Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto wanaokimbia Ukraine bila wazazi au walezi walindwe: UNHCR/UNICEF

Mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 7 kutoka mji wa Chernivsti nchini Ukraine ambaye alisikindikiswa  na bibi yake hadi mpakani mwa nchi ihyo na Romania akiwa na virago vyake.
© UNICEF/Ioana Moldovan
Mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 7 kutoka mji wa Chernivsti nchini Ukraine ambaye alisikindikiswa na bibi yake hadi mpakani mwa nchi ihyo na Romania akiwa na virago vyake.

Watoto wanaokimbia Ukraine bila wazazi au walezi walindwe: UNHCR/UNICEF

Wahamiaji na Wakimbizi

Wiki iliyopita zaidi ya wakimbizi milioni 1 kutoka Ukraine walisaka hifadhi katika nchi kufuatia uvamizi wa Urusi dhidi ya taifa hilo la Ulaya ambako miongoni mwao hao mamia ya maelfu ni watoto jambo ambalo linatia hofu kubwa mashirika ya Umoja wa Mataifa, lile la kuhudumia watoto, UNICEF na lile la kuhudumia wakimbizi, UNHCR.


Taarifa ya pamoja iliyotolewa leo katika miji ya New York, Marekani na Geneva Uswisi na viongozi wa mashirika hayo mawili imesema wengi wa watoto hao wanakimbia wenyewe bila walezi wala wazazi na hivyo punde tu wakishapokelewa katika nchi wanamokimbiliwa chonde chonde wasajiliwe na wapatiwe ulinzi.

Catherine Russell ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF na Filippo Grandi, Kamishna Mkuu wa  UNHCR wamesema “watoto wanaovuka mipaka bila uangalizi wa wazazi au walezi wako hatarini kukumbwa na ukatili, manyanayaso, kutumikishwa na kusafirishwa kiharamu. Serikali zihakikishe zinawapatia watoto na familia zao njia salama za kupita wakati wanakimbia ghasia.

Halikadhalika wametaka watoto hao na familia zao pindi wanapoingia katika nchi nyingine wapatiwe eneo salama na waunganishwe na mifumo salama ya kitaifa ya kulinda usalama wao.

Na kwa wale ambao wamekimbia na kuvuka mipaka bila wazazi wao, viongozi hao wanasema serikali ziwajumuishe kwenye mifumo ya kijamii ya malezi ya watoto na kwamba uasili wa watoto usifanyike wakati au baada ya hali ya dharura kama sasa, na badala yake juhudi kwanza zifanyike kuunganisha watoto hao na familia zao pindi inapowezekana, iwapo kuunganishwa na familia zao ndio jambo bora zaidi.

Takribani watoto 100,000, nusu yao wenye ulemavu wanaishi kwenye taasisi na shule za bweni nchini Ukraine na wengi wao wana jamaa na ndugu zao ambao bado wako hai.
“Tumepata taarifa kuwa baadhi ya taasisi zinataka kuhamishia watoto hao nchi Jirani kwa ajili ya usalama. Wakati tunatambua hilo kwamba linafanyika kwa misingi ya kibinadamu, maslahi ya watoto ya kuwa na wazazi na walezi wao lazima yazingatiwe,” wamesema Bi. Russell na Bwana Grandi.