Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nilikeketwa, nikakeketa, nimeyaona madhara nimeacha – Aliyekuwa ngariba

Hawa Hussein Njolo, aliyekuwa anatekeleza FGM, ambaye pia yeye mwenyewe ni muathirika wa ukeketaji.
Screenshot
Hawa Hussein Njolo, aliyekuwa anatekeleza FGM, ambaye pia yeye mwenyewe ni muathirika wa ukeketaji.

Nilikeketwa, nikakeketa, nimeyaona madhara nimeacha – Aliyekuwa ngariba

Haki za binadamu

Ingawa mila hii ya ukeketaji imekuwepo kwa zaidi ya miaka elfu moja, Umoja wa Mataifa unaamini kwamba mila hii iliyopitwa na wakati inaweza kutokomezwa katika kizazi kimoja. Ndio maana Umoja wa Mataifa unajitahidi kutokomeza kikamilifu matendo hayo katika muongo huu kufikia mwaka 2030, kwa kufuata mwelekeo wa Lengo la 5 la Maendeleo Endelevu linalolenga usawa wa kijinsia.

Harakati hizo zimeanza kuzaa matunda. Hawa Hussein Njolo ni mmoja wa walio kuwa ngariba lakini baada ya kupokea elimu na kufahamu kuwa ukeketaji ni jambo bayo, ameacha shughuli hiyo. Warren Bright ambaye ni Meneja Mawasiliano wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu na masuala ya afya ya uzazi, UNFPA nchini Tanzania amezungumza na mwanamke huyo. 

“Mimi ni ngariba aliyetubu na kuacha na pia muathirika wa ukeketaji.” Ndivyo anavyoanza kujitambulisha Hawa Hussein Njolo kutoka kata ya Itaja mkoani Singida, katikati mwa Tanzania.  

Hawa anaeleza kuwa yeye ni muathirika wa moja kwa moja wa ukeketaji kwa sababu alikeketwa akiwa na umri wa miaka 13.  

“Nilikuwa na ufahamu na nilikuwa ninajitambua. Nilipata uchungu sana, ijapokuwa bibi yangu anasema nilivumilia sikulia na hapo ndipo alipoanza kunitumia kuwabana mabinti wengine na pia ndipo aliponifundisha na mimi kuwa ngariba na nikaanza kukeketa.” Anaeleza Bi Njolo kwa majuto makubwa.  

Uchumi, zawadi na sherehe 

Mwanamke huyu anaeleza kuwa ukeketaji unatumiwa kama chanzo cha kipato kwa wale wanaojishughulisha nao. Anasimulia akisema kuwa bibi yake, ambaye ndiye ngariba aliyemrithisha matendo hayo, alikuwa anapokea malipo ya aina mbalimbali ikiwemo mifugo kama ujira wa kufanya kazi ya kuwakeketa wasichana.  

Hawa anaeleza kuwa wasichana ambao wanaandaliwa kukeketwa hushawishiwa kwa kupewa zawadi na kufanyiwa sherehe. “kwa mfano kama huo mwaka kuna tukio la wasichana wanaokeketwa, koo zote zitajiandaa kufanya sherehe na yule binti yao ambaye atakuwa amekeketwa atakuwa amepewa pesa nyingi sana, atakuwa amezawadiwa mbuzi. Kwa hiyo ilikuwa ni mvuto wa kichumi kwa mila yetu.” 

Kukwepa mkono wa sheria 

Serikali ya Tanzania iekuwa ikifanya jitihada za kupinga vitendo hivi vya ukeketaji. Mbinu mbalimbali zinatumika ikiwemo elimu inayotolewa kwa ufadhili wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na wadau wake. Lakini Hawa anaeleza kuwa ngariba wamekuwa wakibuni njia nyingine za kificho ili kukwepa mkono wa sheria. Yeye mwenyewe anakiri kwamba wakati anafanya kazi hii, yeye na wenzake waliacha kukeketa wasichana wenye umri mkubwa na badala yake wakawa wanawakeketa watoto wakiwa na umri mdogo sana, mbinu ambayo inawasaidia kutogundulika na vyombo vya usalama.  

“Nilimkeketa mtoto wa mdogo wangu.” Hawa anaeleza kisa kilichomfanya hadi akafikiria ni wakati sasa aache shughuli hii ya ukeketaji. “Tulikuwa tunaoshea na mkojo. Nilipomkeketa nikasafiri. Mama yake akawa hajamuosha vizuri damu ikaganda ikaziba njia ya mkojo. Ilibidi nishike wembe tena kumrudia, alilia sana.” 

Ilikuwa bahati nzuri kwamba wakati huo pia Hawa alielimishwa kupitia shirika linalopinga ukeketaji ambalo lilianza kwa kuwakusanya ngariba na kuwapa elimu kwa nini ni vibaya kufanya ukeketaji. Pia shirika hilo lifanya mazungumzo na wazee wa mila ambao pamoja na ugumu wa kutotaka kubadilika, lakini wachache waliobadilika walisaidia kufanya matukio ya ukeketaji kupungua ingawa Hawa nasema bado yapo yanaendelea chinichini katika ngazi ya familia ambapo mama, shangazi na bibi wanaweza kushirikiana kumkeketa mtoto siku chache tu baada ya kuzaliwa.  

Kwa mtazamo wa mwanamke huyu aliyembua kuwa ukeketaji una madhara makubwa katika maisha ya aliyekeketwa, anaona kuwa ni bora vita dhidi ya matukio haya iendelee hadi matukio haya yatakapokomeshwa kabisa.