Mangariba wadondosha nyembe na wakumbatia uhamasishaji dhidi ya ukeketaji

6 Februari 2019

Ili kufanikisha vita dhdi ya ukeketaji ni lazima washika dau wote washirikiane ili kuhakikisha kuwa tendo hilo la kikatili linaloendelezwa kwa madai ya utamaduni linatokomezwa.

Miongoni mwa wadau ni mangariba ambao iwapo watadondosha nyembe zao basi vita dhidi ya ukeketaji itakuwa imefanikiwa kwa kiasi kikubwa.

Hali ni kama hiyo kwa mmoja wa mangariba akiwa mkoani Mara nchini Tanzania ambaye awali alikuwa analipwa shilingi Elfu 10 kwa kila mtoto anayemkeketa lakini kutokana na kampeni kutoka shirika la idadi ya watu duniani, UNFPA, nchini  humo sasa anahamasisha jamii kuachana na ukeketaji kama alivyomwelezea Bright Warren wa UNFPA.

Ngariba huyo, bibi Bhoke amesema aliwakeketa mamia ya wasichana wakati akifanya kazi hiyo ambayo inakiuka haki za wasichana, hatahivyi kufuatia mwamko wa serikali na wadau ikiwemo UNFPA kutokomeza ukeketaji aliamua kuwachana na kazi hiyo ambayo kwa maneno yake ilikuwa inamletea kipato tosha.

Bibi Bhoke baada ya kuachana na vitendo hivyo vya kikatili alikata kauli ya kuhamasisha jamii ikiwemo mangariba wenzake kuachana na mila hiyo potofu kwani baada ya kupata elimu alielewa fika kuwa ilikuwa inaathari kwa wasichana waliokeketwa. Bibi Bhoke anasema mangariba wengine watatu wameamua kuweka visu chini na badala yake kujihusisha na kazi mbadala kwa ajili ya kujipatia kipato.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter