Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vita Yemen yageuza nchi hiyo kuwa jehanam kwa watoto- UNICEF

Mtoto mwenye utapiamlo nchini Yemen akiwa na mama yake kwenye hospitali ya Al-Sadaqah mjini Aden
OCHA/Matteo Minasi
Mtoto mwenye utapiamlo nchini Yemen akiwa na mama yake kwenye hospitali ya Al-Sadaqah mjini Aden

Vita Yemen yageuza nchi hiyo kuwa jehanam kwa watoto- UNICEF

Msaada wa Kibinadamu

Yemeni hivi sasa ni jehanam ya watoto, amesema Geert Cappelaere, Mkurugenzi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Amman, Jordan kuhusu athari za mzozo huo wa Yemen kwa watoto, Bwana Cappelaere amesema “Yemen si jehanam iliyo duniani kwa asilimia 50 hadi 60 ya watoto nchini humo bali kwa kila mtoto wa kike na wa kiume Yemen.”

Amemtaja mtoto Amal Hussein ambaye picha yake iliyotumika katika gazeti moja  nchini Marekani ikionyesha taswira ya watoto Yemen, kuwa amefariki dunia kutokana na utapiamlo uliokithiri, moja ya majanga yanayozingira watoto Yemen.

Mjumbe huyo akatolea mfano mtoto Sara, ambaye amesema amepata ulemavu nusu ya mwili wake kutokana na ugonjwa wa dondakoo, “ugonjwa ambao unazuilika kwa chanjo iwapo mtoto anapata chanjo hiyo kwa wakati. Kwa bahati mbaya, Sara hakupatiwa chanjo hivyo akapata dondakoo. Nusu ya mwili wake umelemaa.”

Bwana Cappalaere amesema anachosikitika zaidi ni kwamba, licha ya kulemaa nusu ya mwili wake hivi sasa, Sara bado anaendelea kusikia mirindimo ya risasi na makombora, “hebu fikiria kile ambacho kimo ndani ya fikra zake.”

Kama hiyo haitoshi amegusia tatizo la utapiamlo uliokithiri au unyafuzi akisema nusu ya watoto nchini Yemen wenye umri wa chini ya miaka mitano wana  unyafuzi. “Huu ni mzunguko unaojirudia. Wajawazito milioni 1.1 au wanawake wanaonyonyesha watoto wana ukosefu wa damu. Wajawazito hawa wanapojifungua wanafahamu kabisa kuwa watoto wao watakuwa na uzito mdogo na hivyo kuendeleza mzunguko huo wa utapiamlo.”

Vijana wakicheza katika magofu shule moja mjini Sanaa Yemen, ambayo iliharibiwa katika mgogoro unaondelea nchini humo.
UN OCHA/GILES CLARKE
Vijana wakicheza katika magofu shule moja mjini Sanaa Yemen, ambayo iliharibiwa katika mgogoro unaondelea nchini humo.

Ameongeza kuwa ni jambo dhahiri kuwa unyafuzi unaathiri maendeleo ya ubongo wa mtoto kwa hiyo “watoto wa Yemen wako hatarini kwa kuwa hawataweza kukua na kustawi kwa kadri ambavyo inatakiwa.”

Hata hivyo amesema licha ya mazingira hayo duni kwa watoto, hawakati tamaa wakizingatia kuwa familia walizozungumza nao, walimu wanaofundisha watoto, madaktari wanaotibu watoto hawajakata tamaa.

“Kwa kuwa hadi sasa hakuna suluhu ya kiuchumi, au hakuna makubaliano ya amani, usaidizi wetu wa kibinadamu lazima uendelee,” amesema Mkurugenzi huyo wa UNICEF kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini akiongeza kuwa “ombi letu kwa jamii ya kimataifa ni kuendelea kuwa wakarimu kwa watu wa Yemen na watoto wa Yemen.”

Ametumia mkutano huo na waandishi wa habari kukumbusha kuwa ingawa kumalizika kwa vita Yemen ni muhimu, bado itahitajika utawala bora il ikuhakikisha maslahi ya watu wote ikiwemo watoto yanazingatiwa.

TUONE AIBU KWA KINACHOENDELEA YEMEN- ANGELINA JOLIE

Katika hatua nyingine mjumbe maalum wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, Angelina Jolie ametoa wito kwa kuwepo kwa makubaliano ya amani nchini Yemen na suluhu la kudumu la mzozo ulioanza nchini humo mwaka 2015.

Bi. Jolie amesema hayo leo huko Korea Kusini aliko ziarani ambako amekutana pia na wakimbizi kutoka Yemen waliopatiwa hifadhi kwenye nchi hiyo ya Asia.

Angelina Jolie akiwa na wakimbizi wa Syria waliopata hifadhi Jordan
UNHCR
Angelina Jolie akiwa na wakimbizi wa Syria waliopata hifadhi Jordan

Amekaribisha mazungumzo ya hivi karibuni ya kusitisha chuki na kutoa wito kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lishirikiane na mataifa ya ukanda wa Mashariki ya Kati ili kusaka suluhu ya kudumu na kuzingatia sheria za kimataifa za kibinadamu kuhusu ulinzi wa raia.

“Kama jamii ya kimataifa lazima tuone aibu kwa kusuasua kuchukua hatua kumaliza janga la Yemen. Tumeangalia hali ikizorota Yemen kiasi kwamba nchi hiyo iko hatarini kuwa na janga la njaa linalosababishwa na binadamu na kupata mlipuko hatari zaidi wa kipindupindu kuwahi kukumba dunia,” amesema mjumbe huyo maalum wa UNHCR.