Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwaka 2020 ni wa kipekee kwa CAR- UN

Walinda amani wanaohudumu katika MINUSCA huko CAR wakifanya doria katika mji mkuu Bangui
UN photo / Catianne Tijerina
Walinda amani wanaohudumu katika MINUSCA huko CAR wakifanya doria katika mji mkuu Bangui

Mwaka 2020 ni wa kipekee kwa CAR- UN

Amani na Usalama

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hii leo wamejulishwa kuwa mwaka huu wa 2020 utakuwa mwaka muhimu sana na wa kihistoria kwa wananchi na taifa la Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR.

Mwakilishi  Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini CAR, Mankeur Ndiaye amesema hayo wakati akihutubia wajumbe hao waliokutana kupokea taarifa ya Katibu Mkuu kuhusu hali ilivyo kwenye taifa hilo la Afrika.

Bwana Ndiaye amesema kuwa mwaka huu ni muhimu kwa sababu mwezi Desemba wananchi wa CAR watapiga kura kuchagua viongozi wao.

Hata hivyo amesema ni muhimu kuhakikisha kuwa uchaguzi huo unakuwa jumuishi kwa kuwezesha walio ukimbizini kupiga kura sambamba na kuimarisha ushiriki wa wanawake kama wapiga kura na kama wagombea wa nafasi za uongozi.

Mankeur Ndiaye, Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR na Mkuu wa MINUSCA akihutubia Baraza la Usalama kuhusu hali inavyoendelea nchini humo
UN Photo/Loey Felipe
Mankeur Ndiaye, Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR na Mkuu wa MINUSCA akihutubia Baraza la Usalama kuhusu hali inavyoendelea nchini humo

Halikadhalika Bwana Ndiaye amesema kuwa, “pamoja na hiyo kuanzishwa kwa jopo la mashauriano likijumuisha vyama vya siasa, mashirika ya kiraia na mamlaka za umma, jopo ambalo tarehe 17 mwezi huu wa Februari lilikutana kwa mara ya kwanza ni fursa nzuri ya kuhakikisha kuna makubaliano juu ya mchakato wa uchaguzi.”

Lakini amesema kuwa chaguzi hizo hazitaweza kufanyika kwa mafanikio iwapo jamii ya kimataifa haitapatia CAR msaada wa kiufundi, vifaa na kifedha.

Amesema licha ya uhamasishaji wa upatikanaji wa rasilimali muhimu, “natoa wito kwa wadau wa CAR kutekeleza ahadi zao za michato ili kufanikisha mipango ya uchaguzi ya taifa hilo.”

Mwaka mmoja wa mkataba wa amani

Mwakilishi huyo wa Katibu Mkuu ambaye pia ni Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini CAR, MINUSCA, amezungumzia maendeleo chanya nchini humo ikiwemo maadhimisho ya mwaka mmoja yaliyofanyika tarehe 6 mwezi Februari mwaka huu tangu kutiwa saini kwa mkataba wa amani kati ya serikali na vikundi 14 vilivyojihami.

“Maadhimishio hayo yalikuwa ni fursa ya kutathmini mafanikio na changamoto za kutekeleza mkataba huo,”  amesema Bwana Ndiaye

Mafanikio mengine ni kuwepo kwa serikali jumuishi iliyowezesha kupitishwa kwa mkataba huo na kwamba pande zilizotia saini zimeridhia mfumo mfumo huo licha ya changamoto zilizopo.

Halikadhalika amegusia kupungua kwa ghasia dhidi ya raia, kuendelea kuongezeka kwa wigo wa mamlaka ya serikali nchini humo pamoja na usimamizi katika majimbo yote 16 kwenye taifa hilo na kusambazwa kwa jeshi la serikali la taifa na vikosi vya usalama kwenye maeneo ambako awali hawakuwepo.

Pichani  ni  mlinda amani kutoka Misri anayehudumu kwenye ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, akimsaidia raia kuteka maji  kwenye kisima ambacho kimejengwa kwa ufadhili wa MINUSCA.
MINUSCA/Hervé Serefio
Pichani ni mlinda amani kutoka Misri anayehudumu kwenye ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, akimsaidia raia kuteka maji kwenye kisima ambacho kimejengwa kwa ufadhili wa MINUSCA.

Katika hotuba yake ya mwisho mbele ya Baraza la Usalama tarehe 25 mwezi Oktoba mwaka jana wa 2019, Bwana Ndiaye alionya kuwa, “Kucheleweshwa kwa chaguzi zijazo kunaweza kuweka ombwe katika ngazi ya juu ya serikali na kusababisha mpito mwingine wa kisiasa ambao baadhi ya wanasiasa wanautaka lakini ambao unaweza kuathiri uimarishaji wa demokrasia, utulivu na amani CAR.”

Azimio namba 2499 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo limeongeza muda wa MINUSCA hadi tarehe 15 mwezi Novemba mwaka huu, limepatia mamlaka ujumbe huo kusaidia CAR katika maandalizi ya  uchaguzi.

Msaada huo ni pamoja na usalama, operesheni za maandalizi, vifaa kwa kadri itakavyoonekana ni sahihi ikiwemo kuhakikisha maeneo ya ndani zaidi yanafikika.