Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Omicron imedhihirisha dunia inahitaji mtazamo mpya kuhusu magonjwa ya mlipuko:WHO

Muuguzi katika Hospitali maalum ya COVID-19 huko Nasrec, Johannesburg, anavaa PPE yake.
IMF Photo/James Oatway
Muuguzi katika Hospitali maalum ya COVID-19 huko Nasrec, Johannesburg, anavaa PPE yake.

Omicron imedhihirisha dunia inahitaji mtazamo mpya kuhusu magonjwa ya mlipuko:WHO

Afya

Virusi vipya vya COVID-19, Omicron vimedhihirisha kwa nini ulimwengu unahitaji makubaliano mapya kuhusu magonjwa ya milipuko kwani mfumo wetu wa sasa unapuuza suala la nchi kutadhaharisha wengine kuhusu vitisho ambavyo vinaweza kuwakumba amesema mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya duniani WHO.

Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus ameyasema hayo leo mjini Geneva Uswisi kwenye kikao maalum cha dharura cha Baraza la Afya Duniani (WHA) kinachowaleta pamoja nchi wanachama wa WHO kujadili ajenda moja pekee, makubaliano ya mkataba wa WHO juu ya kujiandaa na kukabiliana na janga la COVID-19 kwa kuzingatia ripoti ya kikosi kazi cha kuimarisha utayarishaji na mwitikio wa WHO kwa dharura za Kiafya. 

Wiki iliyopita WHO ilitangaza uwepo wa aina mpya ya kirusi cha OMICRON ambacho shirika hilo limesema ni chakutiliwa shaka huku kikionekana kuwa na nguvu zaidi ya kushambulia kuliko kirusi aina ya Delta. 

Kuhusu mlipuko wa magonjwa 

Dkt. Tedross amesema "Kila mtu anajua kwamba magonjwa ya kuambukiza yana njia ya kutokea mara kwa mara duniani. Kumekuwa na tauni nyingi kama vile vita katika historia, lakini mara zote tauni na vita huwashangaza watu kwa njia sawa." 

Milipuko, magonjwa ya kuambukiza na majanga ya milipuko ni ukweli wa asili, na hulka ya kuzuka mara kwa mara imerekodiwa katika historia kuanzia kwa tauni ya Athene mwaka 430 KK, hadi kifo cheusi, janga la mafua la 1918, na sasa COVID-19.

Lakini amesisitiza kuwa “Hiyo haimaanishi kuwa hatuna uwezo wa kuyazuia, kujitayarisha au kupunguza athari zake. Sisi si wafungwa wa hatima au asili. Zaidi ya wanadamu wowote katika historia, tuna uwezo wa kutazamia magonjwa ya milipuko, kujitayarisha, kubaini vimelea, kuvigundua katika hatua za mapema zaidi, kuvizuia kuenea na kuwa majanga ya kimataifa, na kukabiliana nayo yanapotokea.” 

Lakini cha kushangaza amesema sasa tunaingia mwaka wa tatu wa mgogoro mkubwa zaidi wa kiafya katika karne hii na dunia bado inademadema. 
“Virusi hivi ambayo tunaweza kuvizuia, kugundua na kuvitibu vinaendelea kuleta giza kubwa duniani. Badala ya kukutana baada ya janga hili, tunakutana wakati wimbi jipya la kesi na vifo vinavyoingia Ulkaya likiongezeka na kukiwa na vifo visivyoelezeka na visivyohesabiwa kote duniani.” 

Mlipuko wa Omicron unaonyesjha “Ni jinsi gani hali ambavyo bado si shwari na kwamba ingawa kuna baadhi ya maeneo idadi ya wagonjwa na vifo inashuka , kama kuna kitu kimoja cha kujifunza ni kwamba hakuna ukanda, hakuna nchi , hakuna jamii na hakuna mtu atakayekuwa salama hadi pale kila mtu atakapokuwa salama.”

Mmoja wa Raia wa Uganda akipokea chanjo yake ya kwanza ya Covid-19 huko Hoima, Uganda.
John Kibego
Mmoja wa Raia wa Uganda akipokea chanjo yake ya kwanza ya Covid-19 huko Hoima, Uganda.

