Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jumuiya ya kwanza ya Kiafrika ya dawa za mionzi yaundwa kusaidia kupambana na saratani: IAEA 

Mtoto mwenye umri wa miaka miwili anayeugua saratani akifanyiwa vipimo na muuguzi hospitalini nchini Ghana
WHO/Ernest Ankomah
Mtoto mwenye umri wa miaka miwili anayeugua saratani akifanyiwa vipimo na muuguzi hospitalini nchini Ghana

Jumuiya ya kwanza ya Kiafrika ya dawa za mionzi yaundwa kusaidia kupambana na saratani: IAEA 

Afya

Wataalamu kutoka nchi 21 barani Afrika kwa mara ya kwanza wameunda jumuiya ya Afrika ya dawa au tiba ya mionzi (AfrAR) ili kuimarisha uwezo wao na kukidhi vyema mahitaji ya kitaifa ya maandalizi salama na usimamizi wa dawa za mionzi zinazotumika katika kupima, kutibu na kudhibiti saratani na magonjwa mengine. 

Jumuiya hiyo, iliyoanzishwa mwezi uliopita kwa msaada wa shirika la kimataifa la nguvu za atomiki IAEA, Jumuiya ya Sayansi ya dawa za mionzi (SRS) na Jumuiya ya Ulaya ya dawa za nyuklia (EANM), itachangia maendeleo ya wigo wa tiba za mionzi  katika kanda, ambayo kwa sasa inakabiliwa na idadi kubwa ya changamoto.  

Kwa mujibu wa IAEA changamoto hizo ni pamoja na uhaba mkubwa wa wataalamu wa tiba za miozni waliohitimu na kanuni duni za afya ili kuhakikisha ubora na uzalishaji salama wa dawa za mionzi zinazofaa kwa ajili ya tiba kwa wagonjwa.  

Tiba za mionzi zinazotumika kutibu saratani na matatizo ya moyo, figo, mifupa na ubongo, zina kiasi kidogo cha dawa za isotope zenye mionzi na zinahitaji kuzalishwa chini ya hali zilizodhibitiwa kwa uangalifu mkubwa na kupimwa ubora wake kabla ya kupewa wagonjwa.  

Sjhirika hilo linasema hivi sasa, takriban asilimia 70 ya wataalam wa madawa au wafamasia waliohitimu barani Afrika wanafanya kazi katika nchi mbili pekee, Misri na Afrika Kusini. 

Mradi wa IAEA wa kusaidia tiba dhidi  ya saratani katika nchi za kipato cha chini na kati umesaidia mataifa kutekeleza mipango mahsusi ya kutibu saratani
IAEA
Mradi wa IAEA wa kusaidia tiba dhidi ya saratani katika nchi za kipato cha chini na kati umesaidia mataifa kutekeleza mipango mahsusi ya kutibu saratani

Kazi ya jumuiya hiyo mpya 

IAEA imesema jumuiya hiyo itaongeza ufahamu wa dawa za mionzi kama bidhaa za matibabu miongoni mwa wataalamu wa afya barani Afrika, na kuhamasisha wafanya maamuzi kuhusu umuhimu wa huduma za maduka ya dawa za mionzi pamoja na hitaji la udhibiti wake kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.  

Pia itawezesha ushirikiano wa kikanda na kubadilishana mawazo na ujuzi, ili kuongeza uwezo miongoni mwa wataalamu katika bara la Afrika, kupitia majukwaa rasmi ya kisayansi na kitaaluma. 

"Hii ni hatua kubwa iliyofikiwa na nchi wanachama wa Afrika katika suala la maduka ya dawa za mionzi," amesema Shaukat Abdulrazak, mkurugenzi wa idara ya Afrika kwenye shirika la IAEA katika idara ya ushirikiano wa kiufundi wakati wa hafla ya ufunguzi iliyofanyika Rabat, Morocco mapema mwezi Machi.  

“AfrAR imeanzishwa katika harakati za kuwapa wagonjwa barani Afrika fursa ya ufikiaji wa dawa muhimu za mionzi wanazohitaji. Wataalamu wataweza kuunda mtandao na kutathmini kile kinachohitajika kufanywa katika suala la kuimarisha ubora wa utayarishaji na usimamizi wa dawa za miozni barani Afrika.” 

Hatua muhimu katika kuboresha huduma za dawa za mionzi 

Kuanzia mwaka 2018 hadi 2021, mradi wa ushirikiano wa kiufundi wa IAEA ulisaidia nchi chini ya mkataba wa ushirika wa kikanda wa Afrika kwa Utafiti, maendeleo na mafunzo kuhusiana na sayansi ya nyuklia na Teknolojia (AFRA) kuboresha huduma za maduka ya dawa za mionzi hasa katika eneo la maendeleo ya rasilimali watu kupitia elimu na shughuli za mafunzo.  

Mpango mkubwa wa dawa za mionzi kwa nchi zinazozungumza Kifaransa barani Afrika ulizinduliwa na kundi la kwanza la wataalam wa madawa au wafamasia  wanne waliohitimu mwaka jana, huku wengine watano wakitarajiwa kuhitimu mwaka huu.  

Zaidi ya hayo, IAEA inasema wataalamu wengine 35 wa ngazi ya juu wenye ujuzi wa dawa za mionzi  barani Afrika walikamilisha kozi za mafunzo kwa wakufunzi, na hivyo kuimarisha uwezo wa kikanda. 

"Ukosefu wa usawa katika bara zima ni tatizo," amesema Aruna Korde, Mwanasayansi wa dawa za mionzi katika shirika la IAEA.  

Ameongeza kuwa "Uzinduzi wa jumuiya hii mpya sasa, utakuwa na thamani ya ziada ya kusaidia kuongeza upatikanaji wa bidhaa bora za dawa za mionzi kwa wagonjwa kote Afrika." 

Nchi 21 zinazounda jumuiya hiyo ni Algeria, Burkina Faso, Cameroon, Côte d'Ivoire, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, Misri, Ethiopia, Ghana, Kenya, Mauritania, Mauritius, Morocco, Namibia, Niger, Nigeria, Senegal, Afrika Kusini, Sudan, Tunisia, Uganda na Zambia.