Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres atoa wito wananchi walindwe wakati machafuko yakiongezeka magharibi mwa Darfur

Mtazamo kutoka angani wa Geneina, magharibi mwa Darfur nchini Sudan ambako kunashuhudiwa mgogoro wa kikabila.
UNAMID/Hamid Abdulsalam
Mtazamo kutoka angani wa Geneina, magharibi mwa Darfur nchini Sudan ambako kunashuhudiwa mgogoro wa kikabila.

Guterres atoa wito wananchi walindwe wakati machafuko yakiongezeka magharibi mwa Darfur

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ameelezea wasiwasi mkubwa kuhusu kuendelea kwa mapigano magharibi mwa Darfur na kutoa wito kwa mamlaka nchini Sudan kufanya kila juhudi kumaliza mapigano hayo na kulinda raia.

Kwa mujibu wa duru za vyombo vya habari, takriban watu 83 ikiwemo wanawake na watoto wameuawa na zaidi ya 160 wamejeruhiwa katika mapigano ya kikabila mwishoni mwa juma liliopita. 

Nyumba kadhaa zinadaiwa kuharibiwa na karibu watu 50,000 wamefurushwa makwao. 

Kupitia taarifa ya msemaji wa Katibu Mkuu iliyotolewa Jumapili, Katibu Mkuu amehimiza mamlaka kusiitisha mapigano, kurejesha sheria na utulivu na kuhakikisha ulizni wa raia kwa mujibu wa mpango wa serikali wa kitaifa wa kulinda raia. 

Bwana Guterres ametuma rambirambi zake kwa familia ya waliopoteza maisha na kuwatakia afueni ya haraka majeruhi. 

Ukatili huo umetokea ikiwa ni takriban wiki mbili tangu ujumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika (UNAMID) kulimaliza operesheni zake mwishoni mwa mwaka 2020. 

UNAMID inapunguza vikosi vyake na mchakato unatarajiwa kumalizika mwishoni mw aJuni 2021.