Buriani Dkt. Madeleine Albright nimeshtushwa na kusikitishwa na kifo chako :Guterres

23 Machi 2022

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema amepokea kwa mshituko na masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Dkt. Madeleine Albright.

Katika taarifa iliyotolewa na msemaji wake usiku huu mjini New York Marekani Guterres amesema “Kuanzia kumbi za Umoja wa Mataifa hadi uongozi wake wa idara ya mambo ya nje na utetezi kote ulimwenguni, Madeleine Albright alikuwa gwiji wa kufuatilia mambo, mfano wa kuigwa, na bingwa wa hatua za kimataifa na ushirikiano wa kimataifa.” 

 

Katibu Mkuu ameongeza kuwa Bi. Albright ambaye alikimbia Czechoslovakia akiwa mtoto katika mkesha wa vita vya pili vya dunia, aliibuka na kuwa mmoja wa viongozi mashuhuri wa sera za kigeni za Marekani kwa wakati wake. 

 

“Maisha yake ni ushuhuda wenye nguvu wa michango muhimu sana ambayo wakimbizi huleta kwa nchi zinazowakaribisha. Madeleine Albright pia alikuwa rafiki mpendwa. Nilikuwa na fursa ya kufanya kazi naye kwa miaka mingi ndani na nje ya serikali ikiwa ni pamoja na mpango uliolenga kujenga ushirikiano wa kimataifa kwa karne ya 21. Siku zote nilivutiwa na ushauri wake wa busara, uzoefu wa kina aliokuwa nao, maarifa ya kipekee, ubinadamu na utu wake, uchangamfu na akili aliyokuwa nayo”. Amesema Guterres 

 

RPia ametumba rambirambi zake za dhati kwa familia ya Dk. Albright, marafiki, wafanyakazi wenzake, na kila mtu aliyeguswa na maisha yake ya kipekee. 

 

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter