Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama la UN lapongeza wito wa kusitisha mapigano uliofikiwa nchini Yemen

Wananwake wakisaka kuni kwa ajili ya mapishi Mokha, Yemen.
©WFP/Hebatallah Munassar
Wananwake wakisaka kuni kwa ajili ya mapishi Mokha, Yemen.

Baraza la Usalama la UN lapongeza wito wa kusitisha mapigano uliofikiwa nchini Yemen

Amani na Usalama

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hii leo limekaribisha na kupongeza wito uliofikiwa wa kusitisha mapigano kwa miezi miwili nchini Yemen.

Wajumbe wa Baraza la Usalama wamesema wito huo uliotolewa tarehe 01 Aprili 2022 na Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen Hans Grundberg utasaidia kupunguza mateso yanayo wakabili wananchi na kuboresha utulivu wa kikanda.

Kusitishwa huko kwa mapigano kutasaidia kupitishwa kwa misaada ya kibinadamu katika njia ambazo zilikuwa hazipitiki sababu ya machafuko kama vile barabara ya Taiz ambayo itaruhusu usafirishaji wa kawaida wa mafuta, bidhaa nyingine muhimu na safari za ndege zitaanza kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa.

Wajumbe wa Baraza la Usalama wametoa wito kwa pande zote zilizo kwenye mzozoz kuchukua fursa hii iliyotolewa na kufikia mapatano na kushirikiana na Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa kufanya maendeleo ikiwa ni kuelekea usitishaji vita kamili na kupata suluhu shirikishi ya kisiasa.

Pia wameeleza kuunga mkono kikamilifu juhudi za mashauriano ya kisiasa zinazofanywa na mjumbe Maalum Grundberg  huku wakisisitiza udharura wa mchakato shirikishi unaoongozwa na Yemen, unaomilikiwa na wayemen wenyewe chini ya mwamvuli wa Umoja wa Mataifa.

Pia wamesisitiza umuhimu wa ushiriki wa kuwa na kima cha chini wa asilimia 30 ya wanawake katika juhudi hizo kama walivyokubaliana katika mkutano wa kitaifa wa mazungumzo katika azimio 2624 la mwaka 2022.

Kikao hicho cha Baraza la usalama pia kimekaribisha juhudi zilizofanywa na Baraza la ushirikiano la Ghuba kwa kuwezesha mazungumzo ya wayemeni wenyewe yaliyozinduliwa wiki iliyopita, kuunga mkono juhudi za Umoja wa Mataifa.

Hata hiyo Baraza hilo limeonesha wasiwasi mkubwa juu ya mzozo wa kibinadamu wa Yemen na kusisitiza hitaji la dharura la kufadhili misaada ya kibinadamu.