Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunakabiliwa na changamoto kubwa ya amani na usalama Ukraine:Guterres

Mwanamke amesimama katika shule iliyoharibiwa na bomu huko Krasnohorivka, Oblast ya Donetsk, Ukraine.
© UNICEF/Ashley Gilbertson
Mwanamke amesimama katika shule iliyoharibiwa na bomu huko Krasnohorivka, Oblast ya Donetsk, Ukraine.

Tunakabiliwa na changamoto kubwa ya amani na usalama Ukraine:Guterres

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema dunia hivi sasa inakabiliwa na mgogoro mkubwa kabisa wa amani na usalama kuwahi kushuhudiwa katika miaka ya hivi karibuni.  

Guterres ameyasema hayo leo mjini New York Marekani kwenye kikao cha bara Kuu la Umoja wa Mataifa kilichojikita katika hali inayoendelea nchini Ukaine. 

Amewaambia wajumbe wa Baraza Kuu kwamba “uamuzi wa serikali ya shirikisho la Urusi kutambua kile kinachoitwa uhuru wa maeneo fulani ya mikoa ya Donetsk na Luhansk na ufuatiliaji ni ukiukwaji wa uadilifu wa eneo na uhuru wa Ukraine na hauendani na kanuni za mitataba ya Umoja wa Mataifa.” 

 Pia ameongeza kuwa “mikataba ya Minsk ilikuwa ilikuwa manusura katika chumba cha wagonjwa mahututi na tunashukuru kutokana na vifaa kadhaa vya kusaidia kuokoa maisha, lakini vifaa hivyo sasa vimekatwa havifanyi kazi.”. 

Ni wakati wa kujizuia na machafuko 

Katibu Mkuu amesema kuwa “Huu ni wakati wa kujizuia, kutafakari na kupunguza kasi ya machafuko. Hakuna nafasi ya vitendo na kauli ambazo zinaweza kuchukua hali hii ya hatari na kuitumbukiza shimoni. Ni wakati muafaka wa kuanzisha mchakato wa usitishaji vita na kurejea katika njia ya mazungumzo na majadiliano ili kuwaokoa watu wa Ukraine na kwingineko kutokana na janga la vita.” 

Rais wa Baraza Kuu 

Mkutano huo ulifunguliwa na Rais wa Baraza Kuu Abdulla Shahid ambaye ameikumbusha jumuiya ya kimataifa kwamba “msukumo wa kuundwa kwa Umoja wa Mataifa umeandikwa katika maneno ya kwanza ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa  ambayo ni “kuokoa vizazi vijavyo kutokana na janga la vita." 

 Amezitaka pande zote husika kuzidisha mazungumzo yao na kupunguza kasi ya mwelekeo wa sasa kupitia njia ya mazungumzo "Amani ya kudumu haipatikani wala kudumishwa kwa maingiliano ya kijeshi, bali kupitia suluhu za kisiasa," amesema Rais huyo wa Baraza Kuu.