Shukran Nikki Haley kwa ushirikiano mzuri UN- Guterres

9 Oktoba 2018

Msemaji wa Umoja wa Mataifa leo amethibitisha taarifa za kuachia ngazi kwa Mwakilishi wa kudumu wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Nikki Haley ambapo Katibu Mkuu Antonio Guterres amemshukuru kwa kazi na ushirikiano mzuri.

Kufuatia taarifa za kung’atuka kwa mwakilishi wa kudumu wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa,  balozi Nikki Haley, Katibu Mkuu amemshukuru kwa ushirikiano na mshikamano mzurui aliouonyesha. 

Kupitia taarifa ya msemaji wake mbele ya waandishi wa habari mjini New York Marekani  hii leo, Guterres amesema balozi Haley ataondoka rasmi mwishoni mwa mwaka huu.

Uhusiano

Taarifa hiyo imeongeza kwamba Guterres na Haley "kwa muda wote  wamekuwa na uhusiano imara na wenye ufanisi katika kazi, akiwa kama mwakilishi wa kudumu wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa.”

Kwa mujibu wa taarifa hiyo wawakilishi hao wawili “walifanya kazi kwa bidii kuchagiza uhusiano bora kati ya Umoja wa Mataifa na Marekani na kuonyesha thamani ya Umoja wa Mataifa”

Katibu Mkuu amesema anatumai kuendelea kufanya kazi na Balozi Haley hadi mwisho wa muhula wake na pia yeyote atakayekuwa mrithi wake.

Mwakilishi wa kudumu wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Nikki Haley ziarani nchini Sudan Kusini. Picha: UNMISS
Mwakilishi wa kudumu wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Nikki Haley ziarani nchini Sudan Kusini. Picha: UNMISS

Duru za habari

DKwa mujibu wa duru za habari Rais wa Marekani Donald Trump, alitangaza kujiuzulu kwa Haley leo Jumanne katika ikulu ya Marekani, White House mjini Washington D.C, ambapo alisema balozi Haley “Ni mtu mzuri sana ambaye amefanya kazi nzuri”

Naye balozi Haley kwa upande wake amesema “ni heshima kubwa maishani” kuhudumu kama mwakilishi wa kudumu wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa.”

Balozi Haley aliteuliwa na Rais Trump kuwakilisha nchi yake kwenye Umoja wa Mataifa mwezi Novemba mwaka 2016, kufuatia uchaguzi mkuu wa Marekani.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter