Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yalaani vikali mashambulizi mawili dhidi ya wahudumu wa kibinadamu CAR 

Mlinda amani wa MINUSCA akiwa katika doria nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR-Kutoka Maktaba
MINUSCA/Herve Cyriauqe Serefi
Mlinda amani wa MINUSCA akiwa katika doria nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR-Kutoka Maktaba

UN yalaani vikali mashambulizi mawili dhidi ya wahudumu wa kibinadamu CAR 

Amani na Usalama

Mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa na Naibu Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR, Denise Brown amelaani vikali mashambulizi mawili yaliyofanywa na watu wenye silaha dhidi ya wafanyakazi wa mashirika ya kibinadamu nchini humo. 

Mratibu huyo Bi. Brown amesema “nimeshtushwa na kukasirishwa na mashambulizi hayo mawili yaliyotokea Aprili 7 na Aprili 9 ambapo wahudumu 6 wa maswala ya kibinadamu  na mfanyakazi mmoja wa kituo cha afya cha wilaya walijeruhiwa huku mmoja vibaya sana wakati wakiwa kwenye huduma za kibinadamu Kusini mwa CAR.” 

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo MINUSCA unasema shambulio hilo limelazimisha moja ya mashirika yaliyotiwa hofu kusitisha huduma zake za kliniki zinazohama na shughuli zake zingine za kuboresha upatikanaji wa maji safi kwa watu 11,000 katika maeneo ya vijijini ya mkoa wa Basse-Kotto, wakiwemo watoto wengi na wanawake wajawazito. 

"Kila wakati wasaidizi wa kibinadamu wanaposhambuliwa, maisha ya maelfu ya watu walio hatarini huwa hatarini zaidi. Wafanyakazi wa misaada ambao wanasaidia watu katika mazingira magumu sana lazima walindwe wasishambuliwe”, amesema Bi. Brown. 

Changamoto ya mashambulizi kama haya 

 

Jamhuri ya Afrika ya Kati ni mojawapo ya nchi zenye changamoto nyingi duniani kwa wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu.  

Kwa mujibu wa MINUSCA kati ya tarehe 1 Januari na 15 Aprili 2022, matukio 43 yaliyoathiri mashirika ya kibinadamu yalirekodiwa ambapo wafanyakazi 11 wa misaada walijeruhiwa.  

Kwa mwaka wa 2021, angalau tukio moja kwa siku lililoathiri wafanyikazi wa kibinadamu lilirekodiwa, na nusu ya matukio hayo ikiwa ni wizi, udokozi na uvamizi.  

Matukio haya ya usalama yanatatiza utoaji wa misaada ya kibinadamu, ambayo zaidi ya nusu ya wakazi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wanaitegemea. 

Bi. Brown ameongeza kuwa "raia ndio waathirika wakuu wa vita katika Jamhuri ya Afrika ya Kati na usaidizi wa kibinadamu ni suala la uhai au kifo kwa mamilioni ya watu. Wasaidizi wa kibinadamu wanaokuja kuwaokoa kwa njia isiyoegemea upande wowote na bila upendeleo lazima wapewe fursa ya kuwafikia watu hao na kwa usalama.” 

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kwamba mwaka huu wa 2022, watu milioni 3.1 wanahitaji msaada wa kibinadamu na ulinzi CAR, ambayo ni asilimia 63 ya watu wote.  

Kati ya hao, watu milioni 2.2 wenye mahitaji makubwa hawawezi kuishi bila msaada na ulinzi unaohitajika.  

Shirika hilo limeongeza kuwa licha ya mazingira magumu na hatari ya kufanya kazi, kwa mwaka 2021 pekee wahudumu wa kibinadamu wamesaidia watu milioni 1.8 katika hali za dharura.