Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shehena ya kwanza ya misaada ya kibinadamu kutoka UNICEF yawasili Ukraine

Maelfu ya raia wa Ukraine wakitafuta usalama katika nchi jirani ya Poland.
© WFP/Marco Frattini
Maelfu ya raia wa Ukraine wakitafuta usalama katika nchi jirani ya Poland.

Shehena ya kwanza ya misaada ya kibinadamu kutoka UNICEF yawasili Ukraine

Msaada wa Kibinadamu

Sehemu ya kwanza ya misaada ya kibinadamu kutoka shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF imewasili leo huko Lviv, magharibi mwa Ukraine, kutoka Kituo cha Ugavi na Usafirishaji cha UNICEF huko Copenhagen, Denmark.  

Taarifa iliyotolewa hii leo mjini Kyiv, Ukraine imeeleza kuwa hii ni sehemu ya msafara wa malori sita yenye takriban tani 62 za misaada ikielekea katika nchi hiyo iliyoharibiwa na vita. 

Misaada hiyo ni pamoja na vifaa vya kuwakinga wahudumu wa afya dhidi ya COVID-19 wanaposhughulikia mahitaji muhimu ya kiafya ya watoto na familia, pamoja na vifaa vya matibabu vinavyohitajika sana, ikiwa ni pamoja na dawa, vifaa vya huduma ya kwanza, vifaa vya ukunga na vifaa vya upasuaji, na huduma kwa watoto wachanga na vitu vingine kwa ajili ya kuburudisha watoto. 

"Hali ya watoto na familia nchini Ukraine inazidi kuwa mbaya," Murat Sahin, Mwakilishi wa UNICEF nchini Ukraine amesema na akiongeza kuwa, "vifaa hivi vitasaidia kutoa msaada unaohitajika kwa wanawake, watoto na wafanyikazi wa afya." 

Kundi la ziada la misaada ikiwa ni pamoja na blanketi 17,000 na nguo za majira ya baridi za watoto pia ziko njiani kupitia Poland kutoka ghala la UNICEF la Ofisi ya Uturuki huko Mersin. 

UNICEF inasema tangu mzozo huo ulipozidi, familia zimekuwa zikijificha chini ya ardhi kwenye mahandaki, bila huduma za kimsingi. Hospitali na wodi za wajawazito zimehamisha wagonjwa wao kwenye vyumba vya chini ya ardhi. Kote nchini, mamia ya maelfu ya watu hawana maji salama ya kunywa kutokana na uharibifu wa miundombinu ya mfumo wa maji. Nchi ina upungufu wa vifaa muhimu vya matibabu na imelazimika kusitisha juhudi za haraka za kupunguza mlipuko wa polio. 

Kitengo cha kushughulikia majanga kwa watoto cha UNICEF Ukraine kimeomba jumla ya dola za Marekani milioni 349 ambazo ni pamoja na dola milioni 276 kwa ajili ya programu zake ndani ya Ukraine na kinahitaji dola milioni 73 za ziada kusaidia watoto katika nchi jirani. 

TAGS: Ukraine, UNICEF