Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Wakimbizi wa Ukraine wanaishi katika makazi ya muda huko Krowica Sama

Idadi ya wakimbizi wa ndani Ukraine yakaribia milioni 6.5: IOM

© WHO/Agata Grzybowska/RATS Agency
Wakimbizi wa Ukraine wanaishi katika makazi ya muda huko Krowica Sama

Idadi ya wakimbizi wa ndani Ukraine yakaribia milioni 6.5: IOM

Wahamiaji na Wakimbizi

Mashambulizi yanayoendelea nchini Ukraine kwa takriban mwezi mmoja sasa yamesababisha zaidi ya watu milioni 6.48 kuwa wakimbizi wa ndani nchini humo. 

Idadi hiyo imetangazwa leo jijini Geneva uswisi na shrikia la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM baaada ya kufanya utafiti katika wiki ya tarehe 09 mpaka 16 mwezi huu wa Machi 2022. 

Utafiti huo umeonesha asilimia 13.5 ya wakimbizi hao wa ndani walishawahi kukumbwa na maswahibu kama hayo ya kuyakimbia makazi yao mwaka 2014-2015. 

Wengi wa waliokimbia ni wanawake wajawazito na wanaonyonyesha, wazee, watu wenye ulemavu, watu wenye magonjwa sugu na watu walioathiriwa moja kwa moja na unyanyasaji. 

Mkurugenzi mkuu wa shirika la IOM António Vitorino amesema kiwango cha mateso wanachopitia watu hao kinapita aina yoyote ya maswahibu mtu anayoweza kufikiri yanaweza kumtokea na kwamba kwa sasa kipaumbele cha shirika hilo ni kuwafikishia mahitaji wananchi waliokwama ndani ya nchi hiyo. 

“Timu zetu zimekuwa zikiwafikia maelfu ya watu na kuwapa misaada muhimu, lakini tunahitaji uhasama ukome ili kuweza kuwafikia watu katika maeneo yaliyoathirika zaidi.” Amesema Vitorino

Msaada wa mikate ikishushwa katika hospitali huko Kharkiv, Ukraine msaada kutoka WFP
© WFP
Msaada wa mikate ikishushwa katika hospitali huko Kharkiv, Ukraine msaada kutoka WFP

Simu ya bure kukomesha usafirishaji haramu wa binadamu 

Vitorino ameeleza kuwa wakimbizi wa ndani nchini Ukraine wanahitaji misaada ya kibinadamu ya haraka kwakuwa hali inazidi kuwa mbaya nchini humo nakuhimiza “kusitishwa kwa uhasama ili kuweze  kuundwa kwa njia salama zitakazo ruhusu raia kukimbilia maeneo yenye usalama.”

Amesema shirika lake nimeweka namba za simu za dharura kwenye kila kanda ili kusaidia wananchi wanakimbia mapigano dhidi Urusi ambapo “kati ya tarehe 24 Februari na 16 Machi, IOM Ukraine ilitoa usaidizi kwa  zaidi ya watu 12,000 kupitia namba ya simu ya bure ya kitaifa inayohusika na kusaidia wakimbizi wa ndani."

IOM pia ili kukomesha usafirishaji haramu wa binadamu imeweka nambari ya simu ya kupiga ambayo ni 527 na nibure kwa mtu yeyote kupiga. 
Kupitia namba hizo za simu maswali makuu watendaji wamekuwa wakijibu kutoka kwa wananchi wanaopiga simu ni 
A.    Maelezo ya jumla kuhusu biashara haramu ya binadamu na usafiri salama,
B.    Taratibu za kutafuta hifadhi na kupata hadhi ya ukimbizi, na 
C.    Usaidizi unaowezekana kutoka kwa taasisi za kidiplomasia na mashirika yanayohusika na masuala ya kidiplomasia.

Usambazaji wa mikate ukiendelea ndani ya kituo cha treni huko Kharkiv, Ukraine
© WFP
Usambazaji wa mikate ukiendelea ndani ya kituo cha treni huko Kharkiv, Ukraine

Uratibu wa Misaada

Kwakushirikiana na ofisi inayoshughulikia wakimbizi wa ndani Ukraine, IOM imetoa msaada wa chakula na vyombo ya jikoni katika maeneo mawili ya makazi ya wakimbizi huko Zakarpattia na kutoa vifaa vya usafi katika taasisi nne za kijamii huko Luhansk. 

Hadi sasa, IOM imesambaza zaidi ya mablanketi 18,000 ya joto na vifaa vya usafi 8,000 kwa wakimbizi wa ndani walioko  katika mikoa ya Lviv, Ivano Frankivsk, Dnipro, Mykolaiv na Zakarpattia. 

Wakati vifaa vipya vya misaada ya kibinadamu vinapowasili kwenye ghala za IOM nchini Ukraine kila siku, ugawaji wa ziada unaratibiwa na serikali ya nchi hiyo katika ngazi ya manispaa na mitandao wa washirika.

IOM inaendelea kutoa misaada inayohitajika sana nchini Ukraine na nchi jirani, kwa uratibu wa karibu na mashirika mengine yakibinadamu.