Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuko tayari kusaidia waathirika wa machafuko Ukraine:Mashirika ya UN

Mwanamke anasimama katikati ya bustani yake ya waridi huko UkrainE. (Maktaba)
Danish Red Cross/Jakob Dall
Mwanamke anasimama katikati ya bustani yake ya waridi huko UkrainE. (Maktaba)

Tuko tayari kusaidia waathirika wa machafuko Ukraine:Mashirika ya UN

Msaada wa Kibinadamu

Mashirika ya Umoja wa Mataifa lile la mpango wa chakula duniani WFP, la kuhudumia wakimbizi UNHCR na la elimu sayansi na utamaduni UNESCO, pamoja na kutiwa hofu kubwa na kulaani kinachoendelea nchini Ukraine, yamesema yako tayari kusaidia kwa hali na mali waathirika wa machafuko hayo nchini Ukraine

WFP haiwezi kumudu mzozo mwingine

 

Katika taarifa yake iliyotolewa leo shirika la WFP limesema “Wakati Ukraine ikiingia kwenye mzozo, WFP iko tayari kutumwa kwenda kusaidia watu walioathirika. Hatua za kwanza katika dharura za kibinadamu, WFP ina uwezo wa kuingia ndani ya saa 72 baada ya mzozo kuzuka, ili mradi tu fursa imetolewa na rasilimali zinapatikana.”

 

Shirika hilo limekumbusha kwamba kati ya Novemba 2014 na Aprili 2018, WFP iliendesha operesheni mashariki mwa Ukraine, na kuwafikia zaidi ya watu milioni moja kupitia fedha taslimu, vocha za chakula au mgao wa chakula ulionunuliwa nchini humo, unaoendeshwa katika maeneo yanayodhibitiwa na serikali na yasiyo ya serikali.

 

Hata hivyo "Tunatiwa wasiwasi na athari za uhasama kwa uwezo wa kuishi na maisha ya raia," amesema Margot van der Velden, mkurugenzi wa dharura wa WFP.

 

Ameongeza kuwa "Kadiri hali inavyoendelea, kuna haja ya kuhakikisha kuwa jamii zilizoathirika zimeendelea kupata usaidizi wowote wa kibinadamu ambao wanaweza kuhitaji na kwamba usalama wa wafanyikazi wa misaada ya kibinadamu mashinani umehakikishwa”.

 

Shirika hilo la chakula limeongeza kuwa “Hivi sasa kukiwa na hadi watu milioni 276 ambao wana uhaba mkubwa wa chakula au katika hatari kubwa kwenye nchi 81, na milioni 45 tayari wako kwenye hatihati ya baa la njaa, ulimwengu hauwezi kumudu mzozo mwingine.”

 

Wafanyakazi wa WFP katika nchi kadhaa zilizoathiriwa na migogoro wanashuhudia athari mbaya ya mapigano kwa mamilioni ya maisha. Kwa sababu hii, tunatetea diplomasia kama njia pekee ya kutatua matatizo.

 

 

Baada ya mzozo wa silaha kuzuka mashariki mwa Ukraine, idadi ya watu katika mji mdogo wa Novotoshkivske ilipungua.
© UNICEF/Aleksey Filippov
Baada ya mzozo wa silaha kuzuka mashariki mwa Ukraine, idadi ya watu katika mji mdogo wa Novotoshkivske ilipungua.

UNHCR: Hali ya Ukraine ni tishio kubwa

 

Kamishina mkuu wa shirika la Umoja wa UNHCR Filippo Grandi akiongeza sauti yake kwa kinachoendelea nchini Ukraine amesema “Tuna wasiwasi mkubwa kuhusu hali inayozidi kuzorota na hatua za kijeshi zinazoendelea nchini Ukraine. Madhara ya kibinadamu kwa raia yatakuwa mabaya sana. Hakuna washindi katika vita lakini maisha ya watu ndio yatakayosambaratika.”

 

Ameongeza kuwa “Tayari tumeona taarifa za majeruhi na watu kuanza kukimbia makwao kutafuta usalama. Maisha ya raia na miundombinu ya kiraia lazima ilindwe na kulindwa wakati wote, kulingana na sheria za kimataifa za kibinadamu.”

 

UNHCR imesema inafanya kazi na mamlaka, Umoja wa Mataifa na washirika wengine nchini Ukraine na iko tayari kutoa usaidizi wa kibinadamu popote inapobidi na inapowezekana. Kwa maana hiyo, usalama na ufikiaji wa juhudi za kibinadamu lazima uhakikishwe.

 

UNHCR pia inafanya kazi na serikali katika nchi jirani, na kuzitaka kuweka mipaka wazi kwa wale wanaotafuta usalama na ulinzi.

 

“Tuko tayari kuunga mkono juhudi za wote kuchukua hatua kwa hali yoyote ya kulazimishwa kuhama. Kwa hiyo, tumeongeza shughuli zetu na uwezo wetu nchini Ukraine na nchi jirani. Tunasalia na nia thabiti ya kusaidia watu wote walioathiriwa nchini Ukraini na nchi za kanda hiyo.”

 

Jengo lililoharibiwa huko Avdiivka, Donetsk, Ukraine. (Maktaba)
© UNICEF/Ashley Gilbertson
Jengo lililoharibiwa huko Avdiivka, Donetsk, Ukraine. (Maktaba)

UNESCO: Sheria za kimataifa lazima zoheshimiwe

 

Kwa upande wake shirika la UNESCO limetoa wito wa kuheshimiwa kwa sheria za kimataifa za kibinadamu, hasa mkataba wa Uholanzi wa mwaka 1954 wa ulinzi wa mali ya utamaduni katika wakati wa migogoro ya kivita na itifaki zake mbili ya (1954 na 1999), ili kuhakikisha kuzuia uharibifu wa urithi wa kitamaduni katika aina zake zote.

 

Limeongeza kuwa hii pia ni pamoja na wajibu chini ya zzimio 2222 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (2015) “kuhusu ulinzi wa wanahabari, wanataaluma wa vyombo vya habari na wafanyakazi wanaohusika katika hali ya migogoro, kukuza vyombo vya habari vilivyo huru, na visivyo na upendeleo kama mojawapo ya misingi muhimu ya jamii yenye kidemokrasia, na ambayo vinaweza kuchangia ulinzi wa raia.”

 

UNESCO pia inatoa wito wa kuzuiwa kwa mashambulizi dhidi ya watoto, walimu, wafanyakazi wa elimu au shule, na haki ya elimu kuzingatiwa.