Bado kuna sintofahamu kuhusu Omicron 

Ingawa uchunguzi na tathimini zaidi inaendelea kuhusu virusi vipya vya Omicron WHO imeonya kwamba kutokana na mabadiliko ambayo yanaweza kutoa uwezo wa kuepuka kinga na uwezekano wa uambukizaji, uwezekano wa kuenea zaidi kwa Omicron katika ngazi ya kimataifa ni mkubwa.  

Kulingana na sifa hizi, WHO imesema “kunaweza kuwa na ongezeko la siku zijazo la COVID-19, ambalo linaweza kuwa na madhara makubwa, kulingana na sababu kadhaa ikiwa ni pamoja na mahali ambapo mlipuko utazuka. Hatari ya jumla ya kimataifa inayohusiana na VOC Omicron mpya inatathminiwa kuwa ya juu sana.” 

Kwa upande mwingine WHO imesema Afrika Kusini na Botswana zinafaa kushukuriwa kwa kugundua, kupanga na kuripoti haraka aina hii mpya ya virusi na sio kuadhibiwa. 

“Hatupaswi kuhitaji kengele nyingine ya kutuamsha, sote tunapaswa kuwa macho kwa tishio la virusi hivi. Dharura ya Omicron ni kumbusho tosha kwamba ingawa wengi wanadhani tumemalizana na COVID-19, ukweli ni kwamba haijamalizana nasi. Tunaishi katika mzunguko wa hofu na taharuki na tusipoangalia mafanikio tuliyopata yanaweza kutoweka haraka hivyo kibatrua chetu kikubwa kwa sasa ni kutokomeza janga hili” Limesema shirika hilo la afya duniani. 

Usafiri wa ndege kati ya Marekani na Uingereza umepungua kwa kiasi kikubwa wakati wa janga la COVID-19.
UN News/Daniel Dickinson
Usafiri wa ndege kati ya Marekani na Uingereza umepungua kwa kiasi kikubwa wakati wa janga la COVID-19.

Hakuna nchi itakayomaliza janga hili peke yake

WHO imesisitiza kwamba hakuna nchi itakayoweza kumaliza janga la COVID-19 peke yake ushirikiano na mashikamano wa kimataifa unahitajika na hasa usawa wa chanjo.  

Limetoa mfano kwamba hadi sasa zaidi ya asilimia 80% ya chanjo zilizozalishwa duniani zimekwenda kwa mataifa Tajiri ya G20, nchi za kipato cha chini nyingi zikiwa za Afrika zimepokea asilimia 0.6% pekee ya chanjo zote. 

“Chanjo kwa wote sio hisani, ni kwa ajili ya faida ya kila nchi “ Limesema shirika hilo likiongeza kwamba nchi 103 bado hazijafikia lengo la kuchanja watu wake kwa asilimia 40% sababu kubwa hazina fursa ya kupata chanjo hizo na nyingi ziko barani Afrika. 

Hadi sasa COVID-19 imekatili maisha ya watu zaidi ya milioni 5, na hivyo ni vifo ambavyo vimeripotiwa tu inakadiriwa idadi inaweza kuwa kubwa zaidi. 

Kikao kimeafikia kanuni katika maeneo muhimu manne kukabiliana na hali ya sasa: 

•    Mosi: utawala bora ili kuhakikisha hatua za pamoja zinafanyika na fursa ya usawa wa chanjo na nyenzo zingine. 
•    Pili: Ufadhili unaostahili ili kuimarisha kinga ya kimataifa ambayo ni endelevu, yenye ufanisi na inayoenda sanjari na vipaumbele vya kimataifa. 
•    Tatu: Mifumo bora na nyezo kuweza kutabiri, kuzuia, kubaini na kukabiliana haraka na milipuko na uwezekano wa kuzuka majanga ya kiafya. 
•    Na nne: Dunia inahitaji WHO iliyoimarishwa, kuwezeshwa na yenye ufadhili endelevu kuwa kitovu cha mchakato wa kimataifa na masuala ya afya. 

Kwa mantiki hiyo WHO imeweka bayana kwamba “Huu ndio wakati wetu wa kudhihirisha uwezo wetu mkubwa kuliko janga hili, kushinda masuala ya kutoamianiana, na kujenga mfumo ambao una faida kwa wote na kuwaachia urithi bora vizazi vijavyo.”