Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Misri acha kufurusha wasaka hifadhi kutoka Eritrea 

Wahamiaji na wakimbizi wengi wa Afrika wanapenda kwenda Djibouti ni sehemu hususan wale wanaotoka Ethiopia, Eritrea na Somalia
IOM/Alexander Bee
Wahamiaji na wakimbizi wengi wa Afrika wanapenda kwenda Djibouti ni sehemu hususan wale wanaotoka Ethiopia, Eritrea na Somalia

Misri acha kufurusha wasaka hifadhi kutoka Eritrea 

Wahamiaji na Wakimbizi

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wa haki za binadamu wamelaani hatua ya hivi karibuni na inayoendelea nchini Misri ya kufukuza wasaka hifadhi kutoka Eritrea na kutoa wito kwa mamlaka kusitisha mara moja kitendo hicho.  

Wataalamu hao kupitia taarifa iliyotolewa leo jijini Geneva, Uswisi wameeleza hofu yao kwa kile kinachoendelea kuwa msingi wa kutunga sera za kukamata kiholela na kufukuza kwa makundi raia wa Eritrea na wameonya mamlaka za Misri kuwa aina hiyo ya ufurushaji raia ni kinyume na wajibu wa Misri chini ya sheria ya kimataifa.  

Wasaka hifadhi wamekuwa wanakumbwa na mateso, kukosa huduma za msingi, wengine kutoweshwa, kukamatwa kiholela, kunyima chakula na matibabu na usafirishaji haramu, wamesema wataalamu hao. 

Tangu mwezi Oktoba mwaka 2021, mamlaka za Misri zimefurusha takribani raia 68 wa Eritrea wakiwemo Watoto, bila kutathmini hatari ambazo ikiwemo  haki zao za kibinadamu kukiukwa watakaporejea Eritrea. 

“Wengi wa waliorejea Eritrea, hawajaonekana au hawajasikika na yaaminika wanashikiliwa katika maeneo ambayo hawana mawasiliano yoyote,” imesema taarifa hiyo. 

Wataalamu hao wametoa wito kwa mamlaka za Eritrea kutoa taarifa kuhusu waliko wananchi hao huku wakisema kuwa kuna shaka na shuku kubwa kuwa wanaweza kuwa wamepelekwa kwenye uwanja wa mapigano huko Magharibi mwa Tigray. 

Yadaiwa kuwa wasaka hifadhi hao walikuwa wanashikiliwa kwenye vituo vya polisi vilivyofurika watu huko Misri kwa vipindi tofauti tofauti kuanzia miezi michache hadi wengine miaka kadhaa, huku wakinyimwa chakula, matibabu, huduma za maji safi na kujisafi. 

Katu hawakuwahi kupatiwa taarifa kuhusu kile kilichosababishwa waswekwe mahabusu na hawakupatiwa fursa ya kukutana na wanasheria, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, au mamlaka nyingine zinazohusika na kusaka hifadhi. 

Ingawa Misri ni mwanachama wa mkataba wa kimataifa wa wakimbizi wa mwaka 1951, taifa hilo halina mifumo ya kutosha ya kitaifa ya kulinda wasaka hifadhi na hakuna hatua zozote za kisheria zilizochukuliwa kubaini waathirika wa usafirishaji haramu au kuhakikisha ulinzi wao.