Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF DRC yawezesha wanafunzi kujivunia shule yao 

Christian Ngwe, kiranja katika shule ya msingi ya Nganda Yala jijini Kinshasa nchini DRC, akiwa amepiga picha mbele ya jengo la vyoo vipya vya shule yao.
© UNICEF/Jean-Claude Wenga
Christian Ngwe, kiranja katika shule ya msingi ya Nganda Yala jijini Kinshasa nchini DRC, akiwa amepiga picha mbele ya jengo la vyoo vipya vya shule yao.

UNICEF DRC yawezesha wanafunzi kujivunia shule yao 

Afya

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF kwa msaada kutoka eneo la mji mkuu wa Ubelgiji, Brussels, limeimarisha huduma za usafi na kujisafi WASH, kwenye shule moja mjini Kinshasa na hivyo kuwezesha wanafunzi kujifunza katika mazingira safi na salama.

Eneo ni N’sele, kitongoji katika mji mkuu wa DR Congo, Kinshasa, azungumzaye ni Mkuu wa program ya kitaifa ya afya shuleni. 

Anasema shule hii ya msingi ya Nganda Yala iliyoko kwenye eneo hili kwa miaka mingi imekumbwa na matatizo mengi ikiwemo ya kiafya. Nazungumzia vyoo ambavyo  havikuwa katika hali nzuri! 

Kauli ya afisa huyo ilikuwa ni wakati wa tukio la shule hii ya Nganda Yala kupatiwa cheti cha kutambuliwa kwa usafi. 

Je awali hali ya usafi ilikuwa vipi? Christian Ngwe, mwanafunzi mwenye umri wa miaka 11 na kiranja wa shule anasema, “najisikia vizuri sasa kwa sababu wamejenga vyoo. Najisikia vizuri kwa sababu tulipokuwa tunatumia vyoo vya zamani, wanafunzi wengi waliugua magonjwa. Sasa najisikia vizuri kwa sababu shule yetu imejenga vyoo vipya.” 

Sasa vyoo vya wavulana na wasichana vimewekewa ishara na milango, bila kusahau eneo la maji ya bomba ya kuwezesha wanafunzi kunawa mikono. Halikadhalika kuna tenki kubwa la maji la kusambaza maji safi na salama. 

Ukafika wakati wa Mwalimu Mkuu kukabidhiwa cheti cha Shule yenye Afya pamoja na bendera!! 

Kiranja Christian akafunguka akisema, “ninajivunia shule yetu. Tutaitunza vyema. Tutaipanga vizuri. Tutaondoa uchafu ili hata wale watakaokuja nyuma yetu waendeleze kile tunachokifanya. "