa mujibu wa Mkataba wa Amani wa Juba. 

Bwana Guterres amesisitiza umuhimu wa kuimarisha usalama huko Darfur ikiwemo kupitia utekelezaji wa Mkataba wa Amani wa Juba. 

Mkataba wa Amani wa Juba ulitiwa saini tarehe 3 mwezi Oktoba mwaka 2020 huko Juba nchini Sudan Kusini kwa lengo la kutatua mzozo wa wenyewe kwa wenyewe ambao umesababisha mamia ya maelfu ya watu kupoteza maisha huku mamilioni wakiwa wakimbizi ndani na nje ya nchi yao. 

Halikadhalika kuimarisha utawala wa sheria na kutekeleza kwa kikamilifu mpango wa kitaifa wa ulinzi wa raia. 

Pamoja na wito huo pia Bwana Guterres ametaka ufikishaji wa misaada ya kibinadamu kwa raia usiwe na vikwazo vyovyote huku akitaka uchunguzi huru wa mauaji hayo ili wahusika wa mapigano hayo ya kikabila wawajibishwe.