Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ofisi ya Haki za Binadamu yafuatilia madai ya ufyatuliaji risasi raia Ukraine 

Mwanamume akitoa makovu katika jengo la makazi Kyiv, Ukraine.
© WHO/Anastasia Vlasova
Mwanamume akitoa makovu katika jengo la makazi Kyiv, Ukraine.

Ofisi ya Haki za Binadamu yafuatilia madai ya ufyatuliaji risasi raia Ukraine 

Amani na Usalama

Tumepokea madai ya kuwa tangu tarehe 24 mwezi Februari mwaka huu, raia wanaokimbia vita nchini Ukraine wanafyatuliwa risasi na kuuawa na vikosi vya Urusi, hayo ni moja ya madai ambayo tunafuatilia. 

Hiyo ni kauli ya Matilda Bogner, Mkuu wa ujumbe wa kufuatilia hali ya haki za binadamu nchini Ukraine, ujumbe ambao  unatoka ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu, OHCHR

Akiwasilisha ripoti ya miezi 6 kuhusu hali ya Ukraine mbele ya Baraza la Haki za Binadamu hii leo huko Geneva, Uswisi, Bi. Bogner amesema wanajeshi wa Urusi wanadaiwa kufyatulia risasi raia wakiwa kwenye magari wakati wanataka kukimbia vita na zaidi ya yote, “tunafuatilia madai mengine kuwa majeshi ya Urusi yanaua raia wakiwemo wanaokusanyika kwa amani.” 

Hata hivyo amesema wamepokea pia madai kuwa katika maeneo yanayosimamiwa na serikali ya Ukraine, raia wanaodaiwa kuunga mkono majeshi ya Urusi au kuunga mkono mitazamo ya Urusi wanauawa. 

Hali tete pia kwa waandishi wa habari 

Katika kipindi hiki cha mwezi mmoja uliopita tumegundua pia jukumu muhimu walilo nalo waandishi wa habari katika kupata taarifa katika mazingira hayo magumu na hatari. “Lakini tumeona, kadri mapigano yanavyozidi, waandishi wa habari na wafanyakazi wa vyombo vya  habari wanazidi kuwa hatarini. Hadi sasa waandishi wa habari na wafanyakazi wa vyombo vya habari 7 wameuawa nchini Ukraine tangu tarehe 24 mwezi Februari na 12 wameshambuliwa huku 6 kati yao wakijeruhiwa. Mwanahabari mmoja hadi sasa hajulikani aliko na mara ya mwisho alikuwa katika eneo lenye mapigano makali,” amesema Bi.  Bogner. 

Mashambulizi ya kijeshi kwenye maeneo ya raia yanaweza kuwa uhalifu wa kivita 

Katika ripoti yake amebainisha pia vikosi vya kijeshi vinatumia silaha za vilipuzi zinazoathiri maeneo yenye watu wengi na silaha hizo ni pamoja na makombora mazito, maroketi na mashambulizi kutoka angani. 

“Makazi binafsi, majengo yenye ghorofa nyingi, ofisi za serikali, hospitali, shule, vituo vya maji na mifumo ya umeme imeharibiwa kabisa huku madhara kwa raia, haki zao za binadamu, ikiwemo haki ya kupata chakula, huduma za afya, elimu na makazi ikiathiriwa,” amesema Bi. Bogner. 

Amefafanua kuwa kiwango cha vifo na majeruhi miongoni mwa raia na uharibifu wa miundombinu ya kiraia ni kiashiria kinachodokeza kuwa misingi ya kutofautisha maeneo na kanuni ya kuchukua tahadhari kabla ya mashambulizi vimepuuzwa. 

“Tarehe 9 mwezi Machi hospitali namba 3 huko Mariupol, iliharibiwa kabisa na uwezekano mkubwa ni kutokana na kombora la angani lililoangushwa na Urusi., raia 17 miongoni mwao watoto na wajawazito walijeruhiwa. Mwanamke mmoja alisaidiwa kujifungua kwa upasuaji punde baada ya shambulio lakini yeye na mwanae walifariki dunia. MAdaktari walimfanyia upasuaji kwa kutumia mshumaa.” 

Bi. Bogner  amesema mashambulizi ya aina hii yanasababisha machungu makubwa yasiyopimika na yanaweza kuwa uhalifu wa kivita hivyo ni lazima yakomeshwe. 

Mashambulizi Ukraine yamerudisha nyuma maendeleo- UNHCR 

Mwakilishi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR nchini Ukraine Karolina Lindholm Billing anasema kwa kipindi cha mwezi mmoja kila kitu kimebadilika Ukraine. 

Bi. Billing anasema “wiki mbili kabla ya kuanza kwa vita, nilikuweko mashariki mwa Ukraine kwa wiki mbili. Nilikuweko huko na Mwakilishi Mkazi wa shirika la Umoja wa Mataifa mpango wa maendeleo duniani, UNDP kwa ajili ya kuzindua na kutembelea vituo vya kijamii kwa ajili ya watoto wenye ulemavu na wazee huko Avdiika na Popasna.” 

Anaamini kuwa vVituo hivyo hivi sasa kama ilivyo kwa makazi mengine binafsi na majengo ambayo wasaidizi wa kibinadamu na wadau wa maendeleo wamesaidia kujenga na kukarabati katika kipindi cha miaka 8 iliyopita, bila shaka vimegeuka vifusi. 

“Mwezi huu umerudisha nyuma maendeleo haya na kuweka vikwazo zaidi kuliko hata ilivyokuwa miaka 8 iliyopita. Hii leo tunakabiliwa na uhalisia wa janga kubwa la kibinadamu ambalo linakua kila sekunde moja inayopita. Ugumu wa hali ya sasa ni kubwa kupindukia,” amesema Mwakilishi huyo wa UNHCR wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi. 

Msichana kutoka Ukraine akipumzika na mbwa wake baada ya kuwasili Medyka, Poland na familia yake.
© UNICEF/John Stanmeyer VII Photo
Msichana kutoka Ukraine akipumzika na mbwa wake baada ya kuwasili Medyka, Poland na familia yake.

Kwa WFP mahitaij ya wananchi wa Ukraine ni mlo, usalama na usafiri 

Kwa upande wake Msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani, WFP mjini Geneva, Uswisi, Tomson Phiri amesema mwezi mmoja tangu kuanza kwa vita nchini Ukraine asilimia 45 ya wakazi wa nchini humo wana hofu ya kupata chakula.  

Bwana Phiri amesema hivi sasa chakula ndio moja ya mambo makuu matatu yanayowatia hofu wananchi hao. Mambo mengine ni usalama na mafuta kwa ajili ya usafiri.  

“WFP inakadiria kuwa mtu 1 kati ya 5 nchini Ukraine tayrai ameibuka na mbinu za kukabiliana na njaa ikiwemo kupunguza kiwango na idadi ya milo kwa siku huku watu wazima wakiamua kula mlo kidogo ili watoto waweze kupata chakula cha kutosha,” amesema Bwana Phiri. 

Mfumo wa usambazaji chakula Ukraine nao umevurugika, na mifumo ya sasa ambayo inapatia mlo makumi ya mamilioni ya wananchi walionasa kwenye mapigano nayo inasambaratika; malori ya mizigo na treni vimesambaratisha, viwanja vya ndege vimepigwa mabomu, madaraja yamebomolewa, maduka makubwa ya chakula yako matupu halikadhalika bohari za vyakula. 

WFP kwa upande wake kwa kipindi hicho cha mwezi mmoja imesambaza chakula kwa watu milioni 3 ndani ya Ukraine na sasa inaweka mifumo ya kurahisisha usambazaji.