Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Angelina Jolie aadhimisha siku ya wanawake duniani na wakimbizi Yemen

Mjumbe Maalum wa UNHCR Angelina Jolie amewasili Yemen tarehe 6 Machi, 2022, kwa ziara ya kusaidia kuonesha athari za mzozo wa miaka saba kwa watu wa Yemen.
© UNHCR/Marwan Tahtah
Mjumbe Maalum wa UNHCR Angelina Jolie amewasili Yemen tarehe 6 Machi, 2022, kwa ziara ya kusaidia kuonesha athari za mzozo wa miaka saba kwa watu wa Yemen.

Angelina Jolie aadhimisha siku ya wanawake duniani na wakimbizi Yemen

Msaada wa Kibinadamu

Mjumbe Maalum wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, Angelina Jolie ameitaka jumuiya ya kimataifa kuongeza uungaji mkono kwenye kutoa misaada ya kibinadamu na kukomesha ghasia nchini Yemen kwakuwa nchi hiyo mbali ya kuwa na machafuko kwa muda mrefu haijafadhiliwa kwa kiasi kikubwa.

Jolie ambaye ni mjumbe wa UNHCR tangu mwaka 2011 yupo nchini Yemen kwenye ziara maalum yakuonesha athari mbaya za mzozo nchini humo uliodumu kwa miaka saba na zaidi ya watu milioni 4 wamekimbia makazi yao.

“Leo, Wananchi wa Yemen wawili kati ya watatu wanahitaji msaada wa kibinadamu ili kuishi , sawa na watu milioni 20. Asilimia 92 ya Wayemeni wote waliokimbia makazi yao hawana vyanzo vya mapato hata kidogo na wanapaswa kuishi kwa chini ya dola 40 kwa mwezi.” Amesema Jolie na kuongeza kuwa

“Mzozo wa muda mrefu wa Yemen umesababisha migogoro mingi inayoathiri kila nyanja ya maisha kwa wananchi wa kawaida. Mzozo huo umesababisha maelfu ya raia kuuawa, kuenea kwa ufukara, njaa na kuporomoka kwa uchumi hali inayowasukuma wananchi wengi wa Yemen ukingoni.”

Mjumbe huyo maalum ametoa wito kwa pande zote kuepuka kuwalenga raia, na kuhakikisha wale wenye kuhitaji misaada wanafikiwa na kunakuwa na njia salama kwa raia kukimbia maeneo yenye migogoro.

Mwanamke aliyekimbia makazi yake na watoto wake wakiwa katika makazi ya muda kwenye pwani ya magharibi ya Yemen.
IOM/Rami Ibrahim
Mwanamke aliyekimbia makazi yake na watoto wake wakiwa katika makazi ya muda kwenye pwani ya magharibi ya Yemen.

Kiwango cha mateso ni kikubwa

Jolie aliwasili Yemen tarehe 6 Machi kwa ziara ya siku tatu amekutana na wakimbizi wa ndani wa Yemen pamoja na wakimbizi wa kaskazini na kusini mwa nchi hiyo.

Jolie alishuhudia athari mbaya ya mzozo huo haswa wanawake na wasichana, ambao ni zaidi ya nusu ya watu waliokimbia makazi. Wakimbizi hao tayari wanakabiliwa na viwango vya ukosefu wa usawa wa kijinsia na ubaguzi.

“Kiwango cha mateso ya wanadamu hawa hapa si cha kufikiria. Kwa kila siku ambapo mzozo wa kikatili unaendelea hapa Yemen, maisha zaidi na zaidi ya watu wasio na hatia yanapotea na watu wengi zaidi wataendelea kuteseka. Tunaishi katika ulimwengu ambao mateso na hofu hutawala vichwa vya habari, lakini ambapo vichwa vya habari kama hivyo vinaweza kusababisha maonesho makubwa ya huruma na mshikamano wa kimataifa.Natumai huruma na mshikamano huu utaenezwa kwa watu wa Yemen, ambao wanahitaji kwa dharura utatuzi wa haraka na wa amani wa mzozo huu pamoja na watu wengine waliokimbilia nchi nyingine kote duniani.”

Mjumbe Maalum wa UNHCR Angelina Jolie alipoitembelea familia ya wakimbizi wa ndani huko Lahj, Yemen
© UNHCR/Marwan Tahtah
Mjumbe Maalum wa UNHCR Angelina Jolie alipoitembelea familia ya wakimbizi wa ndani huko Lahj, Yemen

Aadhimisha siku ya wanawake duniani na wakimbizi

Akiwa kusini mwa Yemen katika mkoa wa Lahj ameshuhudia wakimbizi wa ndani wanaishi katika makazi duni na familia hizo zilimueleza namna walivyopoteza nyumba zao, rizki zao na hata kuzima kabisa ndoto na matumaini ya watoto wao.

 Mudeera, mama wa watoto watano ambaye amekimbia machafuko huko Taiz miaka minne iliyopita amesemahakuna mtoto wake aliyeenda shule, mwenye cheti cha kuzaliwa au aliyepata chanjo. Kila siku anahangaika kuwapatia chakula chochote zaidi ya chai na mkate.

Nako huko Kaskazini mwa Yemen, kwenye eneo la wakimbizi wa ndani, Jolie alikutana na Maryam mwenye umri wa miaka 65, ambaye amekimbia makazi yake tangu 2016 na ambaye alipoteza mumewe kwenye vita. Alimweleza Jolie jinsi wajukuu zake watatu walivyoaga dunia kwa sababu familia haikuweza kumudu huduma ya afya waliyohitaji.