Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Hema katika jangwa nchini Mauritania

Sasa hatuna wasiwasi tena mvua isiponyesha:Wakulima Mauritania

Unsplash / Daniel Born
Hema katika jangwa nchini Mauritania

Sasa hatuna wasiwasi tena mvua isiponyesha:Wakulima Mauritania

Tabianchi na mazingira

Mabadiliko ya tabianchi yanaleta madhara kila kona ya dunia ikiwemo kupungua kwa viwango vya mvua na hivyo kuleta usumbufu mkubwa wa wakulima, mathalan nchini Mauritani kiwango cha mvua kilichokuwa kikinyesha miaka 30 iliyopita sasa wanapata robo tu ya kiwango hicho hali iliyowatesa wakulima na wafugaji lakini mradi wa Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo ya kilimo IFAD umewanusuru kwa kuwahakikishia maji mwaka mzima.

Mauritania, nchi inayotambulika kuwa na majangwa na ukame kwa muda wa miaka mitatu mfululizo imeshuhudia upungufu mkubwa wa mvua kutokana na ukame wa mara kwa mara.

Hali hii imesababisha kupungua kwa kiasi kikubwa kwa shughuli za kilimo kwa kuwa wakulima wengi wanategemea mvua kwa ajili ya kilimo ambacho hatimaye huwapatia chakula na cha ziada wanauza kwa ajili ya kipato.

Mratibu wa Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo ya Kilimo IFAD nchini humo Ahmed Ould Amar anasema “mbali na changamoto hiyo lakini wakazi wa Ukanda wa Kusini wanakabiliwa na uhaba wa maeneo ya kilimo kwa kuwa eneo hilo ni la mteremko na mvua na mafuriko vimemomonyoa udongo, huku ukosefu wa maji na uhaba wa chakula vikileta migogoro baina ya wakulima na wafugaji ambao mifugo yao ilikuwa ikiingia katika mashamba ya wakulima na kula mazao.”

Ili kutatua changamoto hizo IFAD kwa kushirikiana na serikali ya Mauritania wamefadhili mradi wa maji unaowezesha wakulima kuendesha shughuli zao mwaka mzima bila wasiwasi kama anavyoeleza Zeinebaou Binti Mohamed mkulima kutoka mkoa wa Ghidimakha

“Mradi huu unatusaidia kutupatia mashine za umwagiliaji, pampu za maji na matangi ya kuhifadhi maji, mbegu za mazao na uzio ili mifugo isiiingie katika mashamba yetu. Pia wametupatia mabomba makubwa ya maji na haya yanatusaidia katika kilimo na tunawashukuru kwa hilo.”

Wakati wananchi wa Mauritania wakifurahia mradi huu Umoja wa Mataifa umesema ni muhimu kila eneo la dunia kuhakikisha wanasaidia kupata suluhu za kudumu za changamoto za maji kama nchini Mauritania kwa kuwa watu bilioni 2.3 duniani kote wanakabiliwa na upungufu wa maji hali inayosababisha njaa na shida kubwa.

Umoja wa Mataifa pia umetahadharisha kuwa ifikapo mwaka 2050 robo tatu ya watu wote duniani wanaweza kuathiriwa na ukame